Zaidi ya nusu ya wananchi (54%) wanafikiri kuwa maisha yao yatakuwa bora zaidi ifikapo mwaka 2025. Huu ndio mtazamo wa wananchi wakio katika makundi yote- vijana kwa wazee, wanaume kwa wanawake, na wakazi wa vijijini na mijini. Mtazamo huu ni tofauti kabisa na ule wa nchi za Marekani na Ulaya ambapo karibu wananchi saba kati ya kumi (65%) wanafikiri kuwa watoto wao watakuwa na hali mbaya zaidi kifedha kuliko walivyo wao sasa.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza na Society for International Development (SID) kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina laTanzania ifikapo mwaka 2025: Je, Watanzania wana matarajio gani na maisha yao ya baadaye? Muhtasari umetokana na takwimu zaSauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi. Utafiti huu hufanyika katika maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye matokeo haya). Matokeo haya yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,408 mwezi Agosti 2014.

Wakiangalia nchi kwa ujumla, wananchi wawili kati ya watatu wanaamini kuwa Tanzania itakuwa mahali pazuri pa kuishi mwaka 2025. Wananchi makundi yote bila kujali hali zao za kiuchumi wanaamini hivyo; mathalan, wananchi wenye kipato kikubwa 64% na wananchi maskini 68% wana matumaini na siku zijazo. Watanzania wana matumaini na akiba tuliyonayo kwa ajili ya nchi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi bado wana wasiwasi. Karibu mwananchi mmoja kati ya watano (18%) wanahofia maisha yako yatakuwa mabaya zaidi mwaka 2025 kuliko yalivyo leo, na wapo wengine wanaodhani nchi itakuwa mahali pabaya pa kuishi mwaka 2025. Hapa kuna baadhi ya tofauti kati ya matajiri na maskini, mwananchi mmoja kati ya wanne katika kundi la matajiri (25%) na mmoja kati ya watano katika kundi la maskini (18%) hawana matumaini kuhusu siku zijazo.

Haijalishi mtazamo gani wananchi wanao, bado wanaamini kuwa matokeo na mustakabali wa Tanzania uko mikononi mwa Watanzania. Wananchi tisa kati ya kumi wanaamini kuwa viongozi wa Tanzania (54%) au wananchi (37%) watakuwa na udhibiti zaidi wa maamuzi ya nchi yao. Linapokuja suala la maisha yao wenyewe, wananchi wanaamini jitihada zao wenyewe kuwa ndizo zitazobadilisha maisha yao; wananchi sita kati ya kumi wanafikiri kuwa wao wenyewe ndio wenye ushawishi zaidi juu ya hatma yao ya baadaye. Hata hivyo, wakati mwananchi mmoja kati ya watano anaamini kuwa Serikali itakuwa na ushawishi mkubwa juu ya ustawi wa maisha yao ya baadaye, hakuna mwananchi wa mjini aliyetaja Serikali kama ina ushawishi muhimu. Mbali na wao wenyewe, wahojiwa wa mijini walitaja familia zao (20%) na marafiki au wenzao (19%) kuwa wenye ushawishi juu ya maisha yao ya baadaye.

Ukiangalia kila jambo moja baada ya jingine, karibu wananchi watatu kati ya wanne (72%) wanaamini kuwa Tanzania itakuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025. Wananchi saba kati ya kumi (68%) pia wanafikiri kutakuwa na Rais mwanamke ifikapo mwaka 2025, na wananchi sita kati ya kumi (64%) wanatabiri kukua kwa uzalishaji wa viwanda na kupungua kwa kilimo. Kwa upande mwingine, wananchi wengi wanatabiri kutokea migogoro ya kidini (62%) na nusu yao (51%) wanatarajia kugawanyika kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chochote kitakachotokea huko mbeleni, wananchi wanaona mabadiliko makubwa, wananchi sita kati ya kumi wanatabiri kuwa upinzani utashinda urais, na tembo watapotea kabisa ifikapo 2025. Jambo la kushangaza, matukio mawili yenye uwezekano mdogo kutokea ni Tanzania kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia (38% ) na kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki chini ya Rais mmoja (34%).

Mambo muhimu wanayotaka wananchi kwa siku zijazo ni maboresho kwenye huduma za kijamii (28% wanaona ni kipaumbele chao muhimu) na ukuaji wa uchumi (16% wanaona ni kipaumbele muhimu).

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi wa shirika la Society for International Development, alitoa maoni yake kwenye matokeo haya "Watanzania kwa kiasi kikubwa wana matumaini na maisha yao binafsi ya baadaye, hasa ikilinganishwa na wenzao kutoka nchi zenye maendeleo makubwa kiuchumi, Marekani na Ulaya. Matumaini haya na mtazamo chanya ni mtaji mkubwa. Vinaimarisha uwezo wa nchi kusonga mbele kwa kujiamini na pia inaweka mzigo kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya mafanikio kwa nchi yetu."

Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema "Katika kipindi cha mabadiliko muhimu ya kitaifa na ya kimataifa, wananchi wa matabaka yote kiuchumi, maeneo na jinsia zote, wana matumaini kuhusu kile kilichopo siku za mbeleni nchini Tanzania. Changamoto kwa Serikali ya Tanzania, wasomi wa ndani pamoja na wananchi wenyewe, ni kuhakikisha kuwa matumaini haya yanaendelezwa kupitia utungaji sera na utekelezaji wenye ufanisi, kuhimiza maendeleo yenye usawa na kujenga mshikamano wa kijamii, ili matarajio ya wananchi ya maisha bora siku zijazo yafikiwe."

0 comments:

 
Top