Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Watanzania Bara na Zanzibar wataendelea kushirikiana kwa karne kadhaa zijazo kutokana na muingiliano wao wa kidamu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Alisema uwepo wa ushirikiano huo ndio njia pekee itakayotowa fursa kwa Watanzania hao kusaidiana katika kutatua changamoto zinazojichomoza miongoni mwao na vizazi vyao.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa ujirani mwema kati ya Wanachama na Viongozi wa Mkoa wa Magharibi na wageni wao kutoka Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es salaam.

Mkutano huo uliofanyika katika Tawi la Chama cha Mapinduzi Kwerekwe “B” unafuatia ziara za ujirani mwema kati ya pande hizo mbili zinazofanyika mwanzoni mwa mwezi wa Aprili ya kila mwaka kutegemea upande unaokuwa mwenyeji wa ugeni huo.

Balozi Seif alisema hakuna kikundi wala mtu anayeweza kuung’oa Muungano uliopo wa Tanganyika na Zanzibar kutokana na historia yake kwa jinsi ulivyoimarika kwa miaka kadhaa iliyopita.

Amewataka na kuwaomba Watanzania wote kuiunga mkono Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba kwa vile inakidhi mahitaji na haki za makundi yote yaliyopo hapa Nchini.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Katiba iliyopendekezwa yenye muundo wa mfumo wa Serikali mbili ndio itakayolivua Taifa la Tanzania kuendelea kudumu kwa zaidi ya miaka mengine hamsini ijayo.

Akizungumzia suala la Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwataka Wanachama wa CCM Kuheshimu maamuzi ya Vikao vya Chama chao wakati vinapofanya kazi ya kuteuwa wagombea wao.

Alisema ni vyema kwa wanachama hao kukubali maamuzi yanayotolewa na chama chao kwa kuwaunga mkono wagombea waliopendekezwa katika ngazi zote kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ujao.

Akisoma risala Katibu wa Kamati ya ujirani mwema Ndugu Muhidini Makame Ussi alisema ujirani mwema kati ya Kata ya Mtoni Wilaya ya Temeke na Wilaya ya Dimani umeanza tokea mwaka 1995.

Nd. Muhidini alisema ujirani mwema huo unaojumuisha Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa pande hizo mbili umeanzishwa kwa lengo la kuimarisha ujirani mwema sambamba na kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964.

Mapema Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtoni ambae pia ni Katibu Mwenezi wa Kata hiyo Ndugu Hija Makamba alisema Viongozi na Wanachama wa CCM wa pande hizo mbili tayari wamekuwa na utaratibu wa kutembeleana hata katika siku za kawaida kwa takriban miaka 20 sasa.

Ndugu Hija alieleza kwamba ziara hizo zimekuwa zikitoa nafasi kwa wanachama na Viongozi wa pande hizo mbili za Wilaya ya Dimani na Wilaya ya Temeke kubadilishana mawazo ya Kisiasa na hata yale ya Kiutamaduni.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top