Na,Jumbe Ismailly-Singida
JESHI la polisi Mkoani Singida limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa na vyama vya siasa vilivyosimamisha mgombea wa Urais chini ya mwavuli wa UKAWA,kufanyika nov,03,mwaka huu kwa nchi nzima kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya uchaguzi nchini (NEC).

Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida,Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP) Thobias Sedoyeka aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na taarifa za kiintelejensia kuwa jumanne (leo) vyama vya siasa vilivyosimamisha mgombea wa Urais chini ya mwavuli wa UKAWA katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini nzima Okt,25,mwaka huu vinatarajia kufanya maandamano ya kupinga matokeo.

Aidha kamanda Sedoyeka alifafanua pia kwamba pamoja na kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa,vyama hivyo vinaitaka pia mamlaka husika kumtangaza mgombea wao katika Uchaguzi,Bwana Edward Lowasa wakiamini kuwa ndiye mshindi wa kiti cha Urais.

“Sisi jeshi la polisi Mkoani Singida tunasema kuwa maandamano hayo ni batili na hatuyaruhusu kwa namna yoyote ile huku tukiwataka viongozi wa vyama hivyo kutofanya hivyo kamwe na badala yake watumie njia stahiki za Utawala wa kisheria ikiwemo kwenda kwenye vyombo ambavyo vinawajibika kushughulikia malalamiko yao”alisisitiza kamanda Sedoyeka.

Hata hivyo Kamishna Msaidizi wa polisi huyo alifafanua kwamba uchunguzi unaonyesha kuwa maandamano hayo yatashirikisha makundi mbalimbali ya watu,hususani vijana zaidi na kupita sehemu mbalimbali za Mji kabla ya kuhitimisha katika Ofisi walizolenga.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika kesho(leo jumanne) kuanzia majira ya saa nne asubuhi ambapo yanaweza kuanzia sehemu yeyote itakayopangwa na kuishia katika Ofisi za viongozi wakuu wa serikali ya Mkoa au wilaya.

Aidha Kamishna huyo msaidizi hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwaonya vijana kutojihusisha na maandamano hayo na badala yake linawataka waendelee na kazi zao za uzalishaji mali kwani halitasita kutumia nguvu za ziada pale itakapobidi kitendo ambacho huenda kikaathiri utendaji kazi wao pamoja na watu wengine ambao hawatahusika na maandamano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) Mkoa wa Singida,Shabani Limu alikiri kupokea maagizo kutoka ngazi za juu za chama hicho,na kuongeza kuwa mpaka sasa bado hakuna mafanikio ya kufanyika kwa maandamano hayo kutokana na makamanda wa polisi wa wilaya zote kutoyaruhusu kwa kuhofia uvunjifu wa amani.

“Ni kweli tumepokea taarifa kutoka kamati kuu ya chama kwamba maamuzi ya kamati kuu ni kufanya maandamano nchi nzima kupinga matokeo ya Urais ambayo yametangazwa na Tume ya uchaguzi,nimesambaza taarifa zote kwa viongozi wangu wa wilaya wakawa wamepekela taarifa hizi kwa maafisa
wa polisi wa wilaya zao lakini mpaka leo (jana) na mpaka sasa wakati nikiendelea kuzungumza na nyie maafisa wa polisi wa wilaya wamekataa maandamano haya kwa kudai kuwa maandamano haya hayatakuwa ya amani”alisisitiza.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo anashangazwa na kauli za jeshi la polisi kwa kujihusiaha na utabiri kama waganga wa tiba mbadala kuwa maandamano hayatakuwa ya amani na kuongeza kwamba kazi ya jeshi la polisi ni kulinda maandamano na wala siyo kazi ya jeshi hilo kukataa maandamano.

0 comments:

 
Top