Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar itaweza kushinda vita dhidi ya udhalilishwaji wanawake na watoto iwapo kutakuwa na nguvu ya pamoja kati ya Serikali, jumuiya za kiraia na jamii nzima katika kuvitokomeza.

Maalim Seif amesema hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar, waliofanya naye mazungumzo huko nyumbani kwake Mbweni mjini Unguja, kuhusiana na shughuli wanazozifanya.

Amesema mbinu muafaka ya kutokomeza vitendo hivyo ni kufanyika utafiti wa kina ili baadaye wadu wote wakiwemo Polisi, Mahkama, viongozi wa dini, wana jamii na Serikali kuwekewa mkakati maalum katika kufanikisha wajibu wa kila upande.

Maalim Seif amesema hali ya udhalilishwaji wanawake na watoto Zanzibar imefikia katika kiwango cha kutisha na nilizima hatua zinazochukuliwa na taasisi mbali mbali, ikiwemo TAMWA Zanzibar ziungwe mkono kwa nguvu zote.

Makamu wa Kwanza wa Rais amekipongeza Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar kutokana na kazi nzuri ya kupigiwa mfano yanayoifanya kuelimisha jamii kukomesha vitendo vya udhalilishwaji wanawwake na watoto.

“Kuishawishi jamii na hasa wanaume waachane vitendo hivi si kazi rahisi, lakini nyinyi mnaifanya kwa ufanisi, nadhani hatua mliyofikia sasa ni ya mafanikio makubwa”, alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Naye Mratibu wa TAMWA Zanzibar, Mzuri Issa amesema mbali na kupiga vita vitendo vya udhalilishwaji, Jumuiya hiyo inaendelea na juhudi za kuwajengea uwezo wanawake wa Zanzibar katika maeneo tafauti, ikiwemo kuwawezesha kushika nafasi za maamuzi, ikiwemo Ubunge na Uwakilishi.

Amesema mbali na wanawake kuonesha uwezo mkubwa katika kusimamia majukumu yapo wanaposhika nyadhifa mbali mbali, lakini wamekuwa wakipambana na vikwazo vigumu wanapoamua kuwania nafasi za kisiasa kupitia vyama.

Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (UN Women), Ali Sultan akizungumza katika hafla hiyo amesema miongoni mwa hatua wanazozichukua ni kuwapa ujasiri na kuwaondolea hofu wanawake kwa azma ya kuwawezesha kuwania nafasi mbali mbali za kisiasa kupitia vyama vyao.

Khamis Haji, OMKR

0 comments:

 
Top