Uongozi wa Hoteli ya Kimataifa ya Karafuu Beach Resort Spa ya Michamvi Wilaya ya Kati umeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wa Kijiji cha Michamvi Wilaya ya kati kwa juhudi walizochukuwa katika kusaidia kuuzima moto mkubwa uliotokea juzi mnamo saa 10.00 za alfajiri.

Meneja wa Hoteli hiyo Bwana Zakaria Juma alitoa pongezi hizo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hotelini hapo kuangalia athari ya moto huo kwa lengo la kutoa Pole pamoja na kuufariji Uongozi na Wafanyakazi wa Hoteli hiyo.

Bwana Zakaria Juma alisema licha ya baadhi ya vitu na vifaa vya Hoteli hiyo kuathiriwa na moto huo lakini juhudi na uungwana ulioonyeshwa na Serikali pamoja na Wananchi ambao ulipelekea kutopotea kwa kitu chochote kilichobakia kwenye kizaa zaa hicho umeleta faraja kwao pamoja na wageni waliokuwemo kwenye Hoteli hiyo.

Meneja huyo wa Karafuu Beach Resort Spa alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba moto huo ambao hadi sasa haujatambulika chanzo chake pamoja na hasara iliyopatikana umeteketeza vyumba 35, Ghala, Duka, Sehemu ya Mapokezi na Mkahawa wa Hoteli hiyo.

Alisema vyumba 70 kati ya 135 vya hoteli hiyo vimesalimika baada ya juhudi zilizochukuliwa kwa pamoja kati ya Wananchi na Wafanyakazi wa Hoteli hiyo kwa kujaribu kuzunguushia mabati eneo la kusini la Hoteli hiyo.

“ Hoteli yetu imejigawa katika maeneo mawili ya vumba na huduma zote. Lipo lile tunaloliita Masai ambalo ndio lililoteketea kwa moto na jengine lililosalimika ni lile liitwalo Bondeni “. Alifafanua Bwana Zakaria Juma.

Alifahamisha kwamba Uongozi wa Juu wa Hoteli hiyo umefikiria kuandaa mpango maalum wa kufanya matengenezo mapya ya eneo lililoathirika na kuendelea kutoa huduma kama kawaida ifikapo mwezi wa saba mwaka huu.

Bwana Zakaria Juma alisisitiza kwamba huduma za kupokea wageni zinaendelea kama kawaida katika eneo la Bondeni ambalo halikuathirika na moto huo.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapa pole na kuwafariji wafanyakazi na Uongozi wa Hoteli hiyo aliwataka kuwa wastahamilivu katika kipindi hichi kigumu ambacho kimeleta usumbufu kwa wageni wao.

Balozi Seif ameupongeza Uongozi wa Karafuu Beach Resort Spa kwa umakini wake wa kuuwekea Bima mradi wao jambo ambalo litasaidia kupunguza machungu kutokana na hasara hiyo.

Hata Hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba ipo haja kwa Uongozi huo kufikiria namna ya ya kubadilisha matumizi ya makuti katika uwezekaji wa majengo ya Hoteli hiyo ambayo ni hatari wakati linapotokea janga la moto.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wawekezaji wa miradi yote ya Kiuchumi na maendeleo kwamba itakuwa pamoja katika kuisaidia wakati inapopata matatizo .

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top