Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiomba Serikali ya Norway kupitia wataalamu wake wa masuala ya mazingira kuisaidia Zanzibar katika jitihada zake za kufanya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyopo ulimwenguni kote.

Alisema ongezeko la joto pamoja na mmong’onyoko mkubwa wa ardhi unaoonekana kuikumba Zanzibar lakini zaidi kisiwa cha Pemba umesababisha baadhi ya visiwa vidogo vidogo vya pembeni kufunikwa kabisa na maji ya bahari.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa ombi hilo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi Mpya wa Norway Nchini Tanzania Bibi Hanne – Marrie Kaarstad aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Nchi yake kushifa wadhifa huo wa Kidiplomasia.

Alisema licha ya matatizo mengi ya uchafuzi wa mazingira yanayosababishwa na ukataji kiholela wa Mikoko, uchimbaji onyo wa michanga na uvuvi usiozingatia taratibu lakini bado utafiti wa kina kwa kutumia wataalamu waliobobea Kimataifa unahitajika ili kuisaidia jamii kielimu kukabiliana na mabadiliko hayo.

“ Ukataji onyo wa mikoko pembezoni mwa fukwe za Bahari unachangia kwa kiasi kikubwa mmong’onyoko wa ardhi na kuipa nafasi kubwa Bahari kuila ardhi iliyo pembezoni mwa fukwe hizo “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Norway kupitia Shirika la Maendeleo la Nchi hiyo { Norad } kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kusaidia uimarishaji wa miundo mbinu kwenye sekta ya umeme.

Alisema msaada wa Norway kwa kiasi kikubwa umewaongezea Wananchi wengi hasa Vijijini kupiga hatua ya maendeleo na kuwapunguzia ukali wa maisha uliokuwa ukiwakabili kwa miaka mingi iliyopita.

Mapema Balozi Mpya wa Norway Nchini Tanzania Bibi Hanne – Marrie Kaarstad alikiri kwamba Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo ikilinganishwa na miaka 23 iliyopita wakati alipoitembelea.

Balozi Hanne – Marrie alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi yake itaendelea kuiunga Mkono Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika mbinu za kuimarisha uchumi na kupunguza ukali wa maisha ya wananchi wake.

Alisema mpango maalum umeandaliwa na Norway wa kuwapatia fursa za ziara za kujifunza baadhi ya Viongozi wa Tanzania Nchini humo hasa kwenye mradi wa mabadiliko ya Tabia Nchi.

Alisema mpango huo utatoa nafasi kwa wananchi walio wengi kupata mbinu za kujifunza kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo hii kubwa inayoikumba dunia ya mabadiliko ya Tabia Nchi.

Aliyashauri Mataifa ya Bara la Afrika kuendelea kushirikiana katika mapamnano dhidi ya changamoto hilo la mabadiliko ya Tabia Nchi.

Balozi Hanne – Marrie alifahamisha kwamba mpango huo wa ziara za Viongozi utakwenda sambamba na ule ulioandaliwa na Norway wa kutoa elimu kwa Vijana ambao uko tayari wakati wowote kuanza kazi.

Alieleza kuwa elimu ni kila kitu katika kumjenga mtoto kiakili kuweza kuwa na mbinu za kukabiliana na maisha yake ya kawaida.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top