Zanzibar imeanza mikakati maalum ya kujiweka tayari kupambana dhidi ya janga la Kimataifa la kuibuka kwa maradhi ya Ebola endapo yataingia ndani ya visiwa vya unguja na Pemba maradhi ambayo tayari yameshazikumba nchi kadhaa za Afrika magharibi.

Mikakati hiyo imechukuliwa kutokana na mazingira halisi ya Visiwa vya Zanzibar kufungamana pamoja na maingiliano ya mara kwa mara kwa wageni kutoka nchi mbali mbali duniani kupitia sekta ya utalii inayoingiza wageni wengi.

Kikao cha Kamati ya Taifa ya kukabiliana na maafa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kilikutana kwa dharura Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kupanga mikakati itakayosaidia kukabiliana na janga hilo.

Wajumbe wa kikao hicho kilichotoa baraka ya kuundwa kwa kamati ndogo itakayoratibu mikakati hiyo chini ya uwenyekiti wa Wizara ya Afya wameelezea umuhimu wa kuendelea kutolewa elimu kwa wananchi itakayosaidia kujikinga na maradhi hayo hatari.

Walisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na shirika la Bandari, mamlaka ya Viwanja vya ndege, Idara ya Uhamiaji pamoja na taasisi nyengine ziendeleze uchunguzi na ufuatiliaji wa wageni wote wanaotoka katika nchi ambazo tayari ugonjwa huo umeshaathiri.

“ Utaratibu wa kutolewa elimu maalum kupitia vyombo vya Habari pamoja na magari ya sinema kwa kamati za maafa kuanzia Taifa hadi shehia juu ya ugonjwa huo unafaa kupewa msukumo wa dharura pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye bandari bubu “. Walisema wajumbe hao.

Baadhi ya wajumbe hao walishauri kujumuishwa kwa wawekezaji vitega uchumi mbali mbali waliopo hapa nchini ambao wana taaluma wa fani tofauti inayoweza kusaidia mikakati hiyo.

Walieleza kwamba utafiti ufanywe kuangalia sifa za wawekezaji hao ambao huziainisha kwenye mikataba yao wakati wanapoomba uwekezaji vitega uchumi vyao hapa nchini.

“ Tumeshuhudia baadhi ya wawekezaji hao wakati wa maafa ya kuzama kwa meli ya M.V Spice Island kwenye mkondo wa Nungwi walivyotusaidia kitaalamu pamoja na mawasiliano “. Alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya watembezaji watalii Zanzibar { ZATI } Simai Mohammed.

Kuhusu suala la ushiriki wa vyombo vya Habari katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa ebola Wajumbe hao walishauri watendaji wa vyombo hivyo kupatiwa semina maalum zitakazosaidia katika kutoka elimu hiyo kwa wananchi.

Walifahamisha kwamba wapo Wahariri na hata baadhi ya mitandao ya kijamii inaopenda kutumia matukio kama haya kueleza mambo yaliyo tafauti na uhalisia wa matukio yenyewe.

Ugonjwa wa Ebola uliogundulika mwaka 1976 Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo { DRC } na Sudan ni miongoni mwa ugonjwa hatari wa mripuko unaoenea kwa kasi na kusababisha vifo vingi kwa wakati mmoja.

Dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na homa, kuumwa kwa kichwa, kuumwa kwa misuli na viungo vya mikono na miguu, koo, kukosa nguvu za mwili na baadaye kufuatiwa na vipele katika ngozi, macho kuwa malegevu, kwikwi na hatimae kutokwa na damu katika tundu mbali mbali za mwili ikiwemo pua, masikio, mdogo na ngozi.

Ugonjwa huu wa Ebola hujichomoza baada ya virusi vyake kuenezwa kwa kupitia mnyama kwenda kwa binaadamu na binaadamu kwenda kwa mwengine mnyama popo akithibitika kuwa ndie chanzo kikuu cha ugonjwa huo.

Hadi sasa hakuna dawa wala chanjo maalum inayoweza kutibu ugonjwa wa Ebola lakini kinachofanyika kwa hivi sasa ni mgonjwa husika kupatyiwa matibabu ya kusaidiwa kutokana na dalili zilizojitokeza.

Mripuko wa ebola unaoendelea hivi sasa ulianza kugundulika mara ya kwanza nchini Guinea mnamo Tarehe 21 Marchi mwaka huu wa 2014 na baadae kuenea kwa kasi katika nchi jirani za Liberia, Siera Leone na Nigeri.

Hadi kufikia Tarehe 11/8/2014 jumla ya wagonjwa 1,975 wamegunduliwa kuambukizwa ugonjwa huo wakiwemo wafanyakazi wa afya 140 ambapo kati yao wagonjwa 1,069 na wafanyakazi 80 wa afya wamefariki dunia.

Shirika la Afya Ulimwenguni { WHO } Tarahe 8/8/82014 lililazimika kutangaza mripuko huo kuwa ni janga la Kimataifa la Afya la Kijamii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top