Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar imeagizwa kuchukuwa tatua za dharura za kuifanyia matengenezo makubwa Bara bara ya Donge Mtambile hadi Muwanda pwani ili kuwapunguzia usumbufu wa muda mrefu wanaoupata Wananchi wa eneo hilo hasa wakati wa mvua.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Wananchi wa Donge Mchangani na Muwanda katika Mkutano wa kupokea kero za Wananchi hao uliofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Muwanda.
Balozi Seif alisema nia ya Serikali Kuu ni kuhakikisha kwamba maeneo yote Mijini na Vijijini yanatengenezewa miundo mbinu mizuri ya bara bara na Mawasiliano ili kuyajengea mazingira murwa na uwezo wa uzalishaji maeneo hayo.
Alisema vijiji vya Donge Muwanda na Mchangani vimebarikiwa kuwa na ardhi ya rutba inayozalisha vyakula vingi vya mizizi, mboga mboga na nafaka hivyo juhudi za Serikali zitahitajika kufanywa ili kuwajengea mfumo mzuri wa bara bara wakulima wa maeneo hayo kupelekea mazao yao kwenye masoko.
Alieleza kwamba Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano italazimika kutekeleza kazi hiyo kwa hatua ya awali ya uwekaji Kifusi ili kupunguza mashimo wakati nguvu za muda mrefu zitawekwa katika kuiwekeza lami na kudumu kwa kipindi kirefu zaidi.
“ Nia ya Serikali Kuu wakati wote ni kuona inatengeneza bara bara zote kuu na hata zile zenye kuelekea kwenye maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara “. Alisema Balozi Seif.
Aliwapongeza Wananchi wa Vijiji hivyo viwili kwa ustahamilivu wao wa muda mrefu waliouonyesha kutokana na ukosefu wa miundo mbinu ya bara bara na kuwashukuru kwa kazi kubwa wanaoendelea kuichukuwa katika kuimarisha mazao ya kilimo.
Akigusia suala la uharibifu wa mazingira unaoonekana kuikumba mno Wilaya ya Kaskazini “B “ Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaomba wananchi wa Wilaya hiyo kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana pamoja na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Balozi Seif alisema kasi ya uchimbaji wa mchanga ndani ya Wilaya ya Kaskazini “ B” hivi sasa inatisha jambo ambalo itafikia wakati wakulima ndani ya Wilaya hiyo kukosa maeneo ya kilimo yenye rutba.
Alifahamisha kwamba kutokana na kasi hiyo anatarajia kuiagiza Idara ya Misitu na mali zisizorejesheka Zanzibar kupunguza kasi ya utoaji wa vibali vya uchimbaji mchanga katika Wilaya ya Kaskazini “ B “.
Balozi Seif aliongeza kwamba kasi ya uchimbaji mchanga hivi sasa inahatarisha hata miundo mbinu ya umeme inayopelekea baadhi ya nguzo za waya mkubwa wa huduma hiyo kuwa hatarini kuanguka.
“ Uchimbaji wa mchanga kwa jinsi ulivyoshamiri hivi sasa kwa kisingizio cha mchanga wa Kakaskazini “ B “ ni mzuri na bora kwa ufyatuaji matofali kuliko pengine popote pale hapa Zanzibar unahatarisha hata nguzo kubwa za miundo mbinu ya umeme kuanguka “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Kuhusu Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mchakato huo hivi sasa unaendelea vyema katika Mbunge Maalum la Katiba mjini Dodoma na matarajio makubwa ni kukamilika ifikapo Oktoba 4 Mwaka huu.
Balozi Seif aliwanasihi Wananchi watakapopelekewa Katiba Mpya waiunge mkono kwa kuipigia kura kwa vile mfumo wa muundo wa Katiba uliopendekezwa na Wabunge walio wengi ndani ya Bunge hilo ndio wenye muelekeo wa kulinda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo kwa karibu miaka 50 sasa.
Alisema nje ya muundo huo uliopendekezwa na wengi kwa hali halisi ya siasa ya Tanzania inavyotaka kupelekwa na baadhi ya wanasiasa ni kutaka kuhatarisha Muungano uliopo sasa.
Mapema akisoma Risala ya Wananchi hao wa Vijiji vya Donge Muwanda na Donge Mchangani Bwana Ahmed Abdulla alielezea changa moto zinazowakabili Wananchi hao katika harakati zao za kila siku.
Bwana Ahmed alizitaja changa moto hizo kuwa ni ubovu wa Bara bara yao, ukosefu wa huduma za Maji safi na salama, Deni la Kituo cha Ualimu, pamoja na ukosefu wa zana za kilimo na Trekta.
Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kulilipa Deni la Kituo hicho cha Ualimu la Shilingi Laki 9000,000 /-, kusaidia Kompyuta, mashine ya Foto Kopi pamoja na kuomba kupatia gharama za ujenzi wa vyoo vya Kituo hicho.
Pia Balozi Seif akaahidi kuvipatia mashine ya kusukumia maji kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo wana vikundi vya ushirika vya Vijiji vya Donge Mchangani na Donge Muwanda ikienda sambamba na kufuatilia tatizo la Maji safi na salama kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment