Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Vijana kuwacha mawazo ya kufikiria kwamba ajira pekee itakayowasaidia kuendesha maisha yao ni ile ya Ofisini pamoja na vikosi vya ulinzi ambazo kutokana na wingi wa idadi yao hazitaweza kukidhi mahitaji yao.

Alisema wakati umefika kwa vijana wanaomaliza masomo yao kuanzisha vikundi vya ushirika vinavyojumuisha kazi za amali na Serikali Kuu itakuwa tayari kusaidia nguvu vijana hao katika kuwapatia vitendea kazi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo katika hafla fupi ya Kukabidhi Boti kwa Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “ walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya baada ya kupata mafunzo ya wiki sita katika nyumba ya kurekebisha watu walioathirika na matumizi ya Dawa hizo.

Boti hiyo pamoja na Mashine yake aliyowakabidhi Vijana hao pembezoni mwa Bahari ya Kijiji cha Mangapwani na kushuhudiwa na baadhi ya wananchi wa Vijiji Jirani vimegharimu jumla ya shilingi Milioni 11,000,000/-, kati ya fedha hizo boti ilichongwa kwa shilingi Milioni 7,000,000/- wakati mashine yake imetumia shilingi milioni 4,000,000/-.

Balozi Seif ambae alikuwa akitekeleza ahadi aliyowapa Vijana hao wakati alipowapokea Tarehe 16 Juni 2015 baada ya kumaliza mafunzo yao alisema chombo hicho kwa kiasi kikubwa kitawapa nafasi nzuri vijana hao kuendesha maisha pamoja na Familia zao.

“ Tafadhalini jitahidini kukitunza chombo hicho. Na iwapo kama kitakushindeni basi naomba ni vyema mkanirejeshea kwa kuniuzia mwenyewe “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba na kuwakumbusha vijana hao kujiepusha na uvuvi haramu uliopigwa marufuku na Serikali ambao unaweza kuharibu mazingira na hatimae lile lengo walilolikusudia kulifanya kwa kutafuta riziki ya halali litakosekana.

Akipokea msaada huo wa Boti pamoja na Mshine yake Mmoja wa Viongozi wa Vijana hao Ndugu Kombo Iddi Juma alimshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa jitihada zake anazochukuwa za kusaidia makundi ya jamii hapa Nchini.

Ndugu Kombo alisema msaada huo wa Balozi Seif alioutoa katika kipindi cha mwezi Mmoja tu baada ya ahadi yake umeleta faraja kwao, Familia na hata wana Kijiji cha Fujoni.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi amerejesha Fomu akijiandaa kuomba fursa ya kuwania nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Jimbo Jipya la Mahonda ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Balozi Seif Ali Iddi ni Miongoni mwa Wanachama 11 wa CCM waliorejesha Fomu hizo hadi sasa tokea kuanza kwa zoezi hilo Tarehe 15 Mwezi huu katika kuomba nafasi za Uwakilishi na Ubunge kwenye Majimbo Manne yaliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.

Akipokea Fomu hizo Katibu wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Kaskazini “B” Bibi Subira Mohammed alimtakia Balozi Seif Safari njema kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu ujao kwa nafasi aliyoomba endapo atapata ridhaa ya Chama.

Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar hivi karibuni Wilaya ya Kaskazini “B” hivi sasa ina Majimbo Manne ambayo ni Mahonda, Bumbwini, Donge na Kiwengwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba

0 comments:

 
Top