Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameonya kwamba tabia ya baadhi ya Wanavijiji wanaoishi katika ukanda wa maeneo ya uwekezaji wa sekta ya Utalii wa kutiliana saini mikataba katika mfumo wa kienyeji usiozingatia taratibu wa Kisheria umekuwa ukiibebesha mzigo mkubwa Serikali Kuu.

Amesema tabia hiyo hivi sasa imekuwa donda ndugu linaloonekana kuleta migogoro kati ya Wanavijiji na wawekezaji wa Hoteli na Nyumba za Wageni na hatimae kuitia dosari Sekta ya Utalii iliyolengwa na Serikali kusaidia uchumi na kuongeza mapato ya Taifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipofanya ziara ya ghafla ya kukagua athari ya ukuta uliojengwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika fukwe ya Hoteli ya Kitalii ya Palumbo Kambakocho iliyopo katika Kjiji cha Uroa Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Ukuta huo uliojengwa kwa nia ya kuzuia kasi ya mawimbi ya Bahari hivi sasa umeanza kuleta athari kubwa ya Mmong’onyoko wa ardhi unaoelekea katika Makaazi ya Wana Vijiji pamoja na makaburi yaliyopo pembezoni mwa eneo hilo.

Balozi Seif alisema katika hatua za kukabiliana na athari hiyo ameuagiza Uongozi wa Idara ya Mazingira Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi ya Uchunguzi wa Sayansi Baharini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi pamoja na Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja kufanya utafiti wa kina kujua athari ya tatizo hilo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa maamuzi mara baada ya kupokea Ripoti ya uchunguzi huo kama itaelekeza kubomolewa kwa ukuta huo au kupatikana suluhisho jengine la kuhami hali hiyo.

Aliiishauri Kamati hiyo aliyoiunda kuangalia upya mikataba iliyotiwa saini Kati ya Muwekezaji na Wana Vijiji hao itakayoainisha kwamba imezingatia taratibu zote zilizowekwa na Taasisi za uwekezaji miradi ya Utalii hapa Nchini.

“ Tumeanza kubaini matatizo yanayoibuliwa na baadhi ya Wanavijiji wa maeneo ya uwekezaji Utalii kutiliana saini Mikataba ya kienyeji isiyozingatia sheria na matokeo yake ni kuibebesha mzigo mkubwa Serikali Kuu “. Alisema Balozi Seif.

Mapema Kaimu Sheha wa Shehia ya Uroa Bwana Abass Sheha alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Uroa ililalamikia ujenzi wa Ukuta huo tokea mwaka 2009 ambao walielewa kuwa utaleta athari ya Mmong’onyoko wa Ardhi.

Bwana Abass alisema kasi ya maji ya Bahari katika eneo hilo iliyozuiwa na Ukuta huo kwa hivi sasa imekuwa ya kutisha na kuleta hofu kwa wanakijiji hao umaliziaji wake unaelekea katika makaazi ya watu na eneo na makaburi.

Akitoa ufafanuzi wa mradi huo wa ujenzi wa ukuta wa kuzuia kasi ya mawimbi ya Bahari Mkurugenzi wa Hoteli ya Palumbo Kambakocho Bwana Pablo Palumbo alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo umefanywa baada ya makubaliano baina ya Uongozi wa Hoteli hiyo pamoja na Wanavijiji wenyewe.

Bwana Pablo alisema Uongozi wa Hoteli yake ulikuwa na nia safi ya kujenga Ukuta huo kutokana na ongezeko la kasi ya maji katika Bahari ya Hindi ndani ya kipindi cha miaka sita tokea kuanza kwa Mradi wao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top