Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza watendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja kuacha tabia ya kuyafumbia macho matatizo yanayoibuka katika utendaji wao wa kazi na badala yake waiarifu Serikali Kuu ili hatua za dharura zichukuliwe katika kuyakabili matatizo hayo.

Alisema kuendelea kuyaacha matatizo hayo yasambae mbali ya kuchafua mazingira lakini pia yanaweza kusababisha maambukizi ya maradhi na kuwaongezea wagonjwa mtafaruku unaoweza kuepukika.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya ghafla kuangalia hali ya usafi sehemu ya vyoo vya wodi ya wagonjwa wa Kifua Kikuu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Ziara hiyo ya Balozi Seif imekuja kufuatia Taarifa za Shirika la Utangazi Zanzibar { ZBC } zilizoelezea hali isiyoridhisha katika sehemu hizo ambayo ilileta mtafaruku kwa Wagonjwa walioazwa kwenye wodi hiyo.

Balozi Seif alisema yeye kama Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali atakuwa tayari wakati wowote kutoa msaada au ushauri wake katika kutanzua matatizo ambayo Viongozi wa Taasisi hiyo wameshindwa kuchukuwa hatua.

Alisema Wagonjwa pamoja na wananchi wamekuwa wakilalamikia kero, changamoto na hata matatizo yanayowakabili katika kupata huduma za afya kwenye Hospitali ya Mnazi Mmmoja ambayo yamekuwa yakisababishwa na baadhi ya watendaji wazembe.

“ Msifikie pahala mkawa na tabia ya kuvilaumu vyombo vya Habari kwa kuwapasha Habari Wananchi juu ya uzembe mnaoendelea kuufanya katika maeneo yenu ya Kazi “. Alionya Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea kwamba Vyombo vya Habari vitaendelea kuwa na haki na wajibu wa kutoa Taarifa kwa umma matukio ya uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji hao.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara ya kuwafariji wananchi wa Jimbo la Kwamtipura ambao nyumba zao zimeathirika kwa upepo mkali uliovuma ghafla juzi na jana mchana.

Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar alipata wasaa wa kuziangalia Nyumba sita za wananchi hao ambazo baadhi yake zimeezuka kabisa mapaa yake.

Sheha wa Shehia ya Kwamtipura Bwana Machano Salum Khamis { Mbonga } alimueleza Makamu wa ili wa Rais Kwamba upepo huo uliovuma juzi na jana mchana umeezua baadhi ya mapaa nyumba sita ambazo nyengine zimepata athari na kuta zake.

Sheha Machano alisema uongozi wa Shehia ulikutana na waathirika hao kuanza kufanya tathmini ya hasara ya nyumba zilizopatwa na maafa hayo na kuchukuwa hatua za dharura za uhifadhi wa familia hizo.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipuira Mh. Hamza Hassan Juma alisema Uongozi wa Kamati ya Jimbo la Kwamtipura , wananchi na familia zilizopatwa na maafa hayo zilishirikiana pamoja katika kujaribu kurejesha hali ya kawaida ya mazingira ya nyumba hizo.

Mh. Hamza alisema hatua hiyo iliyochukuliwa ya dharura kwa pamoja imeweza kuleta faraja kwa familia hizo kurejea katika mazingira ya hali ya kawaida.

Akizungumza na familia za waathirika wa maafa hayo ya upepo katika skuli ya Maandalizi ya Kwamtipura Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif aliwataka Wananchi hao mkuwa na subira katika kipindi hichi cha maafa.

Balozi Seif aliyeambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na kugawa sadaka kidogo kwa familia za maafa hayo alisema ameshtuka mara baada ya kusikia tukio hilo lililoleta hasara kubwa kwa familia hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewashukuru Wananchi na watu wenye uwezo kwa moyo wao waliouonyesha katika kujaribu kusaidia familia hizo wakati wa tukio hilo.

Alisema linapotokeza tatizo miongoni kwa mmoja kati ya jamii ni vizuri tatizo hilo likawa na watu wote katika kulitafutia ufumbuzi wa pamoja na si vyema kwa baadhi ya watu kufurahia majanga yanayowapata wenzao kwa sababu tu za itikadi za kisiasa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top