Serikali ya Uholanzi inakusudia kuongeza fursa zaidi za masomo kwa wanafunzi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupata taaluma ya juu kwenye vyuo vikuu mbali mbali nchini humo.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Bwana Jaap Frederiks wakati akibadilishana mawazo mbali mbali na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Jaap Frederiks alisema wapo wanafunzi wengi wa Kitanzania wanaohitaji kupata elimu ya juu baada ya kumaliza masomo yao ya sekondari lakini kinachowakwaza ni ufinyu wa kupata fursa kama hizo unaosababishwa na ukosefu wa ufadhili.

Balozi huyo wa Uholanzi aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuangalia sekta na maeneo ambayo Nchi yake inaweza kusaidia kitaaluma na hata uwezeshaji.

Bwana Jaap alifahamisha kwamba zipo fursa nyingi katika sekta ya elimu, mazingira, kilimo, ufugaji na hata mawasiliano nchini uholanzi ambazo kama kutakuwa na utaratibu muwafaka zinaweza kuifaidisha Zanzibar kiuchumi na ustawi wa jamii.

“ Zipo fursa nyingi za kitaaluma katika sekta za mazingira,kilimo, elimu na mawasiliano ambazo tayari Uholanzi imeshapiga hatua kubwa kiasi kwamba inaweza kusaidia mataifa yatakayohitajia taaluma hiyo“. Alisema Balozi Jaap.

Akigusia suala la sekta ya utalii Balozi Jaap alisema zipo dalili zinazoonyesha kwamba wawekezaji pamoja na watalii wengi nchini Uholanzi wameonyesha shauku ya kutaka kuitembelea Zanzibar.

Alisema shauku hiyo inatokana na hali halisi ya kimazingira na rasilimali zilizopo katika visiwa vya Zanzibar pamoja na ukarimu wa watu wake.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Uholanzi kupitia Balozi Wake huyo kwa jitihada inazochukuwa nchi hiyo katika kusaidia maendeleo ya Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Balozi Seif alitoa wito kwa wawekezaji na watalii wa Nchi hiyo kuendelea kutumia fursa iliyotolewa na Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya utalii na uwekezaji vitega uchumi.

Akizungumzia suala la uchaguzi Mkuu ujao mwa mwaka 2015 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimtoa hofu Balozi huyo wa Uholanzi kwamba Zanzibar itaendelea kuwa shuwari katika kipindi chote cha kampeni hadi uchaguzi kamili.

Alisema sheria na taratibu za uchaguzi zipo wazi na sahihi zinazotoa nafasi sawa kwa kila chama shiriki kwenye chaguzi hizo kufanya kampeni kwa kuzingatia kanuni za Tume ya uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } na zile za Taifa za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania { NEC }.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Dunia imeshuhudia uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2010 uliofanyika kwa amani baada ya maridhiano ya vyama viwili vikuu vya CCM na CUF vilivyoondosha hofu na wasi wasi uliokuwa umetanda katika chaguzi nyingi zilizopita.

“ Tunashukuru kwamba Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoendeshwa katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa inakwenda vizuri kiasi kwamba unaweza kushindwa kuelewa upi ni upande wa upinzani “. Alisema Balozi Seif.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulinda na kuheshimu haki ya kila mwananchi kupitia taratibu zilizowekwa kikatiba na kamwe haitakuwa tayari kuona baadhi ya watu wanajaribu kuichezea amani ya nchi iliyopo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top