Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haipendelei kuona Wananchi katika baadhi ya shehia wanalumbana na kufikia hatua ya kuhitilafiana katika mambo ambayo wakiamua kukaa pamoja katika kuyajadili kwa njia ya vikao yanaweza kurekebishika bila ya kutumika nguvu za Serikali Kuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wazee na Viongozi wa Shehia za Muyuni “A “ na Muyuni “B” katika kikao cha kujadili matatizo yaliyojitokeza baina ya Wananchi dhidi ya viongozi wao wa shehia hizo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema tabia ya baadhi ya wananchi hasa Vijana kutumia njia ya mkato katika maamuzi yao ya kurejesha Kadi za uanachama ni udhaifu unaofa kuepukwa kwa vile hauwezi ukatoa suluhu ya tatizo linalolalamikiwa na Wananchi hao.
Alisema maisha ya amani na utulivu ndio yanayotegemewa na Serikali Kuu kuendelea kushamiri ndani ya Shehia hapa nchini ambazo zinawajibika kufanya kazi kwa umakini.
Balozi Seif alieleza kuwa Sheha wa Shehia yoyote ile hapa Zanzibar ni mtumishi wa Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar asiyepaswa kuhusika na vitendo vinavyoashiria vurugu ndani ya eneo lake.
Mapema Diwani Mstaafu wa Wadi ya Muyuni Bwana Abdulla Hijja Abdulla ambae ndie mwenyekiti wa Kikao hicho alielezea matatizo mengi yanayowasumbuwa Wananchi hao wa Muyuni “ A “ na Muyuni “ B “ hasa lile la hifadhi ya msitu ambalo waliamuwa kuianzisha kwa hatma yao ya baadaye.
Bwana Abdulla alisema uchelewaji wa kuchukuliwa hatua za kisheria katika ngazi za Shehia, Wilaya na Mkoa dhidi ya watu waliomua kuvamia hifadhi hiyo ndilo tatizo kuu lililoibua mtafaruk kati ya Wananchi hao wa Uongozi wa Shehia hizo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kusini Nd. Khamis Jabir Makame alisema alilazimika kulitembelea eneo la Mgogoro wa Ardhi katika eneo la Hifadhi ya Muyuni muda mfupi uliopita ili kujionea hali halisi ya kile kinacholalamikiwa.
Nd. Jabir alikieleza kikao hicho kwamba akiwa pamoja na Viongozi wenzake wa Wilaya alibaini kuwepo kwa miti ya kudumu iliyooteshwa kwa muda mrefu katika eneo hilo pamoja na Miti ya matunda ambayo tayari imeaanza kuzaa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment