Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Walimu Nchini bado wataendelea kuwa na dhamana kubwa ya kuwafinyanga wanafunzi katika kuelekea kwenye maadili mema yatakayowavua kutumbukia katika majanga ya migogoro na uvunjivu wa amani.

Alisema walimu ndio wahimili wakubwa wa amani kwa kuwaongoza wanafunzi wao kushinda mitego iliyoelekezwa kwao ambayo mara nyingi kuwashawishi kutumbukia katika matendo maovu.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati akikabidhi Kompyuta Tatu na Printa Moja kwa Uongozi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope pamoja na Skuli ya Sekondari ya Fujoni alizopewa msaada na Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE ya Nchini China kwa ajili ya Skuli zilizomo ndani ya Jimbo lake.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika katika skuli hizo mbili iliambatana pia na Balozi Seif kukabidhi Kompyuta Moja kwa Uongozi wa Madrasat Jamiiya Islamic ya Kijiji cha Mahonda kutekeleza ahadi aliyoupa wakati akizungumza nao.

Balozi Seif alisema suala la amani ambalo linamuhusu kila mwana Jamii halina mbadala hasa katika kipindi hichi Taifa linakoelekea katika uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliahidi kwamba ataendelea kuchangia maendeleo ya Wananchi hasa katika sekta ya elimu kadri fursa na uwezo utakavyomruhu.

Aliwahimiza Wanafunzi wa Skuli hizo kujitahidi kusoma kwa bidii kwa kuongeza nguvu zaidi katika masomo ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayoonekana kuwa na soko kubwa la ajira katika karne hii ya sayansi na Teknolojia.

Alizipongeza juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Walimu, Wazazi na Kamati za Skuli za Kitope na Fujoni ambazo zimesaidia kuzibadilisha Skuli hizo na kufikia katika kiwango kinachokubalika kimasomo.

“ Kitope ni moja ya Skuli inayofanya vyema kipindi hichi baada ya mikakati imara iliyochukuliwa na Walimu na Kamati ya Skuli na mimi nikalazimika kuweka nguvu kufuatia matokeo ya wanafunzi wake kuzorota katika kipindi cha nyuma “. Alisema Balozi Seif.

“ Sekondari ya Fujoni kwa hivi sasa inatunavya uso kutokana na matokeo mazuri ya wanafunzi wake yaliyopelekea kwa sasa kuwa na madarasa ya Kidato cha Tano na Cha Sita. Hongereni Walimu na Wazazi “. Alifafanua Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.

Akitoa Shukrani kwa niaba ya Walimu Wanafunzi, Wazazi wa Skuli hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Kitope Bwana Makame Ali Mussa alisema Balozi Seif ataendelea kupata baraka za Wananachi wa Jimbo lake kutokana na moyo wake wa Kizalendo anaouchukuwa wa kuwasimamia Kimaendeleo.

Bwana Mussa alisema Jimbo la Kitope limepata mafanikio makubwa ya Maendeleo ndani ya Kipindi cha miaka kumi ya Uongozi wa Balozi Seif hasa katika Sekta ya Mama ya Elimu ambayo ndio Mkombozi wa Jamii mahali popote pale.

Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Fujoni Mwalimu Mabrouk Ishaq Daima alisema Msaada huo wa Kompyuta umefika wakati muwafaka kwa vile nusu ya zile zilizokuwa zikitumiwa na Wanafunzi zimechakaa baada ya kutoa huduma kwa muda mrefu.

Mwalimu Mabrouk alimpongeza Balozi Seif kwa umakini wake wa kuongeza nguvu za michango na misaada katika Sekta ya Elimu inayofunza na kulea wataalamu wa fani mbali mbali.

Katika hafla hizo fupi zilizofanyika kwa nyakati tofauti kati ya Skuli ya Kitope na Skuli ya Fujoni Balozi Seif alipata fursa ya kulikagua Jengo la Darasa moja lililkojengwakwa nguvu za Wananchi wenyewe katika Skuli ya Sekondari ya Kitope.

Akikagua Darasa na Vyoo vyake Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kusaidia nguvu kwa kuchangia milango, madirisha, Dari pamoja na rangi ili kukamilisha rasmi ujenzi wa Darasa hilo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top