Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewahakikishia wananchi kwamba itaendelea kuchukuwa hatua madhubuti katika kuviimarisha vyama vya ushirika kwa kuendelea kuvifanyia ukaguzi, kuwapatia mafunzo wanachama wa vyama hivyo pamoja na kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuviongezea mtaji.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohemmed Shein wakati wa hafla fupi ya kuuzindua Ushirika wa Jitihada njema wa Bandarini Malindi Mjini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar Dr. Shein ambae Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali inatambua umuhimu wa mchango wa vyama vya ushirika katika kutoa ajira, kuimarisha uchumi na kukuza Demokrasi Nchini.

Alisema hatua kadhaa zimeshachukuliwa katika kuimarisha sekta hiyo sambamba na kukamilika kwa sera ya maendeleo ya Ushirika Zanzibar ya mwaka 2014 ambapo hivi sasa inafanyiwa mapitio sheria nambari 4 ya mwaka 1986.

Alifahamisha kwamba utaratibu wa kuvisajili vyama vya ushirikia nchini unaendelea kwa lengo la kuviimarisha, kuvitambua na kuhakikisha vyama vya vyote vya ushirika vinafanya kazi zake kisheria.

“ Serikali tayari imeshasajili vyama vya ushirika mia 749 vya uzalishaji malio na utoaji huduma. Kiwango hicho kinafanya idadi ya vyama vilivyosajiliwa kufikia elfu 2,493 Zanzibar wakati saccos 16 zimeshasajiliwa na kufanya idadi ya jumla kufikia 203 “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba vyama vya ushirika nchini vimefanikiwa kutengeneza mtaji unaofikia shilingi Bilioni 3.5 ambao umeweza kutoa mikopo zaidi ya shilingi Bilioni Saba katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2015.

Alisema katika tathmini iliyofanywa kwa vyama 88 vya ushirika imebainika kwamba zaidi ya wanachama elfu 6,835 wamepata fursa ya kujiajiri wenyewe kupitia sekta ya ushirika.

Alisema ni jambo la faraja kuona kwamba katika kipindi kirefu sekta ya ushirika imeanza kuwavutia wasomi waliomaliza vyuo vya elimu ya juu ambapo jumla ya vyama vinne vya ushirika vya wasomi vyenye vijana 72 vinavyojishughulisha na utoaji wa huduma za mafunzo na shughuli za kilimo vimesajiliwa.

Dr. Shein alieleza kwamba hayo nji mafanikio makubwa katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ya Sekta ya ushirika kwa mujibu wa Mkuza Awamu ya Pili na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 --2015.

Rais wa Zanzibar aliupongeza Ushirikia wa Jitihada Njema wa Bandarini Zanzibar kwa mafanikio uliopata ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwake na kuongeza idadi ya wanachama iliyofikia 200.

Alisema uamuzi wa kuanzishwa kwa ushirika wa Jitihada Njema mwaka 2014 ni wa busara katika kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini pamoja na kwenda sambamba na lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayowataka Wananchi kuanzisha vikundi vya ushirika kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi na kupambana na umaskini.

Alieleza faraja yake kwa kuona ushirika huo unaweza kulipa mishahara na maposho wanachama wake bila ya kutetereka, kumudu kuwalipia wanachama wake katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } pamoja na kuwawekea uhakika wa kupata huduma za afya wakati wanapozihitaji.

Dr. Shein alitoa rai kwa wanaushirika hao wa Jitihada Njema Bandarini Zanzibar kuzingatia nidhamu ya kazi, uaminifu na uadilifu katika kuzishughulikia mali za watu zenye thamani kubwa.

Alisema lengo la Serikali Kuu ni kuona kuwa muda wa kuhudumia wafanyabiashara wanaotumia Bandari ya Zanzibar unakuwa mchache ili kuwavutia wateja pamoja na wageni wanaotumia Bandari hiyo.

Alieleza kuwa Zanzibar ina Histori ndefu ya shughuli za Bandari kwa kutoa huduma kwa vyombo mbali mbali vya usafiri wa Bandari vinavyochukuwa mizigo na abiria katika ukanda wa mwambao wa Afrika Mashariki.

Alisema umaarufu wa Bandari ya Zanzibar uliongezeka zaidi katika Karne ya 19 kupitia Bandari ya zamani ya Malindi iliyokuwa ikihudumia majahazi na vyombo vyengine vidogo vidogo vya usafiri wa Baharini.

Rais Shein alieleza kuwa shughuli za Bandari ziliimarika zaidi kutokana na kukua kwa muingiliano wa Zanzibar na Mataifa mengine uliosababisha kukuwa kwa biashara na kulazimika kujengwa kwa Bandari ya Malindi mwaka 1924 ambayo iliweza kuzihudumia meli ndogo ndogo na Matishali.

Alisema ukuaji wa bishara ndani ya Bandari ya Malindi iliifanya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha Shirika la Bandari kwa sheria nambari 1 ya Mwaka 1997.

Alieleza kwamba shirika la Bandari ni Mtoto wa lililokuwa shirika la ukapuaji nna uteremshaji wa mizigo Bandarini la Zanzibar Wharfage lililoanzishwa Mwezi August Mwaka 1972 likiwa shirika pekee la Serikali na kufanyakazi kwa kipindi cha miaka 33.

“ Nimefurahi kusikia kwamba waanzilishi wa ushirika wa Jitiohada Njema Bandarini mmetokana na shirika la Bandari na kwa hivyo mna uzoefu wa maeneo 

Rais wa Zanzibar aliwaahidi wanachama wa ushirika wa Jitihada Njema kwamba Serikali itashirikiana nao katika kuona changamoto zinazowakabili zinatafutiwa ufumbuzi ili wapate mafanikio zaidi.

Akisoma Risala ya wana ushirika wa Jitihada Njema Bandarini Mmoja wa Wanaushirika huo Bwana Ali Mohammed alisema Vibarua wa shirika la Bandari walifikia uamuzi wa kuanzisha ushirika huo kwa nia ya kuwa na nguvu za pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao na kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Bwana Ali Mohammed alisema ushirika huo ulioanza na wanachama 100 umekusudia kufanya kazi zake kwa stara tofauti na baadhi ya watu wanavyozifikiria kazi zao ukilenga kushawishi kupunguza wimbi kubwa la ukosefu wa ajira liliopo kwa vijana hapa nchini.

Mwanaushirika huyo wa ushirika wa Jitihada njema Bandarini alifahamisha kwamba zipo changamoto zinazoukabili ushirika huo akizitaja kuwa ni pamoja na ofisi bora na ya uhakika itakayoweza kukidhi mahitaji ya wanaushirika hao.

Katika kuimarisha malengo ya ushirika huo na kujiendesha kimaisha Bwana Ali Mohammed aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Uongozi wa Shirika { ZSSF } ili uwakubalie kuendesha shughuli za usafi katika kiwanja wa Watoto Kariakoo pamojan na Mnara wa Michenzani mara utakapoanza kutoa huduma.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto Nd.Ali Khamis alisema ipo miongozo zaidi ya 15 iliyotayarishwa na Wizara ambayo itajenga mwenendo wa mfumo wa uendeshaji bora wa vyama vya ushirika.

Nd.Ali Khamis alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha nguvu za vikundi vya ushirika ambavyo ndio kimbilio la wananchi walio wengi Nchini katika kujiimarisha kiuchumi na kuongeza mapato yao.

Alifahamisha kwamba Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana , Wanawake na Watoto italifanyia kazi suala la mafunzo kwa wanaushirika wa Jitihada Njema Bandarini ili wafikie hatua ya kufanya kazi zao kitaalamu na ufanisi wenye uhakika.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Uwezeshaji alitoa pongezi Maalum kwa wanaushirika hao wa Jitihada njema kwa mafanikio makubwa wayiyoyapata ndani ya miezi 15 tokeaa ulipoundwa na kuonyesha mfano mzuri wa kuigwa na vikundi vyengine vya ushirika hapa Nchini.

“ Ushirika haupendezi hata kidogo kuona wanachama wake wanajenga tabia na mfumo wa mambo yao kuomba wafanyiwe na Serikli. Nyinyi wana Jitihada Njema mmeonyesha mfano baada ya kuomba mpatiwe Sehemu ya kujenga Ofisi wakati wenzenu huomba wapatiwe Ofisi “. Alifafanua Nd.Ali

Ushirika wa Jitihada Njema Bandarini Zanzibar unajishughulisha na kazi wa utoaji wa huduma za Makontena Bandarini pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika eneo lote la Bandari ya Zanzibar iliyopo Malindi Mjini Zanzibar.

Akitoa shukrani kwa Niaba ya Bodi ya Shirika la Bandari pamoja na Uongozi wa Ushirika wa Jitihada Njema na Wanaushirika wenzake Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mzee Omar Haji alisema Uongozi huo hautamvumilia Mfanyakazi yeyote atakayeanzisha siasa ndani ya Bandari.

Mzee Omar alisema Bandari ni eneo maalum la kuhudumia watu likisimamiwa na watendaji wenye itikadi, makabila na jinsia tofauti kiasi kwamba kuruhusu masuala hayo ni kuvuruga mfumo mzima wa utendaji wa eneo hilo.

“ Siasa zinae sehemu na maeneo yake maalum. Hivyo kamwe hatutamruhusu mtendaji au mfanyakazi ye yote kuingia ndani ya Bandari akaanza kutuhubiria Siasa ambazo baadaye zinaweza kuleta chuki na uhasama “. Alisema Makamu Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Shirika la Bandari Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top