Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewahakikishia wafanyakazi wa shamba la Mipira Kichwele kwamba itafanya jitihada na mbinu zote katika kuona wanalipwa mishahara yao kati ya miezi mitatu hadi Minane wanayoidai Kampuni iliyowekeza Mradi huo ya Agro Tec kwa kipindi kirefu sasa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kadhaa yaliyowasilishwa kwake na Wafanyazi hao wakiushutumu Uongozi wa Kampuni hiyo kuwadhalilisha pamoja na kutopewa haki zao kadhaa Mkutano uliofanyika katika kituo cha Mradi huo kiliopo pembezoni mwa Wilaya za Kaskazini “B”.

Balozi Seif alisema kwamba Kampuni ya Agro Tec haikuwa makini kujipanga katika uendeshaji mradi huo tokea kukabidhiwa kwake jambo ambalo haina tija Serikali Kuu pamoja na Wafanyakazi wenyewe.

Alisema katika kuondosha utata huo wa muda mrefu ni jambo la msingi kwa Kampuni hiyo kufanya utaratibu wa kulipa haki zinazodaiwa na Wafanyakazi hao ikiwemo zile ya mafao ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii { ZSSF } pamoja na Fedha za likizo.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali Kuu kwa kushirikiana na Taasisi zinazosimamia uwekezaji, ukusanyaji wa Mapato, usimamiaji haki za Wafanyakazi na Mfuko wa hifadhi ya Jamii zitafanya uchunguzi wa kina ili kuona uwezo wa Kampuni hii kama unakidhi kuendelea kuwekeza mradi huu.

“ Sisi kama Serikali kwa kushirikiana na taasisi zote husika tutauchunguza mradi huu utendaji wake tokea Kampuni ya Agro Tec ilipokabidhiwa na hatutakuwa na muhali kuifutia kibali Kampuni hiyo endapo haitatekeleza masharti na makubaliano yaliyowekwa ikiwemo haki za Wafanyakazi “. Alisema Balozi Seif.

“ Nakuhakikishieni wafanyakazi nyote wa shamba la Mipira kwamba haki zenu zote zitapatikana kwa mujibu wa taratibu tulizokubaliana na muwekezaji huyu hata kama kuuzwa mali zake na kufidia madeni anayodaiwa “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru wafanyakazi hao wa shamba la Mipira lwa Kichwele kwa ustahamalivu wao wa muda mrefu ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kuepusha shari kati yao na Uongozi wa Kampuni n iliyowekeza mradi huo.

Mapema wakitoa malalamiko yao wafanyakazi hao wa shamba la Mipira la Kichwele walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Bodi iliyopo hivi sasa ya Kampuni hiyo ya Agro Tec haina maslahi kwao.

Walisema mgogoro kati yao na Uongozi wa Kampuni hiyo ulioanza tokea mwaka 2013 umesababisha maisha yao kuwa mashakani na kukosa matumaini ya kuendesha maisha yao kupitia mradi huo.

Naye Kamishna wa Kazi Zanzibar Nd.Kubingwa Simba alisema kwamba Muwekezaji ye yote hapa Nchini hawezi kufunga mradi wake mpaka ahakikishe analipa madeni na stahiki zote kwa washirika wake.

Nd. Simba alisema kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa katika masuala ya uwekezaji Mahkama ndio yenye haki na uwezo wa kutoa maamuzi endapo muwekezaji huyo atakwenda kinyume na mkataba aliyofunga.

Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Ased Bakar Ased alisema umri wa uzalishaji wa miti ya mirira ya kichwele na iliyoko Kisiwani Pemba iliyooteshwa mwaka 1977 umepindukia uzalishaji Kiuchumi.

Dr. Ased alisema mashamba ya mipira yameshapoteza muelekeo kutokana na bei ya bidhaa hiyo katika soko la Kimataifa imeshuka kutoka Dola za Kimarekani elfu 2,500 hadi elfu 1200 kwa Tani Moja.

“ Hakuna dalili ya bei ya bidhaa ya mpira kuongezeka kwa vile ushindani wa zao la mpira kwa sasa haupo tena “. Alifafanua Dr. Ased Bakar Ased.

Hivi sasa wapo Wafanyakazi 14 kati ya 160 wa shamba la mipira la Kichwele wanaoendelea na kazi kwenye mradi huo uliopewa muekezaji kuuendesha tokea mwaka 2003.

Yapo madeni kadhaa yanayodaiwa Kampuni ya Agro Tec kutoka kwa wafanyakazi hao ambayo ni Shilingi Milioni 34,411,267 Deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Shlingi Milioni 3,637,000/- deni la wagemaji Utomvu na shilingi 21,000,000/- wafanyakazi wa Viwandani.

Mengine ni shilingi Milioni 34,027,750 wasimamizi wa wafanyakazi Mashambani, shilingi Milioni 8,400,000/- wafanyakazi Ofisini, Milioni 42,000,000/- wafanyakazi wa mipira Kisiwani Pemba na shilingi Milioni 166,000,965/- deni la likizo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top