Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa wananchi wa jimbo la Ole katika Wilaya ya Wete kisiwani Pemba.

Akikabidhi gari hilo kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Wananchi CUF katika viwanja vya Kangagani, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama hicho ametaka gari hilo litumike kwa kuwahudumia wananchi wote wa jimbo hilo bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Gari hilo lenye thamani ya shilingi milioni 30 limetolewa na Mbunge wa jimbo la Ole Mhe. Rajab Mbarouk Mohamed.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Maalim Seif, amewapongeza wanachama wa chama hicho katika kijiji cha Kangagani kwa ujasiri walionao katika kukabiliana na changamoto za kisiasa.

Amesema kijiji hicho, kimekuwa kikikabiliwa na upinzani mkali kutoka chama cha mapinduzi huku kikiungwa mkono na baadhi ya vyombo vya dola, lakini wanachama wa CUF wamekuwa wavumilivu na wajasiri katika kutetea haki yao ya kisiasa.

Amesema kila mwananchi ana haki ya kikatiba ya kujiunga na chama anachotaka, na kwamba kitendo cha kuwanyanyasa wananchi kwa sababu ya maamuzi yao ya kujiunga na vyama vya upinzani sio sahihi.

Amewataka wanachama hao kuendelea kusimamia maamuzi yao, na kuwataka kufanya maamuzi sahihi ya kukichagua CUF katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuondokana na madhila ya kisiasa na kiuchumi yaliyowakabili kwa muda mrefu sasa.

Amesema wakati wa CUF kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar umefika, na kwamba hakuna mtu au chombo kinachoweza kukizuia chama hicho kushika dola katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Amewahamasisha wanachama hao kuendelea kuunga mkono hoja ya mamlaka kamili ya Zanzibar, kwani bila ya kufanya hivyo hakutakuwa na maendeleo wala uhuru wa Zanzibar wa kuweza kufanya na kusimamia maamuzi yake kitaifa na kimataifa.

Amefahamisha kuwa Zanzibar imepoteza umaarufu wake duniani baada ya kuungana na Tanzganyika, na kwamba wakati umefika sasa wa kuirejeshea heshima na umaarufu wake katika Jumuiya za Kimataifa.

Katika hatua nyengine wanachama ishirini wa chama cha ADC katika jimbo la Ole wamejitoa kwenye chama hicho na kujiunga na CUF.

Sambamba na hilo Maalim Seif alikabidhi kadi mia tano na hamsini na tano kwa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho katika jimbo hilo.

Ametoa wito kwa wanachama hao kuhakikisha kuwa wanapata vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi (ZAN ID) na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Nae mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Hamad Massoud Hamad amesema zaidi ya vijana mia nne na hamsini wenye sifa za kupewa ZAN ID katika jimbo hilo bado hawajapatiwa, na kwamba wamekuwa wakizungushwa bila ya kupatiwa haki hiyo.

Amewataka masheha wa jimbo hilo kutenda haki kwa kuwapatia ZAN ID vijana hao ambao wametimiza masharti yote ya kuweza kupata vitambulisho hivyo.

Kabla ya mkutano huo Maalim Seif alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya CUF katika kijiji cha Kangagani, iliyokwenda sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi katika tawi la Kosovo pamoja na kuzindua Barza ya Ukawa (Ukawa Centre) katika kijiji hicho.

Mapema akisoma risala ya wanachama wa barza ya Ukawa Centre, katibu wa barza hiyo nd. Ali Abdallah, amesema wameamua kuanzisha barza hiyo ili kuunga mkono maamuzi ya viongozi wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wanachi, ulioanzishwa wakati wa mchakato wa katiba mpya.

Hassan Hamad (OMKR)
 

0 comments:

 
Top