Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake Nchini Jamuhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea kuunga mkono harakati za kiuchumi za Zanzibar katika kuona wananchi wake wanafaidika na mfumo wa kisasa wa mtandao wa mawasiliano.

Ofisa wa Tawi la Kampuni hiyo ya ZTE liliopo hapa Zanzibar Bibi Coco Wang alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi msaada wa Kompyuta Kumi kwa ajili ya wanafunzi wa skuli zilizomo ndani ya Jimbo lake.

Akikabidhi msaada huo wa Kompyuta wenye thamani ya zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 12,000,000/- Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar Bibi Coco Wang alisema Kampuni ya ZTE imejipanga kusaidia zaidi sekta ya elimu ambayo ndio msingi mkuu wa maisha ya mwanaadamu.

Bibi Coco alisema mfumo wa mafunzo katika vyuo na hata baadhi ya skuli za sekondari unaotumika katika Mataifa mbali mbali yaliyoendelea unaweza kutumika hapa Zanzibar endapo itaimarisha zaidi miundo mbinu ya mtandao wake wa mawasiliano ya Compyuta.

Akipokea msaada huo wa Kampyuta Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo kwa moyo wake wa kujitolea katika kusaidia mtandao wa mawasiliano ya kisasa hapa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Kampuni ya ZTE imeonyesha uungwana mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kiasi ambacho unafaa kuigwa na Makampuni mengine makubwa katika kusaidia jamii.

Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ndiyo iliyofadhili mradi wa ufungaji Kamera za kurikodi matukio mbali mbali ya kila siku { CCTV CAMERA } katika eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Ufadhili huo umekuja Zanzibar kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China mwishoni mwa mwaka uliopita.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top