Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi wa Kidini wanapaswa kuwa macho katika kuzikataa choko choko zozote na ushawishi unaotolewa na wanasiasa kwa kuzingatia maslahi yao badala ya manufaa ya Taifa zima.

Alisema kazi kubwa inayotakiwa kufanywa na Viongozi hao wa Kidini ni kuwaombea watu wakiwemo Viongozi wa Nchi ili Baraka ziongezeke ndani ya Taifa pamojana umma jambo ambalo litasaidia kupunguza misuguano.

Balozi Seif alisema hayo wakati akilifungua Tamasha la Kuliombea Taifa na Kuhamasisha amani linalofanyika katika Ukumbi wa Masai Laugwa uliyopo Wilaya ya Magamoyo Mkoani Pwani.

Alisema mifarakano au choko choko zinapotokea kwa upande wowote ule Viongozi wa Kidini lazima wawe tayari kupatanisha na sio kutumia dhamana yao kuwa wararuaji huku wakielewa kwamba kazi wanayofanya ni wito kutoka kwa Muumba wao.

Balozi Seif alieleza kwamba amani na utulivu wanaojivunia Watanzania walio wengi kwa miaka mingi sasa ni miongoni mwa neema zinazopaswa kutumiwa vizuri na wananchi wa rika zote.

Alisisitiza kwamba njia nzuri ya kuzitumia neema hizo ni kwa wananchi kuzidisha juhudi katika uzalishaji mali Viwandani na Mashambani, kuzidisha upendo na mshikamano bila ya kujali rangi, kabila au asili ya Mtu.

Aliitahadharisha jamii kutotoa nafasi kwa wale wenye nia mbaya ya kutaka kuliangamiza Taifa katika kulitumbukiza kwenye vurugu na mapigano yalisiyokuwa ya msingi ambayo yanaweza kuepukwa.

“ Mimi kama Kiongozi wa Serikali kwa kushirikiana na viongozi wenzangu na wananchi wenye nia njema na Taifa letu tutaendelea kufanya kazi wakati wote na tutahakikisha kuwa amani na utulivu vinadumu ndani ya nchi yetu ambayo ndio maisha yetu “. Alisema Balozi Seif.

Alitoa wito kwa akina mama Nchini kuendelea kuwa walinzi nambari moja katika kusimamia amani na utulivu na kuwaona maadui wale wote wenye nia na dhamira ya kutaka kusababisha vurugu.

Balozi Seif aliongeza kwamba mara nyingi wanawake na watoto ndio wanaofanywa wahanga wakubwa wakati yanapotokea mapigano au vurugu zozote katika Jamii inayowazunguuka.

“ Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia kwenye vyombo vya habari sehemu mbali mbali duniani jinsi wanawake na watoto wanavyokufa au kujeruhiwa kutokana na vita vinavyozuka katika maeneo yao “. Alionya Balozi Seif.

Akizungumzia suala la dawa za kulevya linaloonekana kuwa tishio kwa kundi kubwa la vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali imekuwa ikichukuwa juhudi kubwa katika kupambana na janga hilo.

Alifahamisha kwamba Serikali zote mbili zimekuwa zikichukuwa hatua za makusudi kwenye viwanja vya Ndege na Bandari kwa kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu hali inayoonyesha kupungua kwa uingiaji huo wa Dawa za kulevya hapa Nchini.

Balozi Seif aliwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi ili kuwabaini wahusika wakuu wa mtandao wa biashara hiyo kwa lengo la kutokomeza kabisa biashara hiyo haramu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kanisa la Restoration kwa jitihada unazochukuwa za kuokoa maisha ya vijana walioathirika na dawa za kulevya.

“ Mafanikio ya Kituo hicho kilichoanzishwa na Restoration Bible Church hayakuwa binafsi kwa kanisa hilo tu bali yamekuwa ni mafanikio yetu sisi sote hapa Nchini “. Alisisitiza Balozi Seif.

Alieleza kwamba kitendo cha Kanisa hilo cha kuanzisha kituo cha kulelea watoto wenye kuishi katika maisha hatarishi kinafaa kuungwa mkono na jamii yote na yeye aliahidi kwamba atakuwa tayari kusaidia nguvu katika kuimarisha malengo ya kituo hicho.

Mapema Askofu Sedrick Ndonde wa Kanisa la Restoration { Restoration Bible Church } alisema Taifa hivi sasa limekuwa na cheche hatarishi inayoonekana kuchochea choko choko za Kidini, kisiasa pamoja na vitendo vya kigaidi.

Alisema hali hiyo yenye kwenda sambamba na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya inasababisha mfumko wa uhalifu unaowafanya wananchi waendelee kuishi katika maisha ya mashaka na hofu.

Askofu Sedrick Ndonde alitahadharisha zaidi kwamba hofu imetanda kutokana na uripuaji wa mabomu, umwagiaji watu tindi kali pamoja na matumizi ya silaha za moto vitendo vilivyoleta madhara kwa watu na wengine kupoteza dunia matendo yanayoashiria kuporomoka kwa hali ya amani hapa Nchini.

Alifahamisha kwamba baadhi ya watu wamekosa uzalendo kwa kutaka kunufaisha matundo yao. Hivyo ni vyema kwa Jamii isikubali amani iliyopo nchini ikachezewa na kuyayuka kama barafu.

Aliwaasa Watanzania na kuwatahadharisha wajifunze jinsi amani ilivyotoweka katika baadhi ya mataifa duniani zikiwemo nchi tofauti za Bara la Afrika baada ya baadhi ya watu ndani ya nchi hizo kushabikia chochezi na vurugu zilizozaa vita na majanga.

Akigusia uanzishwaji wa kituo cha kuhudumia watoto wenye mazingira hatarishi Askofu Sedrick Ndonde wa Kanisa la Restoration alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwake.

Alieleza kwamba Uongozi wa Kanisa hilo una kiu ya kubadilisha tabia za watoto wanaopelekwa kwenye kituo hicho kuwa waongofu wajibu ambao wataendelea nao katika kutekeleza kazi ya Mungu.

“ Kituo chetu kilichoanzishwa mwaka 2010 kinatoa huduma za malazi, chakula pamoja na ada za skuli kwa watoto wanaobadilishwa tabia kazi ambayo inakwenda kwa mafanikio makubwa na kukubalika na jamii “. Alisema Askofu Sedrick Ndonde.

Askofu Sedric Ndonde ambae pia ni Makamu Askofu Mkuu wa Restoration Bible Church Tanzania amewahakikishia waumini wa Dini ya Kikristo na wananchi wote Tanzania kwamba Tamasha hilo lililozinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif la kuliombea Taifa Amani litakuwa likiendelea katika Mikoa mbali mbali hapa Nchini.

Tamasha hilo lilipamba kwa njimbo mbali mbali zilizotayarishwa na kwaya za madhehebu mbali mbali wakiongozwa na waimbaji maarufu wa nyimbo za injili akiwemo Noel Pascol,Stela Joel pamoja na Dr.Magret Sdoris Kongera.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top