Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Wabunge na Viongozi wa Mkoa wa Singida kwa kazi kubwa wanazoendelea kuzifanya za kusimamia miradi ya Kiuchumi na ustawi wa Jamii ya wananchi wa Mkoa huo.

Amesema usimamizi huo umeufanya Mkoa huo kuongezeka harakati za maendeleo jambo ambalo wananchi walio wengi wameonyesha muelekeo mkubwa wa kujitegemea kimaisha.

Balozi Seif alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi michango na kupunuza ahadi alizozitoa wakati wa ziara yake ya hivi karibuni Mkoani Singida aliyoifanya rasmi kuaga kama Mlezi wa Mkoa huo Kichama.

Akikabidhi michango hiyo kwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mh. John Chiligati na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mh.Alhajj Misanga hapo nyumani kwake Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma Balozi Seif alielezea masikitiko yake kwa kuukosa ukarimu wa Wananchi wa Mkoa huo aliouzoea wakati wa ulezi wake.

Balozi Seif aliwakumbusha Viongozi na Wananchi wa Mkoa wa Singida kuendelea kushikamana na yeye atakuwa tayari kuongeza msukumo wake ili kuona maendeleo ya Kijamii yanazidi kukua na kustawisha ustawi wa jamii ya wananchi wa Mkoa huo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mh. John Chiligati alisema Balozi Seif Ali Iddi alifanya kazi kubwa iliyoleta mshikamanio wakati akiwa Mlezi wa Mkoa huo wa Singida.

Mh. Chiligati alisema Balozi Seif amekiacha Chama cha Mapinduzi imara ndani ya Mkoa wa Singida na wakaahidi kwamba malezi mema aliyoyaacha watajitahidi kuyaendeleza ipasavyo.

“ Ukweli tumesikitika kumkosa mlezi muadilifu aliyetuachia majonzi kutokana na uitendaji wake. Lakini hata hivyo tumemuwekea milango wazi awe huru kushauri na kusaidia harakati za maendeleo ya wananchi wa Singida “. Alisema Mh. John Chiligati.

Mbunge huyo wa Jimbo la Singida Masharik pia limpongeza na kumshukuru Mke wa Mlezi huyo Mstaafu wa Mkoa wa Singida Mama Asha Suleiman Iddi kwa msimamo wake wa kusimamia ilani na sera za Chama cha Mapinduzi Kivitendo.

Mh. Chiligati alimuelezea Mama Asha kuwa ni jasiri kutokana nay eye pamoja na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein kuuongoza Umoja wa wake wa Wabunge na Wawakilishi wa CCM Zanzibar ambao umeleta mafanikio makubwa hasa kwa akina mama na watoto.

Balozi Seif katika hafla hiyo fupi alikabidhi mchango wa shilingi Milioni moja na laki Tano kwa ajili ya ununuzi wa mabati ya kuezekea jengo la Mabara ya Skuli ya Sekondari ya Chikuyu iliyopo Wilaya ya Manyoni,shilingi 1,000,000/- za kununulia matofali kwa uendelezaji wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtunduru pamoja na shilingi 1,000,000/- kwa ajili ya Madrasa ya Muzdalifa iliyopo Ilongero.

Balozi Seif pia akakabidhi zawadi za Seti moja moja za Jezi na mipira minne kwa timu za soka na mpira wa pete wa Skuli ya Iyumbu pamoja na skuli ya msingi ya Ilongero.

0 comments:

 
Top