Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao wa Mawasiliano ya Teknolojia ya Kisasa ya ZTE imeahidi kuendelea kuunga mkono katika kusaidia maendeleo ya Nchi za Bara na Afrika ikiwemo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili zifikie hatua bora zaidi kwenye matumizi ya mfumo huo wa Teknolojia.

Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bwana Chen Jinsong alieleza hayo wakati akiuongoza Uongozi wa Kampuni yake kwenye mazungumza ya pamoja na Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Makao makuu ya Kampuni hiyo yaliyopo kwenye Mji wa Shengzhen Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.

Bwana Chen alisema China ina wajibu na kila sababu ya kuona utajiri, Fedha, rasilmali pamoja na Teknolojia iliyonayo inatumika katika kusaidia Mataifa rafiki ya Bara la Afrika ili yafikie hatua ya kujiendesha yenyewe Kisayansi na Teknolojia.

Makamu wa Rais huyo wa Kampuni ya ZTE ambayo tayari imeshafungua Tawi lake Dar es salaam Tanzania na Ofisi ndogo Zanzibar alisema ipo Bajeti maalum inayotengwa kila mwaka na kampuni hiyo katika kusaidia Bara la Afrika. “ Suala la kuunga mkono ni la msingi katika kusaidia nchi rafiki hasa zile zilizomo ndani ya Barala Afrika “, Alisema Bwana Chen Jinsong.

Alifahamisha kwamba Kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma za mawasiliano, afya zikiwemo shughuli za amali kupitia Teknolojia mpya katika kiwango kinachomuwezesha mwanaadamu wa kawaida kuwa na uwezo wa kupata huduma hizo.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inaendelea kuhitaji nguvu za msaada wa kitaaluma kutoka Jamuhuri ya Watu wa China katika kuimarisha uchumi wake. Balozi Seif aliueleza Uongozi wa Kampuni hiyo ya ZTE kwambaTaasisi yao iko huru katika kuitumia fursa ya uwekezaji iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuongeza miradi yao ya uwekezaji.

Wakati wa jioni ujumbe huo wa Zanzibar ulihudhuria chakula cha jioni kilichotayarishwa na wenyeji wao hao wa Kampuni ya mawasiliano ya mtanadao wa Tekonolojia ya kisasa ya Huawei.

Tafrija hiyo ilikuwa na burdani za aina yake iliyoambatana na muziki laini ya kiutamaduni uliotumbuizwa na wasichana warembo waliopendeza wa kampuni hiyo.

Cha kufurahisha zaidi kwenye tafrija hiyo ni ule umahiri wa mwana sanaa wa Jiji la Shengzhen Bwana Liu Qi Pei aliyeonyesha kipaji cake cha kuchora picha za ujumbe wa Zanzibar katika muda mfupi na kuwapa kama zawadi maalum ya kutembelea Kampuni hiyo.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ujumbe wake walitembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Kimataifa ya Mtandao huo wa mawasiliano ya Huawei iliyomo Mjini Shengzhen na kuona harakati zinazoendelea kufanywa na Kampuni hiyo.

Akizungumza na Uongozi wa Kampuni hiyo mara baada ya kukagua shughuli mbali mbali katika vitengo tofauti vya Taasisi hiyo Balozi Seif alisema Teknolojia ya Mawasiliano iliyopo hivi sasa ulimwenguni iko katika kiwango kikubwa kiasi cha kuifanya Dunia kuwa kama kiganja cha mkono badala ya Kijiji.

Balozi Seif alisema hatua hiyo ambayo inaonekana kutoa msukumo mkubwa kwenye maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii inaonekana kuwa ni hatua ya mafanikio kwamwanaadamu ikilinganishwa na karne nyingi zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kampuni ya Huawei kwa juhudi inazoendelea kuchukuwa katika kusaidia maendeleo ya Teknolojia ya mawasiliano { ICT } hasa katika sekta ya Elimu Nchini Tanzania ambayo imeshaonyesha muelekeo wa mafanikio.

Akitoa Taarifa fupi za shughuli za Kampuni hiyo ya Huawei Meneja mtandao wa mauzo wa Kampuni hiyo ambae ni Mtanzania Bwana Kenguka Kenguka alisema program ya elimu iliyoandaliwa na Kampuni hiyo hivi sasa iko katika hatua za mwisho kukamilika ambayo imelenga kutolewa katika skuli 10 za Tanzania.

Bwana Kenguka alieleza kwamba programu hiyo itakuwa rahisi kusambazika kwa haraka kutokana na ukaribu wa mashirikiano yaliyopo baina yake takriban na makampuni yote ya simu za mikononi yaliyopo nchini Tanzania.

Mtaalamu huyo wa masuala ya ICT aliueleza ujumbe huo wa Zanzibar kwamba mfumo huo wa Teknolojia ya Kisasa kwa kiasi kikubwa unasaidia kuunganisha uimarishaji wa uchumi na maendeleo.

Bwana Kenguka alitolea mfano hai uliopo wa maendeleo hayo ya kiuchumi katika suala la ajira ndani ya Kampuni hiyo ambapo tayari zaidi ya wafanyakazi Laki 150,000 wameajiriwa na Kampuni hiyo jambo ambalo limeimarisha nguvu za kiuchumi kwa upande mmoja.

Naye kwa upande wake Naibu Rais wa Kampuni ya Huawei Bwana Daniel Zhang alisema taasisi yake itaendelea kutoa msukumo katika kutoa huduma za mitandao ya mawasiliano kwa Nchi mbali mbali Barani Afrika.

Bwana Zhang alisema ipo miradi tofauti ikiwemo ya Elimu na Umeme wa kutumia jua iliyobuniwa na kupendekezwa na Uongozi wa Kampuni hiyo iwekezwe katika baadhi ya nchi za Afrika. Balozi Seif na Ujumbe wake amekamilisha ziara yake katika Kisiwa cha Jimbo la Hainan kwa kupitia katika Mji wa Shengzhen na Guanzhou ambapo atamalizia ziara hiyo katika Mji Mkuu wa Jamuhuri ya Watu wa China Beijing.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top