Na: Hassan Hamad, OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amefanya ziara ya kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa na wafiwa katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika ziara hiyo Maalim Seif amewaombea wagonjwa hao kuweza kupona haraka, ili waweze kuungana na wananchi wengine katika shughuli za kimaisha, sambamba na kuwataka wale waliofiwa kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Miongoni mwa vijiji alivyotembelea katika mkoa huo ni pamoja na Muyuni, Kizimkazi, Kajengwa, Uroa, Binguni na Kiboje.
Hii ni ziara yake ya kwanza ya kutembelea wagonjwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhan, katika utaratibu wake wa kutembelea wagonjwa na wafiwa kila ifikapo mwezi wa Ramadhan, ziara ambazo huzifanya katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amejumuika na wananchi mbali mbali katika futari ya pamoja nyumbani kwake Mbweni, aliyoiandaa kwa ajili ya watendaji wa vyama vya siasa.
Amewashukuru wananchi hao kwa kuamua kushirikiana nae katika futari hiyo, jambo ambalo amesema linaonesha mapenzi na mshikamano miongoni kwa waislamu.
Maalim Seif ametoa wito kwa waislamu nchini kuendeleza utamaduni wa kualikana na kufutari kwa pamoja, kitendo ambacho hukuza na kuendeleza umoja na maelewano kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment