Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amewakumbusha Wananchi wote Nchini kuelewa kwamba heshima na tabia njema iliyojengeka katika nyoyo za Watu wa Zanzibar kutokana na kupenda ufafiki, amani na utulivu ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Wazanzibari.

Alisema ni muhimu kwa kila Mwananchi kuhakikisha anatoa mchango wake katika kulinda, kuukuza na kuutangaza utamaduni wa Mzanzibari kwa kuzingatia mambo mazuri wanayoyapenda wananchi wenyewe.

Dr. Ali Mohammed Shein alitoa kauli hiyo wakati akilizindua Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibari katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Alisema endapo mkakati wa makusudi utawekwa wa kuwashawishi wageni kuiga mambo ya asili na utamaduni wanaoutembelea bila shaka wageni na watalii hao watavutiwa na kuyapenda na hatimae masuala hayo yatalipatia sifa Taifa hili.

Rais wa Zanzibar Alisema kwamba Zanzibar ina Historia inayowavutia wageni mbali mbali kutokana na Utamaduni wenye mchanganyiko wa mambo mengi jambo ambalo limevipatia heshima ya pekee Visiwa vya Zanzibar.

Alisisitiza jukumu la kila Mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuvikataa na kuvipinga vitendo vinavyotia doa,Desturi, mila na Utamaduni ikiwa ni pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo hivi sasa Serikali inaendelea na juhudi mbali mbali za kuvikomesha.

Aidha alitoa wito kwa Wananchi waendelee kuunga mkono kampeni inayofanywa na Serikali Kuu dhidi ya unyanyasaji wa Kijinsia iliyoianzisha Tarehe 6 Disemba mwaka 2014 isemayo Zanzibar bila ya udhalilishaji wa kijinsia inawezekana.

Dr. Shein aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa kushirikiana na Kamati Maalum ya Maandalizi na Uendeshaji wa Tamasha la Utamaduni la Mzaznzibari kwa kuongeza kasi na ubunifu katika matayarisho yake na kulifanya kuwa bora kila mwaka tokea lilipoanzishwa mwaka 1994.

Alisema nidhahiri kuwa juhudi tiofauti zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha Tamasha hilo ni hatua muhimu katika kuendeleza mila, silka, desturi na utamaduni unatotoa fursa ya kukumbuka na kufahamu mambo yaliyokuwa yakifanywa wazee wa asili.

Alifahamisha kwamba ni vyema waandaaji wa Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari wakafanya juhudi za ziada katika kuwaalika wageni waliowasili Nchini kwa ajili ya Tamasha la Kimataifa la Filam la Nchi za Jahazi kama njia muhimu hya kuutangaza Utamaduni wa Zanzibar na kulipa hadhi Kimataifa Tamasha hilo.

Rais wa Zanzibar alikelezea matarajio yake kwa waandaaji hao ia watafanya juhudi za kutosha za kuweka matangazo katika Mahoteli, Mitandao amoja na sehemu nyengine zinazopendwa na watalii ili wapate fursa za kuona na kuufahamu zaidi Utamaduni wa Mzanzibari.

Alieleza kuwa msimu wa utalii hivi sasa umeanza, hivyo wananchi wanaweza kuyatumia Matamasha kama hayo ikiwa ni vivutio muhimu vya Utalii kama zinavyofanya Nchi mbali mbali Duniani.

Dr. Shein alisema dhana ya Utalii kwa wote inahimiza uhusiano na ushirikiano wa kisekta kwa mujibu wa shughuli za kila mdau ili juhudi za kuutangaza utalii ziendelee kufanywa na sekta zote na faida zinazopatikana ziwafikie Wananchi wote.

“ Wizara inayosimamia Utamaduni inapaswa kushirikiana na Wizara ya uwezeshaji ili wananchi katika makundi yote waweze kuzitumia na kunufaika na fursa zinazoweza kupatikana kwa kuwepo kwa Tamasha la aina hii “. Alifafanua Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na uongozi wa Tamasha hilo kumualika msanii wa muziki wa asili kutoka Comoro Bibi Shamsia Sagar kutoa burdani kwenye tamasha hilo mualiko utakaosaidia kuimarisha uhusiano kati ya Comoro na Zanzibar.

Aliishauri Wizara ya Habari, Utamudni, Utalii na Michezo ifanye juhudi za kasi kwa kualika wasanii wengine mashuhuri kutoka nchi za Mwambao wa Afrika na sehemu nyengine Duniani ambao ushiriki wao utalipa umaarufu Tamasha hilo na hatimae kuwavutia wageni na washiriki wengi zaidi.

Mapema Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Utamaduni na Michezo Zanzibar Nd. Suleiman Mbarouk alisema Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari ni muendelezo wa Agizo la Rais wa Zanzibar la Kuitaka Kamisheni ya Utamaduni na Michezo kusimamia tamasha lifanyike kuanzia Tarehe 19 hadi 25 Mwezi Julai ya kila mwaka.

Nd. Suleiman alisema Tamasha hilo limesimama kwa takriban miaka mitatu sasa kutokana na kuingiliana na Mfungol wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao kwa sasa kiindi hicho tayari kimebadilika na kutoa fursa ya kuendelea na Tamasha hilo kama kawaida.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzindua Tamasha hilo la Utamaduni wa Mzanzibar Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mh. Said Ali Mbarouk alisema Tamasha hilo ni muhimu katika kukirithisha kizazi kipya kuelewa Utamaduni wao wa asili.

Mh. Mbarouk alisema Taifa lisilo na Utamaduni mara nyingi kizazi chake hutumbukia katika matatizo makubwa ya mmong’onyoko wa maadili, upotevu wa mila na silka zao.

Waziri wa Habari alifahamisha kwamba Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar lengo lake kuu ni kuwakumbusha wazazi kurejesha malezi ya heshima kwa kikazi chao kama walivyofanikiwa wao pamoja na mafunzo ya lugha sanifu ya Kiswahili inayokubalika katika jamii pahali popote.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibar ni:- “ Tudumishe Utamaduni wetu katika hali ya amani, utulivu na Umoja “.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar

0 comments:

 
Top