Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Wataalamu wa Ujenzi, Miundo mbinu pamoja na usanifu Miji ya Kisasa wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi { ECG } Kutoka Nchini Misri.

Ujumbe huo unaoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi hiyo Mhandisi Amr Alouba upo Nchini kuangalia maeneo ambayo unaweza kushirikiana na Zanzibar katika Sekta ya Uwekezaji.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar Kiongozi wa Ujumbe huo Mhandisi Amr Aloub alisemaTaasisi hiyo imeamua kuelekeza nguvu zake ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ili kusaidia miundombinu ya kuinua uchumi wa Mataifa hayo.

Mhandisi Amr alifahamisha kwamba Taasisi yake yenye kushughulikia ujenzi wa viwanja vya ndege, miji ya kisasa, vituo vya Kimataifa vya pamoja na usarifu wa majengo ya kibiashara imeshaamua kushirikiana na Zanzibar katika sekta hizo muhimu kwa uchumi wa Taifa.

Bwana Amr Alouba na Ujumbe wake ambae tayari ameshatembea maeneo Huru yaliyotengwa na Serikali pamoja na Mtaa uliotengwa Kibiashara wa Gulioni,kuelekea Kariakoo hadi Michezani { High Street } alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na maeneo mazuri kiuwekezaji jambo ambalo Kampuni yake imeridhina nayo.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Ujumbe huo kwa uwamuzi wake wa kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Balozi Seif alisema Zanzibar hivi sasa inahitaji kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya Viwanda, Uvuvi pamoja na maeneo mengine jambo ambalo Kampuni hiyo inaweza kuwa mshirika mkuu katika uimarishaji wa sekta hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo kwamba uanzishwaji wa viwanda vya kusindika samaki pamoja na utalii ulenga kusaidia kuongeza kasi ya uzalishaji uchumi sambamba na upatikanaji wa ajira kwa vijana.

Taasisi hiyo ya ushauri ya Uhandisi kutoka Nchini Misri Tayari imeshajenga Vituo Sita vya Kimataifa vya Kibiashara katika Nchi mbali mbali kama vile Qatar, Kuweit na wenyeji Misri, Sudan, Kenya pamoja na Tanzania Bara.

Mhandisi Amr Aloub amekuwa mshauri muelekezi aliyesimamia kujengwa kwa Kijiji cha Kibiashara cha Kimataifa kilichopo katika Mtaa wa Kadizani kwenye Mji wa Cairo Nchini Misri.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top