Mikoa Sita ya Kanda ya Kati ya Tanzania inatarajiwa kufaidika na huduma za Afya zilizolengwa kutolewa baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa Kimataifa wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida ambayo tayari mwaka uliopita imeshaanza kutoa huduma za akina mama na Watoto.

Hospitali hiyo yenye vitanda 1,000 vya kulazwa wagonjwa wa maradhi mbali mbali imeshatumia shilingi za Kitanzania Bilioni 68 katika hatua ya awali ya ujenzi wake ambapo kukamilika kwake itafikia gharama ya shilingi Bilioni Mia Tatu na Sitini na Moja.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dr. Dorothy Gwajima alisema hayo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akikagua harakati za maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo unaofanyika katika eneo la Mandewa Veta akiaga rasmi baada ya kumaliza jukumu lake la ulezi wa Mkoa wa Singida Kichama.

Dr. Dorothy alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mashirika Mawili ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF yameshajitokeza kuwekeza miradi iliyomo ndani ya ramani ya ujenzi wa Hospitali hiyo lakini kinachohitajika kwa sasa ni Serikali kusimamia dhamana ya miradi hiyo.

Alisema wazo la kuanzishwa kwa mradi huo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dr. Parseko Vicent Koni ni kuwapunguzia usumbufu wananchi wa kanda hiyo kufuata huduma za afya katika Hospitali ya rufaa Muhimbili iliyopo Jijini Dar es salaam.

“ Tunafarajika kwa kuwa na eneo kubwa la mradi wetu linalofikia Hekta 125 kiwango ambacho kwa mujibu wa ramani yetu tuna uwezo pia wa kujenga nyumba za watumishi, maduka, viwanja vya michezo na burudani pamoja na Skuli ya maandalizi na Sekondari “. Alifafanua Dr. Dorothy.

Akitoa pongezi kufuatia uanzishwaji wa mradi huo Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uwezo na kiwango kuwepo katika Hospitali hiyo kinaweza kutoa huduma pia kwa Watanzania wa maeneo mbali mbali.

Balozi Seif aliwaomba wasimamizi wa mradi huo mkubwa kutovunjika moyo na akaahidi kwamba akiwa kama kiongozi wa juu wa Serikali atahakikisha kwamba juhudi zitachukuliwa na Serikali ili kuona mradi huo unadhaminiwa ili ukamilike kwa wakati uliokusudiwa.

Aliushauri Uongozi wa Hospitali hiyo kuandaa mapema mipango itakayotoa fursa kwa washirika wa maendeleo hasa zile Hospitali kubwa za nje ya Nchi kushirikiana nao katika kuona huduma zitakazotolewa zinalenga kiwango cha Kimataifa.

Akitembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na shirika la Nyumba la Taifa Tanzania { NHC } katika Mtaa wa Mandewa Veta Mjini Singida Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri uongozi wa shirika hilo ujitahidi kuwapatia nyumba wananchi kwa bei nafuu.

Balozi Seif aliwanasihi wataalamu wa ujenzi wa nyumba hizo kuhakikisha kwamba nyumba wanazojenga zinalingana na mazingira halisi ya wananchi wa maeneo yanayohusika.

Mapema Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Tanzania { NHC } Ndugu Peter Buheja alisema mpango mkakati wa ujenzi wa mradi huo ni kujenga nyumba 15 ambapo hivi sasa tayari nyumba kumi zimeshajengwa.

Nd. Peter alisema changa moto zinazoukabili mradi huo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu unaotarakiwa kukamilika mwezi oktoba mwaka huu kwa gharama ya shilingi Milioni Mia 959,800,000/- ni pamoja na ukosefu wa bara bara pamoja na huduma za umeme.

Balozi Seif pia alikagua ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mtunduru na kuchangia shilingi Milioni 1,000,000/ na ahadi ya matofali 1,000 pamoja na ule ujenzi wa kituo cha afya cha Iyumbu alipochangia pia shilingi milioni 1,000,000/- kwa ununuzi wa saruji ikifuatiwa na ahadi ya Mabati 150.

Akizungumza na wananchi na wana chama wa CCM wa Wilaya hiyo ya Iyumbu katika Mkutano wa hadhara Balozi Seif aliwataka wakulima na Wafugaji wa maeneo ya Ikungi kushirikiana kwa vile mara nyingi huwa wakitegemeana katika shughuli zao za kila siku.

Alisema kumekuwa na migongano ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima na wakati mwengine kuleta maafa na mauaji jambo ambalo huzorotesha shughuli zao za uzalishaji pamoja na kujenga chuki baina yao.

Akigusia suala la elimu Balozi Seif aliwaasa wazazi wa Ikungi kusimamia jukumu la taaluma kwa watoto na kuacha tabia ya kuwashirikisha katika masuala ya ufugaji unaodumaza maisha yao ya baadaye.

“ Vijana hivi sasa waachiliwe kutafuta elimu hadi chuo kikuu kiwango ambacho kwa sasa ndicho kinachotazamwa katika masuala ya ajira “. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Alifahamisha kwamba suala la elimu hivi sasa ni jambo la lazima. Hivyo juhudi zifanywe ili kuona watoto wote hapa Nchini wanapatiwa haki yao ya kielimu itakayowatengenezea hatma njema ya maisha yao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top