Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar kwa kazi kubwa unayoifanya katika kuendeleza sekta ya michezo hapa Nchini.
Alisema Wizara hiyo imesimamia vyema katika kurejesha michezo mingi kwenye ukawaida wake tokea mwaka 2010 na kuiomba isimamie pia kuurejesha mchezo wa Vinyoya { BEDMINTON } ambao umeiletea sifa kubwa Zanzibar Kimataifa katika miaka ya nyuma.
Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa Timu 10 za Waume na Tano za Wanawake za Mchezo wa Vikapu { Basketball } vilivyotolewa msaada na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein.
Vifaa hivyo alivyovikabidhi kwa Viongozi na wanamichezo hao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar ni pamoja na Seti za Jezi,mipira, Viatu pamoja na soksi.
Balozi Seif aliwaeleza Viongozi na Wanamichezo hao wa Mchezo wa Kikapu kwamba Michezo mingi imerejea katika uhalisia wake kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 iliyotilia mkazo uimarishaji wa Sekta ya Michezo Nchini.
Alifahamisha kwamba Zanzibar ilibahatika kuwa na aina mbali mbali ya Michezo tokea katika miaka ya 50 na baadhi yao kufifia katika miaka ya 80 na 90 jambo ambalo limechangia kuporomoka kwa umaarufu wake katika Nyanja ya michezo Kimataifa.
“ Yale mambo ya michezo hivi sasa yanaonekana kurejea kutokana na kutiliwa mkazo ndani ya Ilani na Sera ya Chama Tawala cha CCM ya Mwaka 2010 “ . Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar waliwapongeza Viongozi wa Mchezo wa Kikapu Zanzibar kwa umahiri wao wa kuendeleza mchezo huo uliokuwa maarufu ndani ya Bara la Amerika.
Alisema mchezo wa Kikapu hivi sasa umekuwa maarufu hapa Nchini unaoonekana kutabiriwa kuwa na wachezaji maarufu wanaoelekea kuwa kama akina Jordan wa Marekani.
Balozi Seif alisisitiza kwamba katika kuhakikisha sekta ya michezo inaendelea kuimarika alisema Serikali kwa upande wake itajitahidi kutafuta mbinu na wafadhili wa kusaidia mafunzo sambambana na walimu wa michezo tofauti.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Dr. Ali Saleh Mwinyikai alisema miongozo ya kazi iliyokabidhiwa Wizara hiyo kupitia Dira ya Ilani ya Mwaka 2010 ndio iliyopelekea mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta ya michezo hapa Zanzibar.
Dr. Mwinyikai alisema kwamba utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo katika kuimarisha Sekta ya Michezo umefikia zaidi ya asilimia 98% ya lengo lililokusudiwa kwa kuungwa mkono na Serikali Kuu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar {BTMZ } Sharifa Khamis alisema bado sekta ya michezo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zinazosababisha kudumaza kwa baadhi ya michezo Nchini.
Mwenyekiti Sharifa alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya michezo, miundo mbinu mibovu ya sekta hiyo hasa kwenye viwanja, Ufinyu wa mafunzo pamoja na ukosefu wa mashindano ya Kimataifa ya mechi za Kirafiki kwa timu za Zanzibar.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Viongozi wa wanamichezo hao Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Vikapu Zanzibar Ramadhan Khamis amemshukuru Rais wa Zanzibar pamoja na Balozi Seif kwa juhudi zao wanazozichukuwa katika kuunga mkono sekta ya Michezo Nchini.
Ramadhan alisema juhudi za viongozi hao wa Kitaifa ndizo zilizopelekea na kuchangia kwa kuibuka kwa Vipaji vya wanamichezo katika michezo tofauti pamoja na Zanzibar kujiwekea rikodi nzuri za ushindi katika mashindano ya Kimataifa.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Basketball Zanzibar alieleza kwamba wanamichezo hao wataendelea kuwaunga mkono Viongozi hao katika kuhakikisha kwamba wanafanikiwa katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi wote.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment