Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa misaada kwa wananchi wake wakati wote kwa mujibu wa hali na wakati pale wananchi hao wanapokumbwa na matatizo au kupatwa na maafa ambayo yatahitaji nguvu ya Serikali Kuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kuangalia maafa yaliyowakumba Wananchi wa Kijiji cha Fukuchani Mkoa wa Kaskazini Unguja na kuwapa pole baada ya Nyumba zao kuathiriwa na upepo wa ghafla Jumatano ya Tarehe Mosi Julai majira ya saa Tano asubuhi.

Nyumba zipatazo 32 zimeathiriwa na upepo huo uliovuma kwa dakika tatu tu ukileta mtafaruku kwa wakaazi wa Kijiji hicho cha Fukuchani pamoja na watu waliokuwa wakisafiri kwa njia ya bara bara.

Balozi Seif ambae aliambatana na Uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kaskazini “A” na Mkoa wa Kaskazini Unguja aliangalia athari ya nyumba hizo ambazo sita kati yake zimeharibika Mapaa yake, nyumba 13 maharibiko ya wastani na nyumba 9 maharibiko madogo.

Alisema kutokana na maafa hayo Serikali imelazimika kuwafariji Wananchi hao kwa kuwapatia msaada wa Mabati kwa kadri nyumba husika zilivyoharibika ili kuwapa nguvu ya kuweza kuzifanyia matengenezo na hatimae zirejee katika hali ya kawaida.

Balozi Seif aliwataka Wananchi hao wa Kijiji cha Fukuchani kuendelea kuwa na moyo wa subira katika kipindi hichi kigumu kwao kwani maafa hayo ni matokeo yasiyotarajiwa kwa vile yanatokana na maumbile ya Mwenyezi Muungu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Fukuchani kwa juhudi walizochukuwa katika kipindi kifupi katika kuwasaidia Wananchi wenzao wakati walipokumbwa na majanga hayo.

Balozi Seif alishauri kuendelezwa kwa tabia hiyo njema ambayo kwa kiasi kikubwa husaidia kuleta faraja kwa wale watu wanaopatwa na mitihani ya ghafla isiyotarajiwa.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A” Bibi Sida Moh’d Himid alisema tathmini ya awali iliyofanywa na Uongozi wa Wilaya hiyo ya kuangalia maafa hayo imeonyesha gharama iliyotokana na janga hilo ikikisiwa kufikia shilingi za Kitanzania Milioni 92,000,000/-.

Bibi Sida alisema Uongozi huo ulilazimika kufika mara moja kwenye tukio hilo mara baada ya kuarifiwa ili kuona jinsi gani unaweza kuchukuwa hatua za dharura kuwahudumia Wananchi hao.

Naye Sheha wa Shehia ya Fukuchani Bwana Abdulla Mcha Ame akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuangakia hasara ya majengo hayo alisema upepo huo mkubwa uliovuma ghafla haujawahi kutokea katika Historia ya Kijiji hicho.

Sheha Abdulla alisema Dakika Tatu za kizaa zaa hicho zimesababisha shughuli zote za kimaisha zilizokuwa zikiendelezwa na Wananachi hao kulazimika kusimama ghafla.

Katika ziara hiyo ya kuwafariji Wananchi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi Bati elfu 1,000 kwa Wananchi waliokumbwa na maafa hayo, ambapo nyumba sita Kubwa zilizoezuka paa lote wakazi wake wamekabidhiwa Bati 70 kila Mmoja.

Nyumba Tisa Ndogo ndogo zilizoezuka mapaa yake zikabahatika kukabidhiwa Bati 30 kila nyumba na zile zilizoezuka bati chache zimekabidhiwa kwa mujibu wa athari ilivyotokea ikiwemo Skuli ya Fukuchani ambayo imeezuka mabati machache.

Balozi Seif pia akakabidhi mchango wake binafsi wa shilingi 50,000/- kwa kila familia ya nyumba 32 zilizopata na athari pamoja na msaada wa vyakula kwa ajili ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoendelea ukiwa katika kumi la Pili ya kuachiwa huru na moto.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top