Makamu wa Pili wa Rais wa Zanbzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuendeleza utafiti pamoja na utoaji wa huduma za ufuatiliaji kwa wazalishaji wa sekta za mifugo na uvuvi, ili wazalishaji hao wawe na uwezo wa kupata faida kubwa, jambo ambalo litawafanya wananchi wengine hasa vijana kuendelea kujiajiri katika sekta hizo muhimu.

Alisema dira ya Serikali kuhusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi ni kuibadililisha Sekta hiyo kutoka katika mfumo wa uzalishaji wa kujikimu hadi kufikia kilimo cha biashara ifikapo mwaka 2020. 

Balozi Seif alisema hayo wakati akifunga Mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika Ukumbi wa Baraza hilo uliiopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema azma hiyo itafikiwa kwa mkakati wa kuimarisha hali ya uchumi na kijamii kwa wazalishaji wa mifugo na wavuvi kuwekewa mazingira mazuri ya utekelezaji, kupatiwa huduma za kitaalamupamoja na kuongeza thamani na upatikanaji wa taarifa za masoko ili kuongeza uzalishaji na kipato.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba ongezeko kubwa la mahitaji ya soko la utalii nchini ambalo ni mtumiaji mkubwa wa bidhaa za mifugo na samaki, sambamba na ongezeko la watu mijini limesaidia kukua kwa sekta ya mifugo na uvuvi nchini kulikosababisha kuimarika kwa soko la ndani. 

“ Suala la utafiti ni kikwazo kwa sekta zetu hizi, kuanzishwa kwa idara ambayo pia inasimamia suala la utafiti haitoshi, bali kuwepo kwa taasisi zinazojitegemea kushughulikia utafiti kisekta ndio njia pekee ya kuweka mazingira mazuri katika masuala ya utafiti “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Serikali tayari imo katika mpango wa kufanikisha suala zima la vituo vya utafiti kwa kuanzia na sekta ya uvuvi kwa kushirikiana na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China pamoja na Kampuni ya KOICA kutoka Japani.

Alisema Serikali imo katika kuandaa mpango wa kuanzisha Chuo cha Uvuvi hapa Zanzibar kitakachosaidia taaluma kwa vijana kwa lengo la kupata ajira kupitia shughuli za uzalishaji mifugo na uvuvi licha ya kwamba sekta hizo zimekuwa muajiri mkubwa wa vijana

Balozi Seif alieleza kwamba mazingira mazuri ya kisera, sheria, kanuni na miongozo yataandaliwa ili kuifanya sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta endelevu, ufugaji wa ng’ombe pamoja na uwekezaji wa viwanda vya usarifu wa samaki na mifugo bila kuathiri mazingira.

Akigusia Kilimo Balozi Seif alisema SDekta hiyo inaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi walio wengi vijijini na mijini.

Alisema takriban zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wote hapa nchini wanategemea sekta ya Kilimo kwa kuendeleza maisha yao ambapo takwimu zinaleza wazi kwamba kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sekta hii ilichangia wastani wa asilimia 30 ya Pato la Taifa.

Balozi Seif alisema kwa Msimu wa Kilimo cha Mpunga cha Masika 2013/2014, jumla ya ekari 30,444 Unguja na Pemba zililimwa katika maeneo ya juu, sawa na asilimia 87 na ekari 1,736 zililimwa katika maeneo ya umwagiliaji maji sawa na asilimia 88 ya lengo lililowekwa.

Kuhusu suala la amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itaendelea kwa juhudi zake zote kusimamia amani na utulivu iliyopo na ni vyema viongozi na wananchi wakaongeza ushirikiano katika kufanikisha azma hii.

Alisema Taifa linajivunia hazina kubwa iliyojaliwa na Mwenyezi Mungu ya amani na utulivu ambayo ni nyenzo kubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi nchi hii. Hivyo, hakuna budi kwa kila mmoja kuilinda na kuidumisha hazina hiyo kwani ikivurugika hakuna hata mmoja miongoni mwetu mwa jamii atakaebaki salama.

Aliwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba Serikali chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein itajitahidi kuhakikisha kwamba inaimarisha utendaji na uwajibikaji katika Serikali na kuendelea kudumisha amani na utulivu.

Miswada minne ya Sheria katika Mkutano wa 17 wa Baraza hilko la Wawakilishi Zanzibar na kujadiliwa yakiwemo mawasli 48 ya wajumbe wa Baraza hilo yalijibiwa yakifuatiwa na maswali mengine 100 ya nyongeza.

Miswaada hiyo ni ule Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Wauguzi na Wakunga (uanzishwaji wa Baraza la Usajili wa Wauguzi na Wakunga) Nam. 9 ya mwaka 1986 na kuanzisha badala yake Sheria mpya ya Wauguzi na Wakunga na Mambo Yanayohusiana na Hayo.
Mwengine ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Shirika la Nyumba la Zanzibar, Mswaada wa Sheria ya Baraza la Manispaa Nam. 3 ya mwaka 1995 na Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Miji Nam. 4 ya mwaka 1995 na kuanzishwa upya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2014 kwa madhumuni ya kuanzisha Serikali za Mitaa, uwezo wake, kazi na wajibu, muundo, mpangilio, fedha na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.

Mswada wa Nne uliowasilishwa unahusu kufuta Sheria Nam. 1 ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1998 na kuanzisha Sheria mpya ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 2014 na Mambo Mengine yanayohusiana na Hayo.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi siku ya Jumatano, tarehe 21 Januari, 2015 saa 3.00 asubuhi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top