Amani ya Tanzania inaweza kuwa hatarini endapo tabia ya baadhi ya watu waliojichomoza kupiga debe ya kutaka kuungwa mkono na wananchi wawakubali wagombea urais wanaowataka wao kwa kuzingatia madhehebu ya Dini wanayoiamani itaendelea.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiendelea na ziara yake ya siku tatu Mkoani Singida akiaga baada ya kuwa mlezi wa Mkoa huo Kichama kwa kipindi cha miaka mitatu.
Akiwahutubia Viongozi wa Halmashauri Kuu za Wilaya za Singida Mjini, Ikungi, Singida Vijijini pamoja na Mabaraza ya Jumuia za chama hicho kwenye Bwalo la Chuo cha Utumishi Mjini Singida Balozi Seif alisema tabia hii yenye lengo la kutaka kugawa wananchi kitabaka inapaswa kuachwa mara moja.
Alisema Taifa wala Katiba ya Nchi kamwe haijaweka sheria, Muongozo wala utaratibu wa kuwezesha Rais kuteuliwa kwa kupokezana kulingana na madhehebu ya dini.
“ Hichi kigezo cha kubadilishana Urais kinachotumika hapa Nchini kinatokana na imani za Wananchi zinazopata Baraka na uwezo wa Mwenyezi Mungu “. Alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Rais anaweza kuchaguliwa kutoka kabila au madhehebu yoyote yaliyopo hapa Nchini, lakini kinachozingatiwa katika kumpa fursa hiyo ni uwezo wake unaompa nguvu kuweza kuwatumikia Wananchi.
Alielezea matumaini yake kwamba Chama cha Mapinduzi kitaendelea kushika Dola iwapo Viongozi pamoja na Wanachama wake watashikamana na kuepuka makundi yanayodhoofisha nguvu za Chama.
Balozi Seif aliwakumbusha wanachama na Viongozi hao kuunga mkono maamuzi ya Chama wakati wanaporejesha majina ya wanachama kugombea uongozi wa nafasi mbali mbali.
“ Tufikie wakati ndani ya chama chetu kuachana na ile tabia ya baadhi ya watu kung’ang’ania wagombea wanaowataka wao na kutokubaliana na maamuzi ya wengi jambo ambalo hatimae huleta vurugu na makundi “. Alinasihi Balozi Seif.
Aliupongeza Uongozi wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Serikali wa Mkoa wa Singida kwa jitihada unazochukuwa katika kutekeleza vyema ilani na Sera za Chama cha Mapinduzi.
Alisema uendelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo unaonekana kuongezeka mara dufu hasa katika miradi ya Elimu na Afya licha ya changamoto zilizopo katika miradi ya maji, umeme pamoja na ajira kwa Vijana.
Aliwasisitiza umuhimu wa Viongozi wa Mkoa huo wale wa Kisiasa na Kiserikali kuendelea kuwa na hamasa, ari pamoja na nia ya kuchangia maendeleo ya Wananchi wanaowaongoza.
Mapema Mke wa Mlezi huyo wa Mkoa wa Singida Kichama Mama Asha Suleiman Iddi aliwataka Viongozi wa Mkoa huo kuhakikisha kwamba Majimbo la Kata zote za Mkoa huo zinaongozwa na Chama cha Mapinduzi.
Mama Asha kazi hiyo inapaswa kuanzwa kufanywa na Viongozi hao hivi sasa na kuacha kushabikia viongozi waliyoonyesha nia ya kutaka kugombea Urais jambo ambalo linaweza kutoa fursa kwa vyama vyengine vya Siasa kupata nguvu zaidi za upinzani.
Aliwasisitiza Vionozi na wana CCM wa Mkoa huo kuibadilika zaidi katika kuchangia harakati za maendeleo ya Singida hasa katika kuwajengea uwezo zaidi watoto wa Kielimu.
Akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Kijiji cha Mkalakala ndani ya Wilaya ya Mkalama wakati wa jioni Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwaomba wanachama na wananchi hao kuzingatia suala la amani iliyopo hapa nchini.
Balozi Seif alieleza kwamba Historia ya Taifa hili inaonyesha wazi uwepo wa amani ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa zaidi ya miaka hamsini iliyopita nyuma.
Alifahamisha kwamba kutokana na muhumi wa kuendelea kuwepo kwa amani hiyo ndani ya ardhi ya Tanzania jamii lazima imlaani mtu ye yote anayesababisha na kuleta chokochoko hapa nchini.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wana CCM na Wananchi hao wa Kijiji cha Mkalakala Wilaya ya Mkalama kwamba akiwa kama kiongozi wa juu wa Serikali ataangalia uwezekano wa kusaidia vifaa kwa ajili ya Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Kijiji hicho.
Alisema Serikali itajitahidi kuongeza nguvu zaidi katika kuunga mkono jitihada za Wananchi kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo waliopo ndani na nje ya Nchi.
Akigusia mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea mkoani Dodoma Balozi Seif Ali Iddi aliwaeleza wananchi hao kwamba Katiba mpya iko njiani kupatikana licha ya baadhi ya wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kususia kujadili mchakato huo.
“ Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wanaoendelea na mchakato huo hawatakuwa tayari kuona wale waliosusia na kupinga watajaribu kutishia kuvuruga mchakato huo “. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopangwa Bunge Maalum la Katiba linatarajiwa kukamilisha kazi yake na rasimu itakayopendekezwa na Bunge hilo itawasilishwa rasmi kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Moh’d Shein Mwishoni mwa mwezo Oktoba mwaka huu wa 2014.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment