Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kujenga utamaduni wa kufutari pamoja ili kudumisha utaratibu uliotiliwa nguvu na Kiongozi wa Dini hiyo Mtume Muhammad { SAW } na kuendelezwa na maswahaba waliomfuata.

Balozi Seif ametoa sisitizo hilo kwenye hafla ya Futari ya pamoja aliyowaandalia Watoto Yatima wanaolelewa katika Kituo cha malezi ya Watoto yatima cha Kiislamu cha Rahman Kiliopo Chang’ombe Mjini Dodoma.

Futari hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Dini ya Kiislamu wa Mji wa Dodoma wakiambatana na baadhi ya Viongozi wa Serikali na Kisiasa ilifanyika katika Makazi yake yaliyopo Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma.

Balozi Seif alisema mijumuiko hiyo ya waislamu mara kadhaa husaidia kuongeza upendo, ushirikiano na mahaba baina yao jambo ambalo huongeza nguvu za pamoja katika jitihada zao za kusimamisha Dini ya Mwenyezi Muungu.

Akiwapatia sadaka katika kujiandaa kusherehekea siku kuu ya Iddi El - Fitri wanafunzi hao wa Chuo cha Malezi ya Kiislamu ya watoto Yatima cha Rahman Balozi Seif aliwaombea kusherehekea siku kuu hiyo kwa amani,salama na upendo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya waalikwa wa futari hiyo Sheikh Shaaban Kitila wa Masjid Nunge alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa ukarimu wake wa kuwakusanya wauminbi wenzake kwenye futari ya pamoja.

Sheikh Kitile alisema kufutarisha ni jambo la sunna lililosisitizwa na
Mtume Muhammad { SAW } linalotoa nafasi kwa waumini wa dini ya Kiislamu wasio na uwezo kupata futari inayoleta faraja kwao.

Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Rahman kinachosimamiwa na Ustaadhat Rukia Khamis { Maarufu Mama Abdullah } kimeanzishwa mwaka 2007 kikiwa na wanafunzi 20 ambapo hivi sasa kinahudumia watoto yatima wapatao 70.

Balozi Seif amejiwekea utaratibu wa kufutari pamoja na Watoto hao wa Kituo cha kulelea Watoto yatima Mjini Dodoma napokuwa katika shughuli zake za kikazi akiwa Mjini Humo ndani ya Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wakati Kumi la Pili ya Maghfira likimalizika na kuingia kumi la Mwisho la Kuachwa huru na Moto ndani ya Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Radhani waumini wa Dini ya Kiislamu wamekuwa wakiendelea kujumuika katika futari ya pamoja katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top