Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Uongozi wa Jimbo hilo utaendeleza mikakati ya kuweka miundo mbinu muhimu katika sekta za Maji safi na salama, afya, elimu na umeme ili kuwajengea mazingira bora Wananchi katika upatikanaji wa huduma hizo.

Alisema uongozi wa Jimbo hilo utakuwa tayari kufafuta ushauri wa Kitaalamu katika kufanya utafiti wa upatikanaji wa huduma hizo hasa ile ya maji safi na salama katika baadhi ya vijiji vyenye mazingira magumu yha bara bara na milima.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa hafla maalum ya uzinduzi wa huduma za Maji safi na salama zilizofanyika katika Skuli ya Kilombero iliyomo ndani ya Jimbo la Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mradi huo wa Maji safi na salama umetekelezwa kwa pamoja kati ya wananchi wa Kijiji cha Kilombero, Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Kitope kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } na Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } ukigharimu zaidi ya shilingi Milioni 87,000,000/- .

Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi wa Jimbo hilo kwamba Mikakati hiyo ya miundo mbinu itaendelea kutekelezwa hatua baada ya hatua kadri hali ya fedha itakavyoruhusu hasa kwa kutumia mfuko wa Jimbo na nguvu binafsi za Viongozi wa Jimbo hilo.

Aliwaomba Wananchi waendelee kuimarisha miradi yao ya maendeleo ile wanayoitekeleza pamoja na ile wanayofikiria kuianzisha ili kustawisha familia zao badala ya kusubiri kasumba zinazofanywa na watu wasiowatakia ustawi mzuri na maisha bora.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwapa pole Wananchi wa Vijiji vya Kilombero na Pangeni kwa ustahamilivu wao wa miaka mingi wa ukosefu wa maji safi na salama ambayo kwa sasa itakuwa Historia ndani ya Vijiji hivyo.

Aliushukuru na kuupongeza Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } na ule wa Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO } kwa juhudi za pamoja ulizochukuwa katika kuhakikisha wananachi wa Vijiji vyaKilombero na Pangeni wanapata huduma za Maji safi na salama.

“ Leo tumezindua mradi wa maji safi na salama Kilombero baada ya juhudi kubwa zilizochukuliwa na wenzetu wa ZECO na ZAWA na tunapaswa kuwapongeza kwa vile hata katika Kijiji cha Kinduni mradi kama huu unatekelezwa na mimi nitahakikisha najenga kibanda cha maji ndani ya mwezi mmoja kwa lengo la kuharakisha kuwaondoshea usumbufu wa maji wananchi hao “. Alisema Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.

Akizungumzia suala la amani na usalama wa Taifa Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza ushauri wa Jeshi la Polisi Nchini wa kuwaomba Viongozi wa Kisiasa kuacha tabia ya kuchukuwa wafuasi wao sehemu moja kwenda nyengine kufanya Mikutano yao.

Alisema ushauri huo wa Jeshi la Polisi wa kuvitaka Vyama vya Siasa pamoja na Viongozi wa vyama hivyo kufanya Mikutano ya hadhara kwa kuhusisha wananchi wa sehemu husika badala ya kutoa watu Mjini ina lengo la kujaribu kuepuka shari na vurugu ambazo zimeshuhudiwa kutokana na makundi hayo.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba Jeshi la Polisi lazima liendelee na utaratibu huo wa kudhibiti makundi ya watu kufuatilia Mikutano ya Hadhara kutoka maeneo yao na kwenda sehemu nyengine.

“ Katika kuepuka shari na vurugu zisizo na msingi Kiongozi wa Kisiasa haipendezi kumuona anakwenda kuhutubia Mkutano wa Hadhara sehemu ya mbali akiwa na Watu Mgongoni “. Aliasa Balozi Seif.

Alishauri kwamba jamii na wananchi wote wanapaswa kusaidia kulinda na kudumisha hali ya Amani kipindi hichi ambacho Taifa linakaribia kuingia katika Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu.

Akitoa Taarifa ya Mradi huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu alisema kazi zote zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo utakaohudumia wananchi wa Kilombero na Pangeni zimekamilika.

Dr. Garu alisema mradi wa maji safi na salama wa Kilombero wenye kisima chenye uwezo wa kuzalisha maji Lita 17,000 kwa saa moja ni juhudi zilizochukiliwa na Serikali Kuu katika kuwapatia huduma za maji safi na salama Wananchi wapatao 1,934 wa sehemu hiyo.

Mapema Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliendelea kuwaasa Vijana kuwa makini na tahadhari na wanasiasa wenye tabia ya kuwahadaa kufuata mkondo na ushawishi wa kujiingiza katika vitendo vya vurugu.

Mama Asha alisema wapo wanasiasa wanaoeneza kasumba kwa vijana dhidi ya Viongozi wa chama cha Mapinduzi wakati ushahidi wa juhudi na utekelezaji wa Ilani na sera ya chama hicho inayosimamiwa na Viongozi hao wa CCM iko wazi.

Katika Mkutano huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi fedha Taslimu+ shilingi Milioni 6,300,000/- kwa Vikundi 20 vya saccos vya Vijiji vya Kilombero, Pangeni na Boma.

Fedha hizo amezitoa kwa lengo la kuviwezesha Vikundi hivyo vya saccos na Vikoba kutekeleza miradi iliyojipangia ya uzalishaji mali na hatimae kuchangia kupunguza ukali wa maisha.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top