Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini wanapaswa kuurejesha tena utamaduni wao wa asili wa kufutari pamoja nje ya Nyumba zao kama walivyokuwa wakifanya wazee wa zamani ili kuongeza upendo baina yao.

Ukumbusho huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya futari ya pamoja iliyotayarishwa na Kampuni ya Vitega Uchumi ya Jamani na kuwashirikisha baadhi ya waislamu na wafanyakazi wa Kampuni hiyo iliyofanyika kwenye mkahawa wao wa Palm Tree uliopo Jengo la Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi alisema utamaduni huo ambao kwa hivi sasa umefifia sana na kuonekana nadra katika baadhi ya mitaa hasa Vijijini ulikuwa ukidumisha ushirikiano na mahaba miongoni mwa waislamu wanaofutari pamoja.

Alisema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umejaa Baraka zinazompasa kila Muumini wa Dini ya Kiislamu kuzishiba ambazo hupatikana katika matendo mema ya pamoja yanayofanywa na waumini wenyewe likiwemo hili la futari ya pamoja.

Alieleza kwamba waumini wengi Mjini na Vijijini wanashindwa kubuni njia za kujitafutia futari kutokana na ukali wa maisha na hupata faraja pale waumini wenzao wenye uwezo wanapoamua kuandaa futari na kujumuika nao pamoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kamuni ya Vitega uchumi ya Jamani kwa uwamuzi wao waliochukuwa na kuandaa futari hiyo kwa kushirikisha watu tofauti kitendo kinachopaswa kuigwa na taasisi nyengine zilizopo hapa Nchini.

Balozi Seif akiwa Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali alitumia nafasi hiyo kuukumbusha Umma umuhimu wa Wananchi kuendelea kudumisha amani hasa wakati huu Taifa likielekea katika uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka 2015.

Alisema Wananchi wa Tanzania wanapaswa kujifunza kutokana na makosa na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya wananchi wa Nchi jirani vya kuichezea Amani ambapo kwa sasa wametumbukia kwenye kizaa zaa cha machafuko na mauaji yanayowakumba pia watu wasio na hatia yoyote.

Balozi Seif alifahamisha kwamba amani iliyopo Nchini ndio rasilmali pekee inayomuwajibikia kila Mtanzania kuitunza na kuiendeleza kwa faida ya ustawi wa sasa na vizazi vya hapo baadaye.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wakati mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unakaribia kumalizika aliwatakia siku kuu njema ya Iddi El - Fitri Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi wote kusherehekea kwa amani na upendo wakati utakapowadia.

Mapema Mkurugenzi wa huduma wa Kampuni ya Vitega uchumi ya Jamani Bwana Salim Aidha Fereji alisema Uongozi pamoja na Wafanyakazi wa Kampuni hiyo wamefarajika kutokana na Tabia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ya kuwa karibu na wananchi wa rika tofauti katika kushirikiana nao kwenye mambo mbali mbali.

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hivi sasa uko ukingoni ukikamilisha kumi la mwisho na la Tatu la kuachwa huru na moto lililoambatana na Usiku Mtukufu wenye cheo wa Lailatul - Qadir.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top