Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa mara nyengine tena ndani ya saa 24 amekizindua rasmi Kikundi cha Mazoezi ya Viungo cha Upendo chenye Maskani yake katika Kijiji cha Uzini ndani ya Wilaya ya Kati.

Uzinduzi huo ameufanya katika viwanja vya michezo vya Skuli ya Sekondari Uzini na kushirikisha pia vikundi mbali mbali vya Zoni “D” pamoja na vile vikundi rafiki vya mazoezi viliopo hapa Unguja.

Balozi Seif Ali Iddi aliyaongoza maandamano ya wana vikundi walioshiriki katika uzindui huo yaliyoanzaia Kijiji cha Mgeni Haji Kibombani hadi Skuli ya Uzini akiambatana na Viongozi wa Wizara ya habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na wa Serikali wa Wilaya ya Kati na Mkoa wa Kusini Unguja. 

Akizungumza na wanavikundi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wananchi lazima watenge muda maalum katika kufanya uchunguzi wa afya zao licha ya kufanya mazoezi ya kila siku.

Balozi Seif alisema wapo watu miongoni mwa Jamii wanaotembea na kuendelea na harakati zao za kimaisha kila siku bila kujitambua kwamba wamezongwa na matatizo ya kiafya.

Alisema mazonge kama hayo ndio chanzo kikuu kinachowasababishia watu wa aina hiyo kupata vifo vya ghafla na kuwaacha jamaa na watu wa karibu kushangaa na kuanza dhana na shutuma ya kumtafuta mbaya wake.

“ Jamaa na marafiki wanabakia kushangaa na kuanza shutuma kwamba mwenzetu huyu si bure kwa hili hapa upo mkono wa mtu “. Balozi Seif alisema hizo ni fikra potovu zinazoweza kuleta mfarakano ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwakumbusha wanamichezo na wananchi wote kuendeleza amani na utulivu uliopo hapa Nchini na kuwakemea wale wanaoshika bango la kutaka kuzusha balaa la kuiharibu amani hiyo.

Alifahamisha kwamba Jamii itahamanika na kutawanyika bila ya kujali athari itayowakumba akina mama na watoto endapo hali ya amani na utulivu itapotea hapa nchini.

“ Sisi tunataka kuendelea kufanya mazoezi yetu na kuishi bila ya vurugu. Sasa wale wenzetu wanaosimamia bango la kutaka kuzua balaa ya kuiharibu amani yetu lazima inatupasa tuwakemee kwa nguvu zetu zote “ Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikipongeza Kikundi cha mazoezi ya Viungo cha Upendo cha Uzini na kuahidi kwamba zile changamoto zinazokikabili kikundi hicho hasa suala la vifaa vya kusaidia Jamii katika usafi wa mazingira atalichukulia hatua za haraka.

Mapema Daktari wa kitengo cha kudhibiti maradhi yasiyoambukiz Dr. Omar Abdulla alisema zaidi ya asilimia 33% ya maradhi ya moyo na asilimia 3% ya maradhi ya Kisukari ya watu hapa Zanzibar wameathirika na magonjwa hayo.

Dr. Omar alisema chanzo cha ongezeko la maradhi hayo hapa Nchini kinatokana na watu kutopenda kufanya mazoezi sambamba na kutumia kwa kiwango kikubwa vyakula vya mafuta.

Mchango wa papo kwa papo ulifanywa katika hafla ya uzinduzi wa Kikundi cha Upendo Uzini kwa lengo la kusaidia kuimarisha kikundi hicho kilichoanzishwa karibu miaka Mitatu iliopita.

Zaidi ya shilingi Milioni 3,000,000 zimepatikana katika mchango huo ulioongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa kinara wa kuunga mkono wachangiaji mbali mbali waliojitokeza wakiwemo Viongozi wa Serikali.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top