Denmark imeahidi kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika harakati zake za Kiuchumi na Maendeleo kwa lengo la kudumisha uhusiano wa kihistoria wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mpya wa Denmark Nchini Tanzania Bwana Einar Hebogard Jensen wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar akijitambulisha rasmi baada ya kuanza kazi yake ya Kidiplomasia kwa takriban miezi sita sasa.

Balozi Hebogard alisema Denmark na Zanzibar pamoja na Tanzania kwa ujumla zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu mara baada ya Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 jambo ambalo Nchi hiyo imemua kuendelea kusaidia Nyanja za Kiuchumi na Kijamii.

Alisema Denmark kupitia shirika lake la misaada ya Maendeleo la { DANIDA } pamoja na miradi tofauti inayosimamia limekuwa likijikita zaidi katika kusaidia Sekta ya Elimu Nchini.

Balozi Mpya huyo wa Denmark Nchini Tanzania ameelezea kuridhika kwake na mazingirabora pamoja na rasilmali nyingi zilizopo Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Denmark kwa jitihada zake za kusaidia sekta ya Elimu katika kuimarisha majengo ya skuli mbali mbali Unguja na Pemba.

Balozi Seif alisema katika kuendeleza uhusiano wa pande hizo mbili alimuomba Balozi Einar Hebogard Jensen kutumia nafasi yake katika kuwashawishi wawekezaji wan chi kutumia fursa ya uwekezaji hapa Zanzibar.

Alisema Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha uchumi tayari imeshaimarisha miundombinu mbali mbali ikiwemo ile ya Sekta ya Utalii inayoonekana kukua na kusaidia pato la Taifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top