Jamii ya Kiislamu Nchini inapaswa kufuata vilivyo mafundisho sahihi aliyokuwa akiyasimamia Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW } ili Jamii hiyo ipate fursa nzuri ya kuishi katika maisha ya furaha na ustaarabu wa maendeleo makubwa ndani ya Dunia hii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla ya maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Chuo cha Samail Academy na kufanyika katika Msikiti Rahman uliopo Gombani Mjini Chake chake Kisiwani nPemba.

Balozi Seif alisema kigezo chema alichokuwanacho Kiongozi huyo wa waislamu kilijikita zaidi katika kusimamia vyema suala la kudumisha amani katika Dunia, kuleta umoja baina ya waislamu, kujikubalisha kuishi na mayatima sambamba na watu wa rika zote bila ya ubaguzi.

Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Samail Academy kwa juhudi zao walizozichukuwa na hatua waliyoifikia katika kuijenga jamii kitaaluma na maadili yanayokubalika.

Balozi Seif alitoa wito kwa vijana kujishughulisha zaidi katika kutafuta elimu kwani ndio nyenzo pekee inayomfanya mwenye nayo anapoitumia vizuri hupata maendeleo makubwa.

Hata hivyo alionya kwamba wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia vibaya elimu waliyobarikiwa kwa kupotosha wenzao wasiokuwa nayo ili kufikia malengo yao binafsi.

“ Kuna Watu huitumia elimu kuwageuza wenzao kuwa ngazi ya kupandia kuyafikia malengo yao binafsi. Mwenyezi muungu hayataki mambo hayo. Tutumie elimu kwa kuelimisha wengine “. Alisisitiza Balozi Seif.

Alisema mafanikio makubwa kitaaluma na kijamii yatapatikana endapo jamii itajikubalisha kujituma katika misingi ya uaminifu licha ya changamoto za kimaisha zinazowazunguuka katika maeneo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiridhia kukubali kuwa mlezi wa chuo hicho cha Samael Academy aliahidi kuzishughulikia changamoto zinazowakabili Walimu na Wanafunzi hao kwa kutoa mchango wake kadri hali itakavyoruhusu.

Akisoma Risala Mudiri wa Samaeil Academy Sheikh Said Abdulla Nassor alisema Taasisi hiyo iliyoasisiwa mwaka 2012 na kusajiliwa rasmi Mwaka 2014 inajishughulisha na masuala ya kijamii katika maeneo mbali mbali hapa nchini.

Mudir Said alisema Samael Academy imejikita katika kusaidia jamii katika uchimbaji wa visima, kuunganisha Madrasa kuwa na nguvu za pamoja, kuwakusanya watoto yatima kwa kuwajengea mazingira bora ya kielimu na maisha yao ya baadae pamoja na kuanzisha mafunzo kwa walimu wanaotoa hotuba misikitini.

Alisema yao mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2012 akizitaja kuwa ni pamoja na kuzikusanya na kuzisajili madrasa zipatazo 95 zenye wanafunzi elfu 10,995, kusajili mayatima 712 pamoja na kuzitembelea madrasa kwa kuangalia changamoto zinazozikabili.

Mudiri huyo wa Samael Academy Sheikh Said Abdulla Nassor alifahamisha kwamba moja kati ya jambo lililopewa kipaumbele na taasisi hiyo ni kuwaendeleza wanafunzi na vijana waliofanikiwa kumaliza kuhifadhi juzuu 30 za Quran tukufu.

Hata hivyo Sheikh Said Abdulla Nassor alielezea changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo akizitaja kuwa ni pamoja na vikwazo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za umma wanavyovitoa kwa Taasisi hiyo pamoja na usumbufu wa vifaa vya msaada vinavyotolewa wanafadhili wakati wa kutolewa bandarini.

Akitoa salamu zake Rais wa Samael Academy Sheikh Nassir Bin Said alisema Uongozi wa Jumuiya ya Taassi hiyo unafarajika na muitikio mkubwa wa wazazi na walezi waliooonyesha katika kuipokea taasisi hiyo yenye mnasaba na mazingira yao.

Sheikh Nassir alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa na Uongozi huo ili kuona malengo yaliyokusudiwa ya kusaidia jamii kukabiliana na mazingira yanayowazunguuuka yanafanikiwa vyema na kustawisha jamii zao.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo ya Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } Afisa mdhamini Wizara ya Katiba na Sheria Pemba Bwana Omar Khamis alisema Samel Academy tayari imeshaonyesha nia sahihi ya kutaka kusaidia jamii hapa nchini.

Sheikh Omar alisema Taasisi hiyo iko mbioni kujenga misikiti mikubwa mitatu Kisiwani Pemba,maandalizi ya ujenzi wa chuo Kikuu cha Kiislamu Chamanangwe pamoja na ujenzi wa chuo cha Amali Chake chake Pemba.

Alisema uanzishwaji wa chuo hicho cha amali umelenga kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi watakaopata taaluma kwenye taasisi hiyo ambapo maandalizi yameanza katika kuhakikisha kwamba wanafunzo hao wanapata ajira ndani na nje ya Nchi.

Alifafanua kwamba Nchi za Saudi Arabia na Iraq ambazo zimeamuwa kujitolea kusaidia harakati za ujenzi wa chuo hicho cha amali Kisiwani Pemba zimekubali kuwapokea baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wamalizapo mafunzo kwa kuwapatia fursa za ajira katika Mataifa hayo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top