Kampuni ya Mitandao ya simu za Mkononi ya Tigo imejitolea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta ya uwekezaji katika masuala ya mitandao ya mawasiliano sambamba na kusaidia huduma za Kijamii kwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake Mjini Stokholmes Nchini Sweeden Bwana Arthur Basting alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake katika Jengo la Msekwa ndani ya Viunga vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.

Bwana Arthur Basting ambae anasimamia Kampuni Tigo Barani Afrika alisema Uongozi wa Taasisi hiyo imejikita kutoa ushirikiano huo ikizingatia zaidi umuhimu wa mawasiliano ya Teknolojia yaliopo hivi sasa Ulimwenguni kote.

Bwana Arthur alisema Uongozi wa Kampuni ya Tigo unafurahia kuona kwamba Teknolojia ya Mawasiliano kupitia simu za Mikononi hivi sasa imeenea na kupokelewa vyema na wananchi wa Bara la Afrika.

Alisema kutokana na hatua hiyo Uongozi wa Taasisi hiyo umefikiria kuongeza kuhuduma zake mara dufu ndani ya Bara la Afrika ili kuona sekta ya mawasiliano inaendelea kutoa huduma katika masuala ya kijamii na uchumi.

Bwana Arthur alifahamisha kwamba mfumo ulioanzishwa na Kampuni hiyo wa huduma za kusafirisha fedha kupitia mtandao wa Simu za Kiganjani umeleta faraja kwa watu mbali mbali ukionyesha mafanikio makubwa ya kupunguka kwa unyang’anyi na wizi wa fedha baina ya watu au hata taasisi.

Naye Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Tigo Hapa Tanzania Bibi Sylvia Balwire alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Kampuni hiyo tayari imeanza mipango maalum ya kusaidia huduma za Kijamii katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Bibi Sylvia alisema Wataalamu wa Tigo hivi sasa wako katika hatua za mwisho kukamilisha mipango ya kusaidia uendelezaji wa mradi wa kilimo cha Mwani Kisiwani Pemba.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuomba Uongozi wa Kampuni ya Tigo kushirikiana na Kampuni ya Zantel katika kuona huduma za mitandao ya mawasiliano inazidi kuimarika.

Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Kampuni hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari wakati wowote kutoa ushirikiano wa karibu ili kuongeza nguvu zitakazoiwezesha Kampuni hiyo kutekeleza malengo iliyojipangia.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliusharui Uongozi huo kuongeza nguvu zake zaidi katika kusaidia miradi ya Kijamii ambayo bado inaonekana haijawa na nguvu za kujiendesha yenyewe.

“ Hadi wakati huu tunaozungumza zipo skuli zetu nyingi hazijawa na vikalio, huduma za maabara na Maktaba, hata vifaa katika vituo vyetu vya Afya. Uwepo wenu kama wawekezaji unaweza pia kuyaangalia maeneo hayo muhimu kwa ustawi wa Jamii yetu “. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alitoa mifano ya miradi hiyo ambayo inaweza kuongezewa nguvu na Kampuni hiyo ya Tigo kuwa ni pamoja na huduma za afya, Kilimo pamoja na Elimu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top