Matayarisho kwa ajili ya ujio wa Rais wa Jamuhuri ya Msumbiji Bwana Philipe Jacinto Nyusi anayefanya ziara rasmi ya Kiserikali Nchini Tanzania yamekamilika kwa upande wa hapa Zanzibar.

Bw. Nyusi anaiongoza Jamuhuri ya Msumbiji katika kipindi cha Miaka Mitano baada ya kuingia Madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu wa Nchi hiyo wa Tarehe 15 Oktoba mwaka 2014 Kupitia chama Tawala cha Frelimo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa alipata fursa ya kukagua matayarisho hayo yaliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } pamoja na vikundi vya burdani.

Matayarisho ya mapokezi hayo yamefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume ambapo Nyimbo za Taifa za Msumbiji na wa Zanzibar ziliiimbwa zikiambatana na mizinga 21 ya majaribio kupigwa kuashiria kukamilika kwa maandalizi hayo.

Bwana Philipe Nyusi anayetarajiwa kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein mchana wa Jumatatu ya Tarehe 18 Mei mwaka huu atapata fursa ya kupokea saluti na kukagua gwaride rasmi lililotayarishwa kwa heshima yake.

Katika mapokezi hayo Dr. Shein anatarajiwa pia kuambatana na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Kisiasa, wananchi pamoja na Raia wa Msumbiji wanaoishi hapa Zanzibar .

Bwana Philipe Jacinto Nyusi aliyezaliwa Tarehe 9 Febuari mwaka 1959 katika Kijiji cha Namai kwenye Jimbo la Cabo Delgado ndani ya Wilaya ya Mueda Nchini Msumbiji akitokea katika familia ya wazazi waliopigania uhuru wa Taifa hilo kutoka kwa Wareno ana stashahada ya Uhandisi ya chuo Kikuu cha Manchester Nchini Uingereza .

Kiongozi huyo wa Msumbiji Bwana Nyusi kabla ya kuwa Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji kuanzia Tarehe 27 Machi mwaka 2008 hadi 2014 aliwahi pia kuwa Mhadhiri katika Kampus ya Nampula ya chuo Kikuu cha Pedagogica.

Kiongozi huyo wa Jamuhuri ya Msumbiji Bwana Philipe Jacinto Nyusi anakamata wadhifa huo akiwa Rais wa Nne Tokea Taifa hilo kutoka mikononi mwa Ureno akitanguliwa na Kiongozi wa kwanza wa Ukombozi Rais Samora Machel, Bw. Joaquim Chisano pamoja na Bwana Armando Guebuza.

Bwana Nyusi mwenye umri wa miaka 56 akiwa ni Rais wa 4 kuchaguliwa Kidemokrasi Nchini Msumbiji wazazi wake walimvusha kupitia Mto Ruvuma na kuingia Nchini Tanzania kupata elimu yake ya awali katika Skuli ya Msingi ya Frelimo Tunduru Nchini Tanzania.

Alifanikiwa kuendelea na masomo yake ya Sekondari kwa kujiunga na Skuli ya Frelimo ya Mariri iliyopo Cabo Delgado na baadaye Sekondari ya Samora Mashel Mjini Beira.

Mwaka 1973 Bwana Philipe Nyusi aijiunga na Chama cha Frelimo akiwa na umri wa Miaka 14 na kujiingiza katika masuala ya kisiasa na baadaye kupata mafunzo ya kijeshi katika Kambi ya mafunzo ya Nachingwea Nchini Tanzania.

Akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Ukombozi wa Frelimo Bwana Philipe Nyusi alipata mafunzo ya Uongozi katika Mataifa ya India, Afrika Kusini, Swaziland na Marekani.

Mwaka 1990 Bwana Philipe Nyusi alikamilisha mafunzo yake ya Shahada ya kwanza ya Uhandisi katika chuo kikuu cha Ufundi cha Brno iliyokuwa Czechoslovakia. Pia alipara stashahada ya Uongozi katika Chuo Kikuu cha Manchester Nchini Uingereza.

Kwenye Utumishi wa Umma Bwana Nyusi aliwahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Bandari na Reli ambapo utendaji wake ulimuwezesha kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo baadaye kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka hiyo.

Mnamo Tarehe 1 Machi 2014 Kamati Kuu ya Taifa ya Chama cha Frelimo ilimchaguwa Bwana Philipe Nyusi kuwa mgombea wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Nchi hiyo baada ya kupata asilimia 68% ya kura dhidi ya mgombea mwenzake wa chama hicho Bibi Luisa Diogo aliyepata asilimia 31%.

Hiyo ilikuwa raundi ya pili ya kumtafuta Kinara wa Frelimo atakayeipeperusha Bendera ya Chama hicho kwenye uchaguzi Mkuu wa Vyama vingi Nchini Msumbiji wa 2014 baada ya ile ya kwanza aliyopata asilimia 46% chini ya kiwango kinachokubalika kwa mujibu wa Katiba ya Nchi hiyo cha asilimia 50%.

Bwana Philipe Jacinto Nyusi alifanikiwa kueperusha Bendera ya Chama cha Frelimo baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Tarehe 15 Oktoba mwaka 2014 kwa kupata Kura Milioni 2,778,497 sawa na asilimia 57.03%.

Aliwashinda Wapinzani wake Bwana Afonso Dhlakama wa Chama che Renamo aliyepata kura Milioni 1,783,382 sawa na asilimia 36.61% akishika msindi wa Pili na Bwana Dayiz Simango wa Chama cha MDM aliyepata Kura Laki 309,925 sawa na asilimia 6.36%.

Kiongozi huyo wa Jamuhuri ya Msumbiji Bwana Philipe Jacinto Nyusi anakamata wadhifa huo akiwa Rais wa Nne Tokea Taifa hilo kutoka mikononi mwa Ureno akitanguliwa na Kiongozi wa kwanza wa Ukombozi Rais Samora Machel, Bw. Joaquim Chisano pamoja na Bwana Armando Guebuza.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top