Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kushinda uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka kesho ili Serikali inayoongozwa na Rais wa Sasa wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein imalize kipindi chake cha Pili.

Balozi Seif alisema hayo katika Mkutano wa hadhara wa Wanachama wa CCM Jimbo la Koani uliofanyika Kiwilaya hapo kwenye uwanja wa michezo wa Unguja Ukuu baada ya kutembelea ujenzi wa Ofisi za CCM Wadi na Matawi zilizomo ndani ya Wilaya ya Kati.

Alisema ushindi huo utapatikana na kuuzika kabisa upinzani usio na sera endapo wanachama wa chma cha Mapinduzi pamoja na Wananchi wote watapiga kura kwa kuendelea kuiunga Mkono CCM.

Balozi Seif alieleza kwamba mwaka 2015 ni kipindi muwafaka kwa chama cha Mapinduzi kuuzika upinzani unaoonekana kushindwa kuongoza dola tokea kuanzi kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania mapema katika miaka ya 90.

Alionyesha kuchukizwa kwake na tabia ya viongozi wa upinzani ya kujaribu kuupotosha umma kwa kumwita msaliti wa kuuza ardhi ya Zanzibar huko Tanzania Bara.

Balozi Seif alisema kitendo hicho cha udhalilishaji kinaonyesha dharau kubwa anayofanyiwa ambayo kwa sasa inastahiki kujibiwa kwa nguvu zote zinazostahiki dhidi ya wapinzani hao.

Akitoa ufafanuzi kwenye mkutano huo kuhusu suala la ardhi linavyopotoshwa na wapinzani ambalo wanalinakili kimakosa kupitia katiba iliyopendekezwa na bunge Maalum la Katiba Mjumbe wa Bunge hilo ambae pia ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban alisema hakuna kipengele kichoelezea ardhi ya Zanzibar kuhodhiwa na Muungano.

Mh. Shaaban alisema kilichomo ndani ya Katiba inayopendekezwa ni kumpya haki na fursa kila Mtanzania awe anatoka Zanzibar au Tanzania Bara kumiliki ardhi katika sehemu ya Jamuhuri ya Muungano endapo katiba hiyo itapita.

Alisema katika mfumo uliowekwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na haki ya kupanga au kusimamia matumizi ya ardhi yote iliyomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar wakati ile ya Bara itasimamiwa na Serikali ya Muungano mfumo ambao utampa haki Mtanzania ye yote kutumia ardhi hiyo.

Mapema Balozi Seif alikaguwa ujenzi wa Ofisi ya CCM Wadi ya Jumbi, Maskani ya CCM ya Mwera Pongwe, Tawi la CCM Mchangani, Tawi la CCM Bambi ya Bondeni pamoja na Tawi la CCM Kijundu.

Akiahidi kusaidia uwezekaji paa wa Tawi la CCM Kijundu na mifuko ya saruji kwa Tawi la CCM Mchangani Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa wanachama hao wa CCM Matawi na wadi mbali mbali Nchini kusimamia uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi katika Ofisi mpya wanazojenga.

Balozi Seif alisema mfumo wa Chama umeelekeza kwamba ofisi za Chama zinazojengwa kuanzia Maskani hadi mikoa lazima ziwe na miradi ya kiuchumi mpango ambao uawavua wanachama kuwa tegemezi kwenye miradi yao.

Aliwakumbusha wana CCM hao kujiandaa vyema na kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi aprili mwakani pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.

Alisema kazi ya ushindi wa Chama cha Mapinduzi itakuwa rahisi kutokana na umadhubuti wa chama chenyewe utaosimamiwa na wanachama na viuongozi wao.

Alieleza kwamba wakati CCM inamaliza kutekeleza ilani na sera zake kwa ufanisi mkubwa ulioshuhuidiwa na kila mtu, hivi sasa inajiandaa kutengeneza ilani nyengine mpya kwa ajili ya kuinadi wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka ujao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top