Na: Hassan Hamad, OMKR.
Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Uturuki imesema Zanzibar ina maliasili nyingi na mazingira mazuri ya kibiashara ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuisaidia kuondoa hali ya umasikini kwa kiasi kikubwa.

Jumuiya hiyo imesema kutokana na hali hiyo imeamua kuisaidia Zanzibar kukuza utaalamu katika sekta za kibiashara, uzalishaji na masoko ili utajiri huo uweze kunufaisha wananchi wa Zanzibar ipasavyo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyabiashara wa Uturuki na Tanzania, Atakan Giray wakati yeye na ujumbe wake walipofanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Mwenyekiti huyo amesema wameridhishwa na mandhari ya Zanzibar katika nyanja ya biashara, utalii, ujenzi, kilimo na uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya kuzisafirisha na kwamba kinachohitajika ni utaalamu zaidi.

Amesema mazingira ya Uturuki yanalingana kwa kiasi kikubwa na Zanzibar na ni jambo zuri utaalamu unaopatikana Uturuki ukatumika pia Zanzibar katika kukuza sekta za biashara na uzalishaji ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha hali za wananchi kwa kuweza kuongeza kipato chao.

Giray amesema ujumbe kutoka Uturuki utakuja Zanzibar kutembelea maeneo tafauti yenye fursa za kiuchumi na kibiashara na baadaye fursa hizo kutangazwa kupitia vyombo vya habari vya Uturuki ili kuweza kufikia azma hiyo ya kuinua hali za watu wa Zanzibar.

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amezitaja miongoni mwa fursa nyingi za kiuchumi zilizopo Zanzibar kuwa ni uvuvi wa bahari kuu, utalii, kilimo cha viungo na matunda ambazo zina nafasi ya kutoa ajira nyingi na kukuza uchumi.

Maalim Seif amesifu uhusiano wa kihistoria baina ya nchi mbili hizo, ambao umeanza kuzaa matunda kwa Wazanzibari, wakisemo wale wanakwenda kwa wingi nchini Uturuki kwa ajili ya biashara zikiwemo za vyakula, nguo na vifaa vya ujenzi.

“Sekta ya uvuvi, hasa uvuvi wa bahari kuu pia ina fursa kubwa, tuna maliasili nyingi za baharini ambazo hazijatumika, hili ni eneo moja wapo ambalo wafanyabiashara na wawekezaji wa Uturuki wanaweza kujikita zaidi”, amesema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Amesema amefurahishwa na ahadi ya wafanyabiashara wa Uturuki kusaidia utaalamu na kuleta mashine za kisasa na kuitangza zaidi, hatua ambayo itawasaidia vijana na wananchi wa Zanzibar kupata fursa na kukuza uchumi na maendeleo yao. 

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekutana na kufanya mazunguzo na ujumbe wa Ireland ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wan chi hiyo bwana Jean Sherlock.

Katika mazungumzo hayo, Maalim Seif amesema Zanzibar bado inahitaji kushirikiana na washirikia wa maendeleo ikiwemo Ireland katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Amefahamisha kuwa Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa, tayari imeshuhudia athari mbambali zitokanazo na madiliko ya tabia nchi, ikiwemo maji ya bahari kuingia katika maeneo ya kilimo na kuyafanya maeneo hayo kushindwa kutumika kwa shughuli za kilimo.

Ameyataja maeneo mengine ambayo Zanzibar ingeweza kushirikiana na Ireland kuwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji, msongomano wa wanafunzi madarasani pamoja na maendeleo ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Akizungumzia kuhusu hali ya siasa nchini, Maalim Seif amesema Zanzibar iko salama na itaendelea kutunza na kulinda amani iliyopo, ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea kuishi na kufanya shughuli zao bila ya hofu.

Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema ipo haja ya kuwepo waangalizi makini wa kimataifa katika mchakato wa uchaguzi, ili kushuhudia hali halisi ya siasa za Zanzibar.

Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland bwana Jean Sherlock ambaye aliambatana na balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, amesema Ireland itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza miradi yake ya maendeleo.

Bwana Sherlock amesema Ireland inajivunia uhusiano mwema uliopo kati yake na Zanzibar, na kwamba kuna haja ya kuimarishwa zaidi katika maeneo tofauti kwa maendeleo ya nchi zote mbili.

0 comments:

 
Top