Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba wananchi wanalazimika kujenga utamaduni wa kuthamini kazi za wabunifu na wasanii kwa kuona fahari kuzilipia bila ya shuruti pale wanapozitumia jambo ambalo ni uungwana na kinyume chake inahesabika kuwa ni wizi.

Alisema Serikali kupitia Ofisi ya Hakimiliki, Bodi ya Hakimiliki na Jumuiya ya Hakimiliki Zanzibar { COSOZA } itaendelea kusimamia kazi za wabunifu na wasanii ili kuona kuwa maslahi, nguvu na jasho lao halipotei bure kutokana na ulaghai unaoendelea kufanywa na watu wanaozipora kazi zao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati wa hafla ya ugawaji wa Mirabaha kwa Wabunifu na wasanii Zanzibar zilizofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar.

Alisema Serikali itaendelea kuchukuwa hatua za kisheria za kuwadhibiti wezi hao wasiojali jasho la wenzao, lakini kazi hiyo inaweza kufanikiwa kwa ufanisi zaidi endapo wabunifu na wasanii wenyewe watatoa ushirikiano kwa taasisi zinazosimamia maslahi yao katika kudhibiti wizi wa kazi zao.

“ Tushirikiane katika kuwasaka, kuwabaini na kuwaripoti katika vyombo vinavyohusika wale wote watakaobainika wanatumia kazi zenu kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Serikali haipendi kuwabughudhi wananchi wake katika biashara hata kidogo lakini hulazimika kuchukuwa hatua za kisheria mara moja pale ambapo uvunjaji wa sheria unapobainika ili haki ipatikane kutokana na sheria inavyochukuwa mkondo wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwazindua wabunifu na wasanii kuwa wanapoingia kwenye mikataba pamoja na watumiaji wa kazi zao wahakikishe kwamba makubaliano yao yanakuwa halali yanayozingatia misingi ya hakimiliki katika biashara zao.

Balozi Seif aliwataka wabunifu na wasanii wale na tahadhari wakati wa kuweka saini Mikataba, wanakuwa na makubaliano na maelewano ya kweli ili kuwepuka mizozo baina yao na wale wanaotiliana nao saini mikataba hiyo.

Balozi Seif aliwasihi wamiliki wa vituo vya utangazaji kuheshimu haki na kazi za wabunifu na wasanii wakielewa kwamba vituo vyao vinategemea kwa kiasi kikubwa kazi hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki kwa kusimamia vyema ukusanyaji na ugawaji wa Mirabaha na kuitaka iendelee na utaratibu huo kwa kila mwaka.

Balozi Seif aliiomba Ofisi hiyo kuandaa mpango maalum kwa wabunifu wa michoro mbali mbali zikiwemo picha za ramani ili wafaidike moja kwa moja na mirabaha kwa makusanyo badala ya utaratibu wa sasa wa makubaliano ya mbunifu na mhitaji wa kazi husika.

Amewapongeza wabunifu na wasanii wote wa Zanzibar waliopo na wale waliotangulia mbele ya haki kwa kazi zao mbali mbali ambazo zimeitangaza na kuijengea sifa Zanzibar katika medani ya Kimataifa.

Alisema kazi za wabunifu na wasanii hao zimechangia kuelimisha, kuburudisha, kuhamasisha na kuhifadhi utamaduni wa Taifa hili pamoja na kutoa ajira kwa wananchi walio wengi hasa kundi kubwa la Vijana na hatimae kuchangia uchumi wa Taifa.

“ Hatimiliki ukijumlisha na ubunifu na sanaa jawabu unalopata ni ajira pamoja na ukuaji wa uchumi wa Taifa “. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema kutokana na umuhimu wa wabunifu na wasanii, Jumuiya ya Kimataifa iliweka misingi mikuu na muhimu ya kufuatwa na nchi zote wanachama katika kusimamia ulinzi, hadhi, haki na maslahi yao mkataba ambao unasimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maslahi ya wabunifu na wasanii { World Intellectual Property Organisation – WIPO }.

Alisema Tanzania iliridhia mkataba huo wa Berne mwaka 1886 wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikaridhia mkataba huo kwa kupitishwa sheria nambari 14 ya mwaka 2003 yenye kusimamia masuala ya Hakimiliki.

“ Sheria hiyo ndio iliyounda Ofisi inayosimamia masuala ya Hakimiliki, Bodi ya Hakimiliki na Jumuiya ya Hakimiliki maarufu COSOZA “. Alisema Balozi Seif.

Akitoa Taarifa Msimamizi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar Bibi Mtumwa Khatibu Kheir alisema huo ni mgao wa pili wa Mirabaha kwa wabunifu na wasanii wapatao elfu 1124 wa zanzibar.

Bibi Mtumwa alisema Ofisi ya Hakimiliki imefanya kazi kubwa na nzuri kwa kushirikiana na kamisheni ya Utalii pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji vitega uchumi Zanzibar { ZIPA } katika kuziunganisha kwa wateja kazi za wabunifu na wasanii.

Hata hivyo Msimamizi na Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa Ofisi ya Hakimiliki alitanabahisha kwamba wabunifu na wasanii wasiosajiliwa kamwe hawataweza kufaidika na mgao wa Mirabaha inayotolewa.

Bibi Mtumwa Khatibu Ameir aliwataja wabunifu na wasanii wanne waliokuwa mfano mwaka huu kuwa ni pamoja na Bwana Khamis Juma, Bibi Mwapombe Hiari, Bwana Mwalimu Ali Mwalimu na Marehemu Seif salim.

Mapema akimkaribisha Mgeni rasmi Balozi Seif, Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakar alisema vipaji walivyokuwa navyo wabunifu na wasanii wa Zanzibar ni vyema vikaenziwa na kuheshimiwa kwa faida ya Taifa kwa jumla.

Waziri Aboubakar alisema Zanzibar imepata umaarufu mkubwa Duniani kutokana na ongezeko la vipaji vya wabunifu na wasanii wake wanaoonekana kuwa kivutio kwa wageni na watalii mbali mbali wanafuatilia kazi za wabunifu na wasanii hao.

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar aliwashukuru wachangiaji kutoka Taasisi mbali mbali za Umma na zile binafsi wakiwemo pia watu maarufu kwa uamuzi wao wa kusaidia kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa taifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top