Chama cha Msalaba mwekundu Tanzania { red Cross } kimekabidhi msaada wa viatu Pair 90 kwa ajili ya watoto wa familia zilizowekwa Kambini katika Skuli ya Sekondari ya Mwanakwerekwe “C” baada ya Nyumba zao kujaa maji ya mvua.

Msaada huo umefuatia Mvua za Masika zilizotokea usiku wa kuamkia Tarehe 3 Mei mwaka huu na kuleta maafa makubwa yaliyosababisha zaidi ya Nyumba 700 kuathirika ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kuzikosesha makaazi Familia zilizokuwa zikiishi katika nyumba hizo.

Ujumbe wa Red Cross Mkoa wa Mjini Magharibi ukiongozwa na Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho Bwana Shaaban Ali Iddi umekabidhiwa msaada huo kwa Katibu wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salim Moh’d hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Bwana Shaaban Ali Iddi alisema Uongozi wa Red Cross ulifikia hatua ya kutoa msaada huo baada ya kugundua kwamba idadi kubwa ya watu waliohifadhiwa kwenye kambi ya dharura ya Mwanakwerekwe “C” ni Watoto wadogo.

Alisema Red Cross imeguswa na tukio hilo la mafuriko hivyo licha ya juhudi wanazochukuwa za kutoa misaada mbali mbali ya huduma lakini pia ikawajibika kuongeza msaada huo wa Viatu ambao kwa kiasi kikubwa utawasaidia watoto hao.

Mwakilishi huyo wa Mkutano Mkuu wa Red Cross Taifa aliyaomba Mashirika na Taasisi nyengine za Kitaifa na Kimataifa kuendelea kuguswa na Tukio hilo na kutoa misaada kwa jukumu hilo si vyema ikaachiwa pekee Serikali Kuu.

Akipokea Msaada huo Katibu wa Kamatio ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rsis wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d aliipongeza Red Cross kwa jitihada zake inazoendelea kuchukuwa katika kusaidia huduma za Kijamii.

Dr. Khalid alisema Viongozi na Wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania muda wote wamekuwa karibu na Serikali hasa wakati yanapotokea matukio ya majanga na maafa.

Katibu huyo wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na Maafa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Red Cross kwa hatua yake hiyo ambayo itasaidia kupunguza machungu ya Watoto hao, wengi kati yao wamepoteza vitu vyao vyote zikiwemo nguo na hata madaftari ya Skuli.

Alisema Kambi ya dharura ya Mwanakwerekwe “ C “ hivi sasa ina zaidi ya watoto 74 walio chini ya umri wa miaka 14 wanaoendelea kuhifadhiwa ambao watafaidika na msaada huo wa viatu.

“ Asilimia kubwa ya Watoto hao waliopo Kambini wamepoteza Vitu vingi ikiwemo Madaftari ya Skuli, Nguo, Viatu na vitu vyengine muhimu wanavyotumia ambavyo vingi kati yao tayari Idara ya Maafa kupitia Taasisi na Mshirika hisani wameshapatiwa “. Alifafanua Da. Khalid Salum Moh’d.

Pia aliyashukuru na kuyapongeza Mashirika na Taasisi za Umma na hata zile Binafsi zilizojitolea kutoa misaada mbali mbali ya Kibinaadamu na kuziomba zisichoke kwa vile bado mahitaji zaidi kwa waathirika hao yanahitajika.

Katibu huyo wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alieleza kwamba Serikali imeandaa mpango maalum wa usafiri kwa watoto wote waliopo Kwenye Kambi ya dharura Mwanakwerekwe “C” kuendelea na masomo yao kwenye skuli mbali mbali wanazotoka.

Dr. Khalid aliwatoa hofu Wazazi wa Watoto hao kwamba Gari zilizoandaliwa zimepangwa kuwachukuwa watoto hao na kuwapeleka kwenye Skuli zao waanze masomo kama kawaida na kuwarejesha Kambini baada ya kumaliza masomo yao kwa kila kipindi watachokuwapo kambini hapo..

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top