Na,Jumbe Ismailly,Ikungi
TUME ya taifa ya uchaguzi imetakiwa kuhakikisha inasambaza mashsine za BVR za kutosha kwenye vituo vya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,ili kuwawezesha watu wote wenye sifa za kujiandikisha wanaojitokeza kwenye vituo hivyo wanaandikishwa,ili waweze kupata uhalali wa kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini kote oktoba,25,mwaka huu.
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki (CHADEMA),Tundu Lissu ametoa ushauri huo kwenye kituo cha kujiandikishia kilichopo katika shule ya sekondari Ikungi,iliyopo mjini hapa,wakati alipokuwa akitembelea vituo vya kujiandikisha kwa lengo la kuhamasiaha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.
Alifafanua mbunge huyo kwamba ili suala hilo liweze kufanikiwa,tume hiyo haina budi kupelekeka mashine za kutosha kwenye vituo vyenye idadi kubwa ya watu wanaojitokeza kwa ajili ya zoezi hilo la kujiandikisha.
“Kuna matatizo mashine hizi zinaharibika haribika sana ,hivyo ni muhimu kuwepo mafundi kwa muda wote karibu na hizi mashine ili zinapoharibika,ziweze kutengenezwa”alisisitiza Mbunge huyo aliyekuwa katika ziara ya kutembelea vituo kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.
“Kuna baadhi ya maeneo yenye matatizo,na sasa hivi nimetoka kwenye Kijiji cha Matongo na katika Kata hii ya Ikungi,Matongo ndiyo Kijiji kikubwa zaidi na kina watu wengi zaidi kuliko hapa Ikungi,lakini Matongo ina mashine moja tu na tangu jana watu wamelala kwenye kituo na nimekwenda sasa hivi kuna watu karibu mia nne hawajaandikishwa,jana walianza saa nane mchana,siku ya kwanza wameandikisha watu 74 kwa kuwa mashine ilikuwa imeharibika”anasema mbunge huyo.
Hata hivyo alifafanua pia kwamba amepata taarifa kwamba katika Kijiji cha Nkuhi kuna mashine moja wakati Kijiji hicho ni kikubwa kuliko vyote vya kata ya Isuna na kwamba Kijiji cha Ng’ongoosoro kuna hali mbaya pia na hivyo ndiko alikokuwa akielekea kutembelea.
Naye Miss Tanzania 2006,Wema Sepetu aliyekuwa akijiandikisha kwenye kituo cha shule ya sekondari Ikungi,akijibu swali la kwa nini ameamua kwenda wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida kujiandikisha,badala ya kujiandikishia Dar-es-Salaam,alisema amelazimika kufanya hivyo kwa sababu Ikungi ni nyumbani na mama yake mzazi pia ametokea Ikungi ndiyo maana amechagua kwenda hapo.
Hata hivyo Sepetu ambaye pia ni msanii wa Filamu za Bongo Movie hakusita kuweka bayana kuwa kitu chochote kizuri na chenye manufaa pamoja na maendeleo hakina budi kuanzia nyumbani,na ndiyo maana yeye amerudi nyumbani.
Aidha msanii huyo hata hivyo alitumia fursa hiyo ya kujiandikisha kuwahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na hatimaye kupiga kura ili waweze kumpata kiongozi atakayekuwa na uwezo wa kuwawakilisha kikamilifu,hususani kwenye vyombo vya juu vya maamuzi.
Wema ambaye hakuwa tayari kuweka bayana iwapo lengo lake la kwenda kujiandikisha Ikungi ni pamoja na kutaka kugombea nafasi moja ya ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Singida,alitoa ufafanuzi juu ya kauli yake aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM wilaya ya Ikungi kuwa mcheza kwao hutunzwa,kuwa huwa ni msemo wa kiswahili tu na haukuwa na maana yeyote nyingine ile.
“Nimesema mcheza kwao hutunzwa kwa sababu mimi nimetoka Dar kuja kwetu,unaona..kwa hiyo hiyo ni methali tu ambayo nimeitumia ambayo imeendana,…sidhani kama kuna maana nyingine zaidi ambayo natakiwa kuilezea sana ,kwani methali yenyewe inajieleza”alisisitiza kwa kujiamini.
Alipotakiwa kuzungumzia changamoto walizokumbana nazo kwenye zoezi hilo la kujiandikisha,Mwandishi msaidizi kata ya Ikungi na Unyahati,Renatusi Chrispini Kilavi alikiri kwamba siku ya kwanza walifanikiwa kuandikisha watu 425 baada ya kuongeza mashine tatu badala ya moja iliyokuwepo awali.
“Kwa kata ya Ikungi wana vituo vinne na kwa kata ya Unyahati wana vituo vitano na kufanya jumla ya vituo tisa,kwa hiyo zoezi linaendelea vizuri licha ya kuwepo changamoto,lakini siyo za kusimamisha zoezi,ni printer zinasumbua lakini zinafanyiwa matengenezo na zinaendelea na kazi”alisisitiza msimamizi huyo wa vituo.
0 comments:
Post a Comment