Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Hapa Zanzibar Dr. Andemichael Ghirmay ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujiweka tayari kukabiliana na miripuko ya maradhi yoyote yanayoweza kutokea visiwani ili kulinda ustawi wa Wananchi na wageni wanaoingia Nchini..

Alisema Zanzibar imekuwa kituo kikubwa kinachopokea watu wengi kutoka nchi mbali mbali Duniani kufuatia kuimarika kwa Sekta ya Utalii kiasi kwamba tahadhari ya huduma za afya kwa wananchi pamoja na wageni wanaoingia nchini ni vyema ikazingatiwa kwa umakini.

Dr. Andemichael Ghirmay alitoa ushauri huo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi huko Ofisini kwa Balozi iliyopo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema juhudi za pamoja kati ya Serikali, watendaji wa Sekta ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi na mashirika ya maendeleo ya Kitaifa na Kimataifa lazima zichukuliwe katika kudhibiti maradhi hasa yale ya miripuko ambayo mengi kati yao huchipuka kutokana na maingiliano ya wasafari za Kimataifa.

Mwakilishi huyo wa Shirika la Afya Duniani hapa Zanzibar Dr Andemichael ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa utayari wake ilipojiandaa kukabiliana na maradhi ya Ebola endapo yangetokea nchini ambayo yaliwahi kuenea Magharibi mwa Nchi za Bara la Afrika katika miezi ya hivi karibuni.

Dr. Andemichael Ghirmay alisema katika kuimarisha huduma za Afya kwa Nchi wanachama Shirika hilo la Afya Duniani litaendelea kutoa msukumo zaidi wa kitaalamu kwa Zanzibar katika mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali yanayowasumbua wananchi.

Alieleza kwamba Shirika hilo katika mipango yake sita iliyojipangia ya kutoa elimu, Ushauri na kusaidia Utafiti kwa Nchi wanachama Zanzibar imo katika mchakato wa kuendelea kuungwa mkono na shirika hilo katika kupambana na maradhi mbali mbali sambamba na kusaidia Utafiti katika maradhi hayo.

Mwakilishi huyo wa shirika la Afya Duniani Dr. Andemichael Ghirmay amepongeza ushirikiano anaoendelea kuushuhudia uliopo kati ya Wananchi, Wafanyabiashara pamoja na Viongozi wao wa Majimbo katika ujenzi wa Vituo vya Afya katika Majimbo yao.

“ Mimi kama Mtaalamu wa Sekta ya Afya nimefarajika sana kuona mshikamano uliopo kati ya Wabunge na Wawakilishi kwa kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wananchi wao katika ujenzi wa vituo vya huduma za Afya katika Majimbo yao“. Alisema Dr. Andemichael Ghirmay.

Akitoa shukrani zake kwa mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Afya Duniani { WHO } hapa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika sekta ya Afya kufuatia kuungwa mkono na Shirika hilo.

Balozi Seif alisema zipo huduma nyingi za afya zinazoendelea kutolewa katika Hospitali mbali mbali kubwa sambamba na vituo vya Afya vya Wilaya na Vijiji ambazo msingi wake mkubwa unatokana na shirika hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliomba Shirika la Afya Duniani kupitia Mwakilishi wake huyo hapa Zanzibar liendelee kuisaidia Zanzibar kiuwezeshaji, vifaa pamoja na Taaluma ili ifikie lengo lake la kutoa huduma za afya kwa wananchi waliowengi Mjini na Vijijini.

Alisema Sera ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuona wananchi wote ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba wanaendelea kupata huduma za afya si zaidi ya umbali wa kilomita tano kwenye makazi wanayoishi.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Saleh Mohamed Jidawi alisema kwamba Uongozi wa Shirika la Afya Duniani umekuwa karibu mno na Wizara ya Afya Zanzibar.

Dr. Jidawi alisema Shirika hilo ni kiungo kikubwa kinachoendelea kuisaidia Zanzibar katika mapambano yake dhidi ya udhibiti wa maambukizi ya vizuri wa Ukimwi, chanjo kwa akina Mama Wajawazito na Watoto pamoja na kukabiliana na maradhi ya kichocho.

“ Wizara ya Afya tumefanikiwa vyema katika kupambana na udhibiti wa maradhi ya Kichocho na maambukizi ya kuenea kwa virusi vya ukimwi hapa nchini kutokana na kuungwa mkono na wenzetu wa WHO “. Alisema Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar.

Alisema mchango wa Utafiti na utaalamu wa Shirika shirika hilo katika mapambano dhidi ya maradhi ya Malaria umeiwezesha Zanzibar kudhitibi maradhi ya Malaria chini ya Asilimia 0.6%.



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top