Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba si vyema kwa watu au vikundi vyenye uwezo wa kutoa ajira kuwanyanyasa wananchi wenzao katika miradi yao ya kiuchumi kwa sababu za itikadi ya Kisiasa.

Alisema tabia hiyo mbaya inayoashiria kuleta ubaguzi, uhasama na na hatimae kuzaa chuki miongoni mwa jamii inakwenda kinyume na Ubinaadamu na maamrisho ya Mwenyezi Muungu.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa tahadhari hiyo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Boti ya Uvuvi na Mashine yake kwa Vijana wa Maskani ya Tuheshimiane Mnarani katika Kijiji cha Makangale ambao walifukuzwa katika shughuli za ajira ya uvuvi baada ya kukamua kwa hiari yao kukihama chama cha Wananchi {CUF } na kujiunga na Chama cha Mapinduzi { CCM }.

Boti na mashine hiyo vyenye thamani ya shilingi za Kitanzania Milioni Nane, Laki Nne na Hamsini Elfu { 8,450,000/- } amevitoa kwa vijana hao kufuatia ahadi aliyowapa miezi michache iliyopita wakati wa ziara yake Kisiwani Pemba.

“ Leo nina furaha na shauku kubwa katika kukamilisha ahadi niliyoitoa wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenye Kijiji cha Makangale wakati nilipokutana na vijana hao wakanieleza changamoto zinazowakabili baada ya kuamua kuiacha CUF “. Alisema Balozi Seif.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya watu ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba bado wameamua kuendeleza vitendo vya chuki, uhasama na uadui dhidi ya wenzao kwa sababu tu za itikadi za kisiasa na kidini.

Alisema Zanzibar iliamua kuondosha uhasama na chuki miongoni mwa wananchi wake kwa kuunda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kurejesha umoja upendo na mshikamano ulioasisiwa na vizazi vya karne zilivyopita.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif aliwaomba wananchi Nchini kote kuendeleza Umoja, upendo na mshikamano ili Taifa hili lizidi kupiga hatua kubwa ya Maendeleo.

Balozi Seif aliwakumbusha wananchi wa kisiwa cha Pemba kuendelea kuunga mkono Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba na kuipigia kura ya ndio wakati ukifika.

Alisema Kero nyingi zilizokuwa zikilalamikiwa na wananchi wa Zanzibar tayari zimepatiwa ufumbuzi ndani ya Katiba inayopendekezwa. Hivyo cha Msingi ni kukahiukisha kwamba Katiba hiyo inafanikiwa ili ile kiu ya Wananchi hao iweze kumalizika.

Aliwaeleza wananchi hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Chini ya Chama cha Mapinduzi itaendelea kuwatumikia Wananchi wote bila ya ubaguzi kwa vile imeshaamua kuiendesha katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Aliwatahadharisha wananchi hao kuwa makini na baadhi ya watu walioamua kuwapotosha Wananchi juu ya Katiba iliyopendekezwa ambayo imegusa na kukidhi mahitaji ya wananchi na makundi yote yaliyopo hapa nchini.

Akisoma Risala ya Vijana hao wa Makangale Mjumbe wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Kijiji cha Makangale Nd. Mwinyi Mwewe Mwinyi kwa niaba ya wenzake alimuhakikishia Balozi Seif kwa wataitunza Boti hiyo ili iwaongezee kipato n a kuendesha maisha yao ya kila siku.

Mwinyi Mwewe alisema Vijana hao wamefarijika kutokana na Sera za Chama cha Mapinduzi Kutekelezeka vyema na kumpongeza Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif kwa kutekeleza ahadi aliyowapa katika kipindi kifupi.

Alisema huo ni uungwana unaofaa kuigwa na viongozi wengine ndani ya Chama pamoja na Serikali katika kuwatumikia wananchi wanaowaongoza hasa kujaribu kusaidia kero na changamoto zinazowakabili.

Nd.Mwinyi Mwewe kwa niaba ya wenzake wameahidi kulipa ihisani kwa Chama cha Mapinduzi kwa kuitetea Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba pale wakati utakapowadia.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman alisema kwamba msaada wa Boti hiyo ya Uvuvi kwa Vijana wa Makangale itawaondoshea udhia na mashaka walaiyokuwa wakiyapata.

Mh. Omar kitendo cha Balozi Seif mbali ya kuleta faraja kwa vijana hao lakini pia kimeisaidia Serikali ya Mkoa huo katika harakati zake za kuwaunganisha vijana pamoja na kuwajengea mazingira ya ajira.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top