Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema kitendo cha Diaspora kuamua kuwekeza Zanzibar ni mwanzo mzuri wa kuitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuwataka Wazaliwa wa Zanzibar walioko nje ya nchi kuanzisha miradi ya kijamii nyumbani kwao.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati wa hafla maalum ya kuzindua Hospitali ya Jamii inayosimamiwa kwa pamoja kati ya Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda wakishirikiana na Vijana wa Diaspora wenye asili ya Zanzibar hapo pembezoni mwa majengo ya Kiwanda cha Sukari Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema hatua ya wawekezaji hao walioamua kuanzisha miradi ya kijamii katika sekta ya afya umekuwa wakati muwafaka kwa vile unakwenda sambamba na azma ya Serikali Kuu ya kuimarisha sekta ya afya nchini.

Balozi Seif alisema hospitali hiyo itakayokuwa ikitoa huduma za matibabu mbali mbali kwa mchango mdogo itasaidia wafanyakazi wa kiwanda cha sukari Mahonda sambamba na Wananchi walipo pembezoni mwa kiwanda hicho.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuyakaribisha na kuyatia moyo makundi ya Diaspora ili yaendelee kuwekeza katika miradi tofauti kwa lengo la kusaidia ndugu,jamaa na wazazi wao.

“ Mchango wa Kiwanda cha Sukari kilichoshirikiana na Diaspora hao kimeisaidia Serikali katika sera zake za kuwa na kituo cha afya kila baada ya kilomita tano hapa nchini “. Alisema Balozi Seif.

Aliwakumbusha na kuwanasihi wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao kwa kuitumia hospitali hiyo yenye huduma na wataalamu waliobobea katika kufahamu afya zao.

Balozi Seif alisema si vyema kwa watu kusubiri maradhi yakajichomoza wakati ambao inakuwa vigumu kwa madaktari na wataalamu wa afya kuyatibu maradhi hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kiwanda cha sukari Mahonda kwa ustahamilivu wake mkubwa kutokana na changamoto nyingi walizopambana nazo hasa suala gumu la mashamba ya miwa ambalo lilikuwa likivamiwa mara kwa mara na mifugo pamoja na baadhi ya wakulima.

Alisema changamoto hizo zilizikuwa zikisababishwa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa kwa lengo la kujijengea ngome za kupata kuungwa mkono na wananchi hasa wakulima hao wakati wa changuzi mbali mbali.

Alieleza kwamba Serikali kupitia watendaji wake ilikuwa ikichukuwa juhudi za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kwa njia za mazungumzo hagtua ambayo inaonekana kufanikiwa kwa kiwango kikubwa hivi sasa.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatanabahisha wananchi hasa wakulima wa pembezoni mwa mashamba ya miwa kwamba hatua waliyokuwa wakiichukuwa kulima mpunga na viazi katika mashamba ya miwa ilikuwa ni makosa.

Alisema Serikali iliamuwa kukaribisha wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuwekeza miradi yao ambao kwa asilimia kubwa husaidia kutoa ajira kwa wananchi sambamba na kuongeza mapato ya Serikali.

Mapema Mwenyekiti wa Diaspora ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Jamii Mahonda Dr. Ameesh Metha alisema huduma zitakazotolewa kwenye Hospitali hiyo zitamuwezesha hata mwananchi wa kawaida kumudu kuchangia.

Dr. Metha alisema Hospitali hiyo itakayohudumia Wafanyakazi wa kiwanda pamoja na wancnhi wa vijiji vya jirani inaanzia na huduma za Xray, Uchunguzi wa Tumbo {Utra sound }, dawa za maradhi mbali mbali na maabara.

Alisema huduma nyengine muhimu kama uchunguzi wa figo,huduma za Meno, Macho na mazoezi ya viungo zinatarajiwa kutolewa baada ya miezi sita kuanzia sasa.

Mganga Mkuu huyo wa Hospitali ya Jamii Mahonda alifahamisha kwamba Uongozi wa Hospitali umejipanga kufunguwa huduma za matibabu mbali mbali katika Vijiji vya Nungwi na Kiwengwa miezi michache ijayo.

Dr. Amesh Metha amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwa busara zake za kufikiria kuanzisha Diaspora hapa Zanzibar.

Alisema uamuzi huo umesaidia kutoa fursa, changamoto na ushawishi kwa Wazanzibari na Watanzania walioko nje ya nchi kuhamasika na kushawishika kutaka kuwekeza nyumbani kwao hapa nchini.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top