Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke alisema amani na usalama ndio njia pekee na ya msingi itakayoyavusha salama Mataifa mbali mbali ya Bara la Afrika katika kuimarisha uchumi na usawi wao.

Bwana Egon alieleza hayo wakati akijitambulisha rasmi alipokuwa na mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Egon Kochanke alisema mataifa mengi ya Bara la Afrika yamekosa fursa ya kuendelea na harakati za kujiletea maendeleo kwa kukumbwa na wimbi la vurugu na vita.

Alizitolea mfano Nchi za Somalia, Sudani ya Kusini pamoja na Nigeria ambazo zimekosa utulivu wa kisiasa kutokana na kukumbwa na vitendo vya uvunjifu wa amani likiwemo suala la Ugaidi linaloonekana kuitishia amani ya Dunia.

Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania alipongeza na kuridhika na mazingira mazuri ya Rasilmali na uwekezaji yaliyomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar jambo ambalo alisema atatumia nafasi yake ya Kidoplomasia Kuitangaza kwa Makampuni na mashirika ya Uwekezaji vitega uchumi ya Nchini kwake.

“ Nitachukuwa juhudi kama Balozi kujaribu kuyashawishi Makampuni na Mashirika ya Kijerumani kulitumia Soko la Zanzibar katika kuendeleza miradi yao kiuchumi na kibiashara “. Alisema Balozi huyo wa Ujerumani Nchini Tanzania.

Balozi Egon alifahamisha kwamba Zanzibar inaeleweka vyema Nchini Ujerumani kutokana na uzalishaji wake wa vyakula na bidhaa za Viungo ambavyo hupendwa na kuwa na watumiaji wengi duniani.

Katika kuunga mkono juhudi za Zanzibar katika kujinasua kiuchumi pamoja na kuimarisha soko la Ajira Balozi Egon alifahamisha kwamba Serikali ya Ujerumani itaandaa mipango maalum wa kutoa mafunzo ya kazi za amali kwa vijana wa Kizanzibari.

Alisema mpango huo utakaoendeshwa Nchini Ujerumani utajengewa mazingira ya kwenda sambamba na kuwaalika wataalamu wa sekta mbali mbali Zanzibar kupata fursa ya kutangaza mazingira na vivutio vya uwekezaji vya Visiwa vya Zanzibar kwa taasisi na makampuni ya Nchi hiyo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiomba Ujerumani kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika harakati zake za kuimarisha uchumi na maendeleo ya ustawi wa Jamii.

Balozi Seif alisema Serikali hivi sasa inaendelea kuimarish miundo mbinu katika sekta mbali mbali za kiuchumi ikilenga zaidi uimarishaji wa kilimo ambacho huchukua zaidi ya asilimia 80% ya wananchi wote Nchini Tanzania.

Alisema ili kufanikisha sekta hiyo zana za kisasa kama Matrekta yatahitajika katika kuwawezesha wakulima wengi hasa vijijini kuongeza uzalishaji utaozingatia taaluma ya kisasa kwa lengo la kuondokana na kilimo cha asili chenye mapato madogo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Balozi huyo wa Ujerumani Nchini Tanzania aliwaomba wawekezaji, mashirika na Taasisi za Ujerumani kujenga viwanda mbali mbali vitakavyookoa mazao ya kilimo mashambani.

Alisema Zanzibar ni kituo kikubwa cha biashara ndani ya ukanda wa Bara la Afrika ambacho wawekezaji hao wanaweza kukitumia jambo ambalo pia watapunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wanaomaliza masomo yao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top