Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran ina wajibu wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati za maendeleo kutokana na Historia ndefu iliyopo ya muingiliano wa kibiashara baina ya baadhi ya Wananchi wa pande hizo mbili.

Gavana Mkuu wa Jimbo la Sistan na Balachestan Nchini Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran Bwana Ali Osat Hashemi akiuongoza Ujumbe wa Viongozi saba wa Jimbo hilo alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Gavana Ali Osat Hashemi alisema muingiliano huo wa biashara kati ya Irani na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla umepelekea watu wa pande hizo mbili pia kuwa karibu zaidi kwa kuchanganya damu.

Alisema wiki chache zijazo pande hizi mbili zinatarajia kusaini Mkataba wa ushirikiano katika kuendeleza mradi wa mafunzo ya amali ambao utagharimiwa na Iran kwa kiasi cha Dola za Kimarekani Laki 500,000 zitakazotumika katika ununuzi wa vifaa vya kufundishia.

Gavana huyo wa Jimbo la Sistan na Balachestan Nchini Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran alifahamisha kwamba sekta binafsi hasa miradi ya amali inafaa kuungwa mkono kwa vile inasaidia kutoa ajira kubwa kwa Jamii hasa Vijana.

Alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Iran itaendelea kutoa fursa za masomo ya Elimu ya juu kwa Wanafunzi wa Tanzania na Zanzibar katika vyuo vikuu mbali mbali vilivyomo nchini humo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema miradi ya Amali na Sekta ya Afya inayofadhiliwa na Iran kwa Zanzibar ni uthibitisho wa uimarishaji wa uhusiano uliopo kati ya pande hizo mbili.

Balozi Seif aliiomba Jamuhuri ya Kiislamu ya Irani kuendelea kuongeza fursa za mafunzo kwa Vijana wa Zanzibar ili elimu watayoipata hasa katika miradi ya amali iweze kusaidia kupunguza wimbi kubwa la ukosefu wa ajira hapa Nchini.

Alieleza kwamba fursa za ajira bado zinaendelea kuwa changamoto kubwa kwa Mataifa mbali mbali Duniani zikiwemo pia zile Nchi ishirini zilizoendelea kiviwanda Ulimwenguni { yaani G 20 }.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikutana kwa mazungumzo na Balozi Mpya wa Malawi Nchini Tanzania Bibi Hawa O. Ndilole aliyefika kujitambulisha rasmi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Balozi huyo Mpya wa Malawi Bibi Hawa Ndilole alisema Historia kubwa ya Utamaduni na Elimu inayofanana kati ya Malawi na Tanzania inafaa kuendelezwa zaidi kwa maslahi ya mataifa hayo mawili jirani.

Bibi Hawa alifahamisha kwamba muingiliano wa mafunzo ya elimu ya juu ambao unatoa fursa kwa wanafunzi wengi wa Malawi kupata elimu ya vyuo vikuu nchini Tanzania ni moja kati ya uthibitisho huo wa uhusiano mwema.

Naye Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa wataalamu wa kilimo wa Malawi na Zanzibar kufanya utafiti wa pamoja kwenye sekta hiyo ili kusaidia kutoa matunda bora yatakayoimarisha ustawi wa Wananchi wa pande hizo mbili.

Balozi Seif alisema Mataifa ya Bara la Afrika yamebarikiwa kuwa na Utajiri mkubwa wa rasilmali tofauti zinazopaswa kufanyiwa utafiti wa pamoja na wataalamu wazalendo wa Bara hili ili ziendelee kufaidisha Bara hili.

Akizungumza na Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Japani Balozi Batilda Buriani aliyefika Ofisini kwake Vuga kumuaga rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Balozi Seif alimuomba Balozi Batilda kuhakikisha kwamba Tanzania inafaidika kutokana na ushirikiano wake wa Kidiplomasia ya Japan.

Balozi Seif alisema ipo miradi kadhaa ya maendeleo kama huduma za Umeme, Maji pamoja na masuala ya kukabiliana na maafa na majanga inayoendelezwa na Zanzibar ambayo imekuwa ikipata nguvu na ufadhili katika utekelezaji wake kutoka Japan suala ambalo Balozi Batilda atapaswa kulifuatilia ili kuona utekelezaji wake unafikia ufanisi uliokusudiwa.

Alifahamisha kwamba kazi kubwa ya Balozi Batilda Buriani ambayo amekabidhiwa na Taifa katika kusimamia Diplomasia ya Tanzania Nchini Japan ni kuchangamkia fursa zote za Maendeleo ambazo zinaweza kuisaidia Tanzania kupitia taasisi na mashirkia yote yatayokuwa ytayri kujitolewa kusaidia nguvu zao.

Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Batilda Buriani amepata uteuzi huo aliokabidhiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete wadhifa ambao aliwahi kuutumikia kabla Nchini Jamuhuri ya Watu wa Kenya.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibara

0 comments:

 
Top