Zanzibar inatarajia kuimarika zaidi kiulinzi na kiusalama sambamba na kuongeza mapato yake kupitia sekta ya utalii baada ya kukamilika kwa mradi muhimu wa Kamera za kurikodi matukio mbali mbali ya kila siku { CCTV CAMERA } zinazofungwa katika eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Mradi huo muhimu wa Camera uliofadhiliwa na Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE yenye Makao Makuu yake Nchini Jamuhuri ya Watu wa China umekuja Zanzibar kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya Nchini China mwisho mwa mwaka uliopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kukagua Kituo cha mradi huo { Comanding Post } kiliopo Malindi Mjini Zanzibar na kujionea Teknolojia mpya itakayotumika katika kuziongoza Kamera hizo.
Katibu wa Kamati ya Wataalamu ya usimamizi wa Mradi wa CCTV Camera Nd. Jabir Haji Abdulla alimueleza Balozi Seif kwamba mradi huo unatarajiwa kuwa na Carema 300 lakini zitakazofungwa kwa sasa ni Kamera 150 ambapo hadi sasa Kumi tayari zimeshafungwa.
Nd. Jabir alisema Kituo hicho kitakachokuwa chini ya uangalizi wa Idara zote za ulinzi Nchini likiwemo Jeshi la Polisi, usalama wa Taifa, KMKM hivi sasa tayari kina uwezo kamili wa kurikodi matukio mbali mbali yanayotokea katika eneo la Mji Mkongwe.
Katibu huyo wa Kamati ya Wataalamu ya usimamizi wa mradi huo alieleza kwamba Kamera za mradi huo zenye uwezo wa kuvuta tukio kwa zaidi ya mita 150 zitasaidia kurikodi matukio mbali mbali kama ujambazi, makosa ya bara barani yanayofanywa na madereva wazembe pamoja na kuongoza misafara ya viongozi wakuu.
Alifahamisha kwamba katika kuimarisha hali ya usalama ndani ya Mji wa Zanzibar upo mradi mwengine unaotarajiwa kusimamiwa na Kampuni ya Zest utakaohusisha maeneo ya Bagharesa, Mlandege pamoja na Majengo ya Nyumba za Maendeleo Michezani.
“ Kamera hizi zenye uwezo wa kuzunguuka pembe zote { 360% } zina uwezo wa kuvuta tukio lolote kwa zaidi ya Mita 150 na kuwa na vigezo vya kuufanya mji salama “. Alifafanua Katibu huyo wa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa CCTV.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Kampuni ya ZTE kwa jitihada ilizochukuwa za kutekeleza kwa vitendo ahadi iliyompa kuanzisha mradi huo wakati wa ziara yake Nchini China.
Balozi Seif alisema Serikali ilipaswa kuwa na mradi huu muhimu kwa muda mrefu uliopita hasa ikilinganishwa na matukio mbali mbali yaliyowahi kutokea hapa nchini likiwemo la hujuma dhidi ya wageni wanaotembelea katika maeneo ya Utalii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea matumaini yake kwamba mradi huo kwa kiasi kikubwa utakapokamilika utasaidia kupunguza matukio tofauti ya uhalifu, ujambazi pamoja na ajali za kizembe zinazotokea bada barani.
Mradi wa Kamera za kurikodi matukio mbali mbali ya kila siku { CCTV CAMERA } ndani ya Mji wa Zanzibar umeripotiwa kuwa wa mwanzo kuwekwa ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment