Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mafungamano yaliyopo ya Kibiashara baina ya Zanzibar na Mataifa ya Ghuba na Mashariki ya mbali yatazidi kuimarika kufuatia kuongezeka kwa mawasiliano ya safari za anga kati ya pande hizo mbili.

Alisema mafungamano hayo ambayo yanaonekana kulenga zaidi katika sekta ya biashara pia yatafungua milango kwa sekta ya utalii inayoonekana kusaidia uchumi wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizindua safari za anga kati ya Dubai na Zanzibar zilizoanzishwa rasmi na Kampuni ya Kimataifa ya usafiri wa ndege ya Flydubai hafla iliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume Zanzibar.

Alisema wafanyabiashara wengi wa Zanzibar pamoja na Mwambao wa Afrika Mashariki wamekuwa wakilitegemea sana soko la Dubai ambalo ndilo wanalolitumia kwa kupata biadhaa zao.

Balozi Seif alieleza kwamba uanzishwaji wa safari hizo za moja kwa moja kati ya Dubai na Zanzibar utakuwa kiungo kizuri kwa wafanyabiashara hao kuendeleza biashara zao kwa kiwango kikubwa zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba uimarishaji wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar unaoendelea hivi sasa umelenga kutoa huduma zinazokubalika Kimataifa.

Alisema mkakati zaidi umewekwa katika kuona uwanja huo unakuwa na mazingira rafiki ya kushawishi mashirika mbali mbali ya ndege ya kimataifa yanaridhika na ubora wake na kuamua kuutumia kwa kupata huduma kwenye uwanja huo.

“ Uwanja wetu tulilenga utoe huduma za moja kwa moja kati ya Zanzibar na Mataifa mengine ya Ghuba, Mashariki ya Kati na Ulaya. Hivi sasa tumeanza kupata faraja kwa kuona mashirika ya ndege ya Ethiopia, Qatar na Oman yanatumia fursa hiyo “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Kampuni ya Kimataifa ya Flydubai kupitia Makamu wa Rais wake kwa uamuzi wake wa kuanzisha safari hizo za ndege kati ya Dubai na Zanzibar.

Alisema uwamuzi wa Kampuni hiyo umekuja wakati muwafaka kwa vile utaipa fursa zaidi Uongozi wake kuangalia soko la Zanzibar ambalo ni kituo cha bishara katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa karne nyingi zilizopita.

Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi huo wa Kampuni ya Flydubai kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa kila msaada ili kuiwezesha Kampuni hiyo kufanya kazi zake kama ilivyokusudia.

Akitoa taarifa ya Kampuni ya usafiri wa ndege ya Flydubai Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bwana Sudhir Screedhara alisema kampuni yake tayari inaendelea kutoa huduma kwa karibu Miji 12 ya Mataifa ya Bara la Afrika.

Bwana Sudhir alisema mradi wao unaotumia ndege mpya za kisasa aina ya Boeing zipatazo mia moja umewekeza kiwango cha fedha karibu Dolla za Kimarekani Milioni Sitini { U$ 60,000,000 }.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Flydubai ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kukubali kwake kuunga mkono uwamuzi wa Kampuni hiyo wa kutoa huduma za usafiri wa ndege kati ya Dubai na Zanzibar.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara inayohusika na Mawasiliano itakuwa makini katika kuhakikisha miradi yote inayohusu sekta hiyo inasimamiwa vyema.

Alisema uanzishwaji wa safari hizo za ndege za Flydubai utasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaongiza Zanzibar kufikia Milioni 2.0 kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2025.

Dr. Juma alieleza faraja yake kwamba wasafiri ndege ndani ya kanda ya Afrika Mashariki watapata fursa na uwezo wa kuunganisha safari zao za moja kwa moja katika nchi nyengine Duniani kwa kutumia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

Ndege ya Kampuni ya Flydubai ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amaani Abeid Karume Saa 8.00 kamili mchana na kurushiwa maji na gari za Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar kama ishara rasmi ya kukaribishwa ndani ya ardhi ya Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top