Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amewahakikishia Wana CCM na Wananchi wa Mkoa wa Singida kwamba ataendelea kushirikiana nao wakati wote wa utumishi wake akiwa Kiongozi wa Kisiasa na Kiserikali licha ya kumaliza muda wake wa ulezi wa Mkoa huo Kichama.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Wilaya ya Manyoni katika Kijiji cha Chikuyu katika ziara yake ya siku tatu Mkoani Singida kuaga rasmi baada ya kumaliza Utumishi wake wa Kichama akiwa Mlezi wa Mkoa huo..

Alisema mlango uko wazi wakati wowote kwa Viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi Mkoani Singida kumualika katika shughuli yoyote ile ya Maendeleo itakayopangwa kuzinduliwa na yeye akiwa kama kiongozi mkuu wa Taifa hili.

Aliwashukuru Wananchi na wana CCM wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano mkubwa na wakaribu waliompa wakati akiwa mlezi wao ambao umemuwezesha kutekeleza kazi yake ya kuulea Mkoa huo kwa ufanisi na mafanikio makubwa .

“ Mkuu wa Mkoa au Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa mlango uko wazi wakati wowote ule kunialika katika shughuli zenu za maendeleo na mimi nitakuwa tayari kuzifanya “. Alisema Balozi.

Aliwataka wana CCM wa Mkoa wa Singida kuendelea kushikamana ili kujiandaa na maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 wakitambua kwamba kazi iliyopo mbele yao ni kuhakikisha Chama hicho kinaendelea kushika Dola pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Seif alisisitiza kwamba Wana CCM hao wanapaswa kuwa na tahadhari dhidi ya cheche za baadhi ya watu na wanasiasa hasa wale wa upinzani za kutaka kuwagawa wananchi kwa kutumia misingi ya ukabila na udini.

Alifahamisha kwamba Chama cha Mapinduzi ndio chama pekee kisicho na choko choko za udini na ukabila kutokana na sera zake za kusimamia amani na utulivu wa Taifa inayojenga mshikamano ambao uko mikononi mwa chama hicho.

Akizungumza na wana CCM wa Shina Nambari Moja la Jonathan liliopo Chikuyu Balozi Seif aliwapongeza wanachama hao kwa kuimarisha shina lao likiwa ni mfano ambao haujawahi kutokea katika maeneo mbali mbali Nchini Tanzania.

Alisema kitendo chao cha kuanzisha mfuko maalum unaotoa fungu la kuwalipa Balozi pamoja na baadhi ya wanachama wasio na uwezo kupata kadi ya Bima kwa ajili ya huduma za afya kimeleta faraja kwa Chama chenyewe.

Alisisitiza kwamba Chama cha Mapinduzi Taifa kinathamini uwepo wa ngazi ya shina katika chama hicho jambo ambalo nguvu na uhai wake huanzia kwa vile ndiko kwenye wanachama wenyewe.

Katika kuunga mkono juhudi za wana CCM hao wa Shina Nambari Moja la Jonathan Balozi Seif alichangia Shingili Laki Tatu kutunisha Mfuko wa Shina hilo kitendo ambacho kiliamsha ari na hamasa kwa baadhi ya viongozi waliokuwepo katika msafara wake kulazimika kufanya harambe iliyozaa mchango wa zaidi ya shilingi Laki Tisa.

Akigusia mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea Mjini Dodoma Balozi Seif alisema Wajumbe wa Bunge Maalum waliojigawa katika Kamati 12 hivi sasa wamemalizia mjadala katika sura 15 zilizomo ndani ya rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.

Balozi Seif aliwatoa hofu wana CCM na Wananchi hao wa Mkoa wa Singida kwamba wanaojadili rasimu hiyo ni wale wawakilishi wao waliowachagua katika majimbo yao wakijumuika na wenzao wa Taasisi,Jumuiya pamoja na makundi ya Kijamii ya wajumbe 201.

Alisema ile dhana inayoendelea kutangazwa na baadhi ya wanasiasa wasiotaka mchakato huo ufanikiwe ya kwamba mjadala huo unahusisha wajumbe wa chama kimoja tuu cha CCM ni hoja potofu inayopaswa kupuuzwa na kukemewa na Watanzania wote.

Mapema Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua Jengo jipya linalojengwa la maabara ya Skuli ya Sekondari ya Chikuyu iliyomo ndani na Wilaya hiyo ya Manyoni.

Akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi wa skuli hiyo Balozi Seif alisema Taifa linahitaji kuwa na wataalamu wa kutosha katika fani tofauti ikiwemo ile ya Sayansi ili kupiga hatua za haraka za maendeleo.

Alisema Viongozi wanapaswa kuongeza nguvu zao katika kuhakikisha watoto wao wanawajengea mazingira bora ya kielimu ili kuondokana na changa moto za Kielimu zinazowakabili watoto hao.

Balozi Seif alieleza kwamba mafunzo ya nadharia yanayoendelea kutolewa na skuli nyingi hapa nchini hasa zile za Sayansi hayafai kwa wakati huu uliopo wa mabadiliko ya sayanasi na teknolojia Duniani.

Naye Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mama Asha Suleiman Iddi aliwatanabahisha wana CCM na Wananchi wa Wilaya ya Manyoni kuachana na kasumba za wanasiasa wachache wanaotaka kuiona Tanzania inatumbukia ndani ya vurugu na fujo.

Mama Asha alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar chini ya usimamizi wa waasisi wa Sehemu hizo mbili Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ndio uliowafanya wananchi wa pande zote mbili kuwa ndugu wa damu.

Mama Asha na Mumewe waliwaahidi wananchi wa Chikuyu Manyoni kusaidia uwezekaji wa jengo la madarasa matatu ya Maabara za sayansi katika masomo ya Biology, Chemistry na Phisics.

Wakati wa usiku Balozi Seif na ujumbe wake walipata chakula cha usiku kilichoandaliwa na Uongozi wa CCM na Serikali ya Wilaya ya Manyoni hafla iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo na kushirikisha pia Wazee waasisi wa CCM wa Wilaya hiyo.

Akibadilishana nao mawazo viongozi hao Balozi Seif aliwaomba Wazee hao kuendelea kuwanoa watoto wao ili kuwaepusha na ushawishi unaofanywa na watu wasiowatakia hatma njema ya watoto hao.

Alisema Viongozi wengi wakiwemo rika yake wamefanikiwa vyema katika kuitumikia vizuri jamii inayowazunguuka kutokana na msingi mzuri walioupata unaotokana na waasisi wa Taifa hili.

Balozi Seif katika hafla hiyo alikabidhi Kompyuta pamoja na Printa yake akitekeleza ahadi aliyoitoa mwaka jana kwa kikundi cha Ushirika cha Malale Itigi wakati wa ziara yake Manyoni ya Magharibi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top